Tuesday 23 April 2013

WANA CUF 11 WAWANIA JIMBO LA CHAMBANI !!!


WANANCHAMA 11 wa Chama cha Wananchi (CUF) wamejitokeza kuwania ubunge katika jimbo la Chambani, liliko Kisiwani Pemba, kutokana na kifo cha mbunge wake, Salim Hemed Khamis.
Khamis alifariki Machi 28, mwaka huu, siku moja baada ya kuaguka ghafla wakati akihudhuria kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo, alisema jana kuwa mpaka jana mchana wanachama hao ndio waliokuwa wamejitokeza na kusema kuwa zoezi la kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo bado linaendelea.
Kuhusu maandalizi ya uchaguzi, Mketo alisema bado wanaendelea kujipanga na kwamba yataanza rasmi baada ya Baraza Kuu la chama hicho litakapokaa mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya kupitisha jina moja la mgombea.
“Kwa kuwa sisi ndiyo tunaotetea jimbo letu, tunaendelea na taratibu za chama kama zinavyowataka wanachama kuchukua fomu za kugombea, ili Baraza Kuu litakapokaa kuchagua mgombea mmoja na kuanza kampeni kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” alisema.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), uchaguzi katika jimbo hilo utafanyika Juni 16 mwaka huu na kwamba kampeni zinatakiwa kuanza Mei 18 hadi Juni 15 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment