Monday 8 June 2015

AKAAA AKUTANA NA MEYA RAIS WA NCHI ?AMA KWELI WAMESHAUZWA WAZANZIBAR

Hapa ndipo Zanzibar tulipofikishwa katika mfumo wa Muungano uliopo. Rais wa Zanzibar anakwenda katika ziara tuliyoambiwa ni ziara rasmi nchini Ujerumani lakini anaishia kukutana na Meya wa Wurzburg.
Zanzibar iliyokubali kuchanganya (na siyo kusalimisha) mamlaka yake kuhusu mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa na Tanganyika ili yasimamiwe kwa pamoja na inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maslahi na manufaa ya nchi zote mbili (Zanzibar na Tanganyika) leo haiwezi kutumia fursa zilizopo kuinua uchumi wake na kubadilisha maisha ya watu wake.
Tanganyika imevaa koti la Muungano na inazitumia kikamilifu fursa zote za mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa na Zanzibar inaishia kutembelea Meya. Ubalozi wa inayoitwa Jamhuri ya Muungano ambao unapaswa kuzihudumia Zanzibar na Tanganyika kwa usawa umeshindwa kusimamia maslahi ya Zanzibar na badala yake unaendeleza mahusiano ya kimataifa kwa maslahi ya Tanganyika tu. Huu si Muungano; ni Ukoloni.
Madalali wa CCM Zanzibar wanasema mfumo huu ndiyo unaoifaa Zanzibar na wakaona fakhari kutuuza Dodoma. Wazanzibari tutafanya maamuzi ya kuwahukumu Madalali hawa Oktoba 25, 2015. Lugha ni moja tu: DELETE, FUTA KABISA

Wednesday 3 June 2015

MAONI YA MSOMAJI KTK FACEBOOK KWA ZIARA YA RAIS SHEIN UGERUMAN !

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 03 Juni 2015 na ZANZINEWS yenye kichwa cha maneno "Dk Shein ziarani Ujerumani", mwandishi ameandika kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameondoka nchini leo kwenda nchini Ujerumani kwa ziara ya kikazi ya siku nane.
Akiwa nchini humo siku ya Alhamisi ijayo, Dk. Shein atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Muziki yanayofanyika katika mji wa Wurzburg pamoja na kuhudhuria utoaji wa zawadi kwa mwaka 2015. Zanzibar inashiriki katika Maonesho hayo yanayofanyika kila mwaka ambayo yanajumuisha wanamuziki na wasanii mashuhuri kutoka nchi za kiafrika pamoja na nchi za mabara mengine ulimwenguni.
Siku inayofuata Dk. Shein atakutana na kufanya mazungumzo na Mstahiki Meya wa Wurzburg na baadae atatembelea Taasisi ya Utibabu ya mji huo(Medical Mission Institute). Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ataendelea na ziara yake nchini humo ambapo siku ya Jumapili tarehe 07 Juni, 2015 atakwenda katika mji wa Frankfurt ambako jioni atakutana na watanzania wanaoishi nchini Ujerumani.
Siku inayofuata atakwenda katika mji wa Postdam ambako atatembelea skuli ya msingi ya Bruno-H-Burgel ambayo ina ushirikiano na skuli ya Mwanakwerekwe Unguja. Siku hiyo hiyo jioni atakutana na mabalozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walioko nchini Ujerumani. Tarehe 09 Juni, 2015 Dk. Shein atakutana na wanachama wa Chama cha Wafanyabiashara wa Ujerumani ambako atatoa hotuba rasmi.
Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana na mke wake, Mama Mwanamwema Shein; Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Mhe. Said Ali Mbarouk; Waziri wa Kilimo na Maliasili, Dk. Sira Ubwa Mamboya; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Dk. Mahadhi Juma Maalim; na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Wengine ni Mshauri wa Rais (Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa; na Katibu Mkuu wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko, Julian Banzi Raphael.
Dk Shein anatarajiwa kurejea nchini tarehe 10 Juni, 2015. Katika uwanja wa ndege wa Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliagwa na viongozi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi.
MAONI: Nimeisoma kwa makini kabisa Ratiba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Mohammed Ali Shein, kuhusu ziara yake uchini Ujerumani. Ikiwa ratiba hii ni sahihi, inasikitisha sana kuona kuwa hapana popote katika ratiba yake panapoonyesha kuwa Rais Shein atakuwa mgeni rasmi wa kiongozi yoyote wa ngazi ya juu wa Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani au hata kiongozi wa moja kati ya Landers (nchi) 16 za Ujerumani zinazofanya Shirikisho la Ujerumani. Kiongozi wa juu kabisa wa kisiasa ambaye Dk. Shein amepangiwa kukutana na kufanya mazungumzo naye ni Mstahiki Meya wa Wurzburg!
Kusema kweli, ikiwa hii ndiyo ratiba aliyopangiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika ziara yake huko Ujerumani, basi mimi kama ningelikuwa mshauri wake wa masuala ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ningelimshauri asifanye ziara hiyo huko Ujerumani. Ningelimshauri hivi kwa sababu iweje Rais mzima wa Zanzibar, tena akiongoza ujumbe uliyosheheni mawaziri na watendaji wa ngazi ya juu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, aridhike kukutana na kufanya mazungumzo na Meya wa Wurzburg na kutembelea taasisi ya utibabu, skuli, kuhudhuria ufunguzi wa maonyesho ya muziki, na kumalizikia kukutana na kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi nchini Ujerumani. Hivi kweli Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania imeshindwa hata kumpangia kukutana na kufanya mazungumzo mafupi na Rais wa Ujerumani, japo kwa maamkizi (courtesy call) tu? Inasikitisha sana.
Kwa hivyo, kama ratiba hii kuhusu ziara ya Rais wa Zanzibar nchini Ujerumani ni sahihi, basi hapana shaka yoyote ile kuwa Zanzibar inahitaji kupata mamlaka kamili.