Thursday 30 May 2013

MAPENDEKEZO YA KAMATI YA MARIDHIANO ZANZIBAR !!! SOMA UELEWEE EWEEE MZANZIBAR ,,,


Na Salmin Juma

MAPENDEKEZO YA KAMATI YA MARIDHIANO ZANZIBAR KUHUSU UPI UWE MWELEKEO WA WAZANZIBARI KATIKA KUIJADILI RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ITAKAYOTOLEWA NA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA

UTANGULIZI:

Baada ya wananchi wa Zanzibar kutoa maoni yao juu ya vipi Muungano wa Zanzibar na Tanganyika unapaswa kuwa, hatimaye Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatarajiwa kutoa rasimu ya awali ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwishoni mwa mwezi Mei na mwanzoni mwa mwezi Juni 2013. 

Wakati tunaisubiri kwa hamu rasimu hiyo itolewe na kujua kilichomo, sisi wajumbe wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar tumekaa na kutafakari juu ya upi unapaswa kuwa mwelekeo wa Wazanzibari katika kuijadili rasimu hiyo pale itakapotoka. 

Baada ya mashauriano ya kina kati ya wajumbe wa Kamati ya Maridhiano na pia kwa kuwahusisha watu wengine mashuhuri hapa Zanzibar, tumekuja na mapendekezo yafuatayo ambayo leo hii tunayawasilisha kwa wananchi wa Zanzibar kupitia Kongamano hili. Haya si maagizo bali ni mashauri yenu na pindi mkiyakubali basi tutakuombeni tuyafanyie kazi kwa pamoja kwa kuyatumia katika kuipokea na kujadili rasimu pale itakapotolewa. 

Mapendekezo yetu ni kama ifuatavyo:

1.Jina la Muungano:

Muungano huu umetokana na Jamhuri mbili kuungana kwa hiyari. Jamhuri hizo ni Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika. Jina la awali lililotajwa katika Mkataba wa Muungano la muungano wa jamhuri hizi mbili lilikuwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Jina hili baadaye mwezi Oktoba 1964 lilibadilishwa na kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ukiangalia mifano ya nchi nyingine zilizoungana, jina la muungano huweka bayana kwamba zilizoungana ni zaidi ya nchi moja, zaidi ya falme moja au zaidi ya jamhuri moja. Kwa mfano, muungano wa nchi (states) za Marekani unaitwa kwa kiingereza United States of America (USA), ule uliokuwa muungano wa jamhuri za kisovieti ukiitwa Union of Soviet Socialist Republics (USSR) na ule muungano wa falme za kiarabu unaitwa United Arab Emirates (UAE).

Ili kuondosha dhana iliyojengeka kwamba muungano wa jamhuri zetu mbili umeunda nchi moja na kuzifuta nchi zetu, Katiba Mpya inapaswa kuweka jina linalotambua msingi huo na historia hiyo. Hivyo basi, jina jipya liwe ni Muungano wa Jamhuri za Tanzania na kwa kiingereza United Republics of Tanzania.

Jina hili litasaidia utambulisho wa nchi wanachama katika uwanja wa kimataifa pale litapoambatanishwa katika nyaraka zote rasmi pamoja na jina la nchi husika. Kwa maana hiyo katika uwanja wa kimataifa na katika pasi za kusafiria utaweka wazi na kuwa na “UNITED REPUBLICS OF TANZANIA – REPUBLIC OF ZANZIBAR” na “UNITED REPUBLICS OF TANZANIA – REPUBLIC OF TANGANYIKA”.

2.Mipaka ya Zanzibar na Tanganyika:

Wakati zinaungana, Zanzibar na Tanganyika zilikuwa tayari ni nchi zenye mamlaka kamili zikiwa ni wanachama wa Umoja wa Mataifa na hivyo kila moja ilikuwa na mipaka yake inayoeleweka. Katiba na sheria za nchi mbili hizi ziliweka bayana mipaka hiyo na mipaka hiyo ilitambuliwa chini ya sheria za kimataifa.

Rasimu ya Katiba Mpya ni lazima itamke kwa uwazi kabisa na kutambua na kuheshimu mipaka ya nchi mbili hizi kama ilivyokuwa kabla ya siku ya Muungano tarehe 26 Aprili, 1964.

Baada ya hapo, Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Tanganyika (itakayotungwa baada ya kupata Katiba mpya ya Muungano) kila moja iweke wazi mipaka yake.

3.Uraia:

Uraia ndiyo msingi wa ujananchi. Kwa vyovyote vile Katiba Mpya isijumuishe suala la Uraia kuwa la pamoja kupitia Muungano. Kila nchi mwanachama katika muungano ibakie na uraia wake na iratibu masuala yote yanayohusu uraia wake na raia zake. Kwa kufuata mfano kama wa Muungano wa Ulaya (European Union), unaweza kuwa na haki inayotambulika kikatiba ya uhuru wa raia wa nchi moja mwanachama kwenda katika nchi nyengine mwanachama kupitia utaratibu maalum utakaowekwa (free movement of people). Hata hivyo, kila nchi mwanachama iwe na haki ya kuweka utaratibu wa vipi raia hao watafaidi haki na fursa za nchi mwanachama nyingine.

Hili ni la muhimu hasa kwa nchi ndogo kama Zanzibar ambayo ina rasilimali ndogo ya ardhi na hasa ikizingatiwa kuwa ardhi ilikuwa mojawapo ya sababu kuu za kufanyika Mapinduzi. Katika hali kama hiyo, Zanzibar ina sababu nzito za kuona inadhibiti na kusimamia wenyewe Uraia wake na utambulisho wa raia hao.

Hivyo basi, suala la Uraia lisiwemo katika mambo ya Muungano na badala yake kila nchi isimamie yenyewe masuala ya Uraia.

Hata hivyo, kunaweza kukawepo chombo cha pamoja kinachojumuisha nchi mbili hizi cha kuratibu masuala ya Uraia na haki na fursa ambazo raia wanaweza kuwa nazo kwa kila upande.

4.Uhamiaji:

Kutokana na sababu tulizozitaja hapo juu kuhusiana na suala la Uraia inapelekea wazi kuwa kila nchi mwanachama idhibiti na kusimamia wenyewe mambo ya Uhamiaji. Hivyo basi, rasimu ya Katiba Mpya isijumuishe suala la Uhamiaji kuwa ni suala la Muungano. 

Kila nchi mwanachama kati ya Zanzibar na Tanganyika iwe na paspoti yake yenyewe yenye kubeba jina la nchi yake na nembo yake ya Taifa na yenye kudhamini usalama wa raia wake nje ya nchi kupitia uhakikisho unaotolewa na Serikali ya nchi husika.

Ili kuonesha sura ya kuwepo muungano wa kisiasa, paspoti za nchi mbili hizo zinaweza kuwa na jina la Muungano juu na kufuatiwa na jina la nchi mwanachama likiambatana na nembo ya Taifa ya nchi hiyo. Kwa mfano, “UNITED REPUBLICS OF TANZANIA – ZANZIBAR PASSPORT” na “UNITED REPUBLICS OF TANZANIA – TANGANYIKA PASSPORT”.

Kwa upande mwengine kunaweza kukawa na mamlaka ya kuratibu masuala ya uhamiaji wa nchi hizi mbili (Union immigration regulatory authority) kwa lengo la kuweka na kuratibu mfumo mzuri wa mawasiliano kati ya mamlaka za uhamiaji za nchi mbili hizi.

5.Mambo ya Nje:

Mamlaka juu ya mambo ya nje na uwezo wa nchi kuingia mikataba na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa ndiyo roho ya nchi yoyote duniani kutambulika kimataifa na kuweza kusimamia mamlaka yake ya ndani yanapohitaji mashirikiano na nchi nyengine.

Ili nchi iweze kutambulika kimataifa inapaswa kuwa na mambo manne yafuatayo:

(a)eneo la ardhi lenye mipaka inayotambulika;
(b)watu wanaoishi kwenye eneo hilo wanaojitambulisha na eneo hilo;
(c)serikali inayotekeleza majukumu yake; na
(d)uwezo wa kuingia katika mahusiano ya kimataifa na nchi nyengine.

Kwa msingi huo, Wazanzibari wanahitaji kuona kuwa Mambo ya Nje haijumuishwi katika orodha ya mambo ya Muungano na badala yake kila nchi isimamie yenyewe mamlaka yake juu ya mambo ya nje.

Hata hivyo, uratibu wa sera ya mambo ya nje (foreign policy coordination) inaweza kuwa ni suala la muungano lakini utekelezaji wake kila nchi ikausimamia kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje. Uratibu wa sera ya mambo ya nje unaweza kufanywa kupitia chombo cha pamoja kitakachoundwa na Wizara za Mambo ya Nje za nchi mbili hizi kwa mfano kuwa na Council on Foreign Policy.

Kutokana na hoja hizo hapo juu inabaki kuwa kila nchi iwe na uanachama na kiti chake katika Umoja wa Mataifa na jumuiya nyengine za kimataifa. Hayo si ajabu katika miungano. Umoja wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti (USSR) ulikuwa na uanachama na kiti chake Umoja wa Mataifa lakini miongoni mwa nchi wanachama, Jamhuri tatu za Ukraine, Belarus na Georgia ziliamua kuwa na uanachama na viti vyao katika Umoja wa Mataifa na hilo liliwezekana.

Kwa msingi huo huo, Zanzibar iwe na uanchama wake katika Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya SADC na jumuiya nyengine za kikanda na za kimataifa.

6.Sarafu, Benki Kuu, Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje, Ushuru wa Forodha, Kodi ya Mapato na Kodi ya Mashirika:

Uchumi si suala la Muungano hata katika Katiba inayotumika sasa. Hata hivyo, nyenzo za kuendeshea na kusimamia uchumi wa nchi kwa maana ya sera za fedha na uchumi (fiscal and monetary policies) zimeendelea kudhibitiwa kupitia Serikali ya Muungano. 

Vyombo vikuu vinavyosimamia sera hizo ambavyo ni Benki Kuu (BOT), Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) na Wizara ya Fedha ya Serikali ya Muungano vimekuwa vikifanya maamuzi na kuyatekeleza bila ya kuzingatia kuwa kwa maumbile uchumi wa Zanzibar ambao ni uchumi unaotegemea utoaji wa huduma (service oriented economy) hauwezi kuwa sawa na uchumi wa Tanganyika ambao unategemea rasilimali (resource based economy). Sera za fedha na uchumi zikiwemo zile zinazohusu udhibiti wa sarafu na viwango vya kodi, ushuru na riba katika mabenki zimekuwa zikitungwa bila ya kuzingatia msingi huo wa chumi mbili zilizo tofauti na badala yake mara zote zimeegemezwa kwenye kulinda maslahi ya uchumi wa Tanganyika.

Sarafu ya pamoja imekuwa ikishuka thamani kwa kasi kila uchao kutokana na sababu nyingi lakini miongoni mwake zaidi zinatokana na uendeshaji mbaya wa uchumi wa Tanganyika. Serikali inapochapisha sarafu zaidi ili kudhibiti mfumko wa bei athari zake zinaikumba pia Zanzibar.

Zanzibar inahitaji kujikomboa kiuchumi ili iweze kutekeleza malengo ya Mapinduzi kwa wananchi wake na hivyo inahitaji kuwa na mamlaka yake kamili katika kusimamia masuala ya sera za fedha na uchumi yakiwemo masuala yote yanayohusu sarafu, viwango vya kodi na ushuru pamoja na riba katika mabenki, mikopo na biashara ya nchi za nje.

Kutokana na hali hiyo, masuala ya sarafu, benki kuu, mikopo na biashara ya nchi za nje, ushuru wa forodha, kodi ya mapato na kodi ya mashirika kila nchi inapaswa iyasimamie yenyewe.

7.Polisi:

Pamoja na kuwemo katika mambo ya awali ya Muungano lakini uendeshaji wa Polisi umekuwa na matatizo yake katika muungano. Miaka yote Polisi Zanzibar imekuwa ikilalamika kuwa inachukuliwa kama vile ni Mkoa tu na hata bajeti na mahitaji yake mengine yanachukuliwa hivyo hivyo na makao makuu ya Polisi yaliyopo Dar es Salaam.

Katika nchi nyingi duniani Polisi ambayo inashughulika na usalama wa raia na mali zao imekuwa ikiendeshwa chini ya Serikali za Manispaa na hata Majimbo seuze kwa nchi kama ilivyo Zanzibar.

Ukiondoa mishahara na bajeti ndogo ya uendeshaji inayotolewa na makao makuu ya Polisi, gharama nyengine za uendeshaji wa polisi kwa Zanzibar zimekuwa zikichangiwa na mamlaka za Zanzibar ikiwemo Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).

Hivyo basi, wakati umefika kuona mamlaka kuhusu Polisi yanaondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano na kila nchi ishughulikie yenyewe Polisi yake.

8.Mafuta na Gesi Asilia (pamoja na maliasili nyengine zote):

Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa niaba ya Wazanzibari lilishafanya maamuzi mwezi Aprili 2009 kuyaondoa masuala ya mafuta na gesi asilia kutoka kwenye orodha ya mambo ya Muungano. Mbali na maazimio ya Baraza la Wawakilishi, masuala ya mafuta na gesi asilia yanahusu uchumi ambalo si suala la Muungano.

Katiba Mpya haipaswi kuyajumuisha masuala hayo mawili (pamoja na maliasili nyengine kwa ujumla) kuwa mambo ya Muungano.

Hivyo basi, rasimu yoyote itakayoyajumuisha masuala hayo ya Mafuta na Gesi Asilia (pamoja na maliasili nyengine zote kwa ujumla) kuwa masuala ya Muungano haitakubalika kwa Wazanzibari.

9.Vyama vya Siasa:

Muungano uliundwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kupitia serikali zao. Mazungumzo yaliyopelekea muungano huo na hata utekelezaji wa hatua za kuunganisha nchi mbili hizi katika muungano hayakuhusisha vyama vya siasa vya wakati huo, ASP kwa upande wa Zanzibar na TANU kwa upande wa Tanganyika. Ndiyo maana kwa miaka 13 ya Muungano (kuanzia 1964 hadi 1977) kila nchi kati ya nchi mbili hizi iliendelea kuongozwa na chama chake cha siasa.

Moja kati ya dhoruba kubwa dhidi ya makubaliano ya asili ya muungano huu ambayo ni Mkataba wa Muungano ilikuwa ni kuunganisha vyama vya siasa vya ASP na TANU na kuunda CCM ambacho kilijitangazia kushika hatamu na kuwa juu ya vyombo vyengine vyote vya nchi zikiwemo Serikali. Utaratibu huo uliingizwa ndani ya Katiba za nchi na hivyo kuuhalalisha kisheria. Tokea wakati huo, Zanzibar imekosa mamlaka ya kisiasa ya kufanya maamuzi yake kwa mambo yanayoihusu. Na pale ilipofanya hivyo ilifanya kwa kutegemea na kujiamini kwa uongozi uliopo Zanzibar ingawa majaribio ya kutumia nguvu ya vyama kuzuia maamuzi kama hayo yamekuwa yakifanyika na baadhi ya wakati kufuzu.

Maongozi ya nchi yoyote yanategemea historia, mila na utamaduni wa watu wa nchi husika. 

Kwa msingi huo basi, na ili Zanzibar iweze kurejesha mamlaka yake ya kisiasa katika kufanya na kusimamia maamuzi kwa mambo yake, rasimu ya Katiba haipaswi kujumuisha suala la vyama vya siasa kuwa ni jambo la Muungano. Zanzibar na Tanganyika kila moja iweze kuandikisha vyama vyake vya siasa.

10.Utaratibu wa uendeshaji wa Mambo ya Muungano:

Kwa yale mambo yatakayokubaliwa kubaki katika Muungano kama vile:



Utaratibu wa uendeshaji wake uwekwe wazi katika Katiba kwamba maamuzi yote yatafanywa kwa mashauriano na makubaliano kati ya nchi mbili zinazounda Muungano huu na yatakuwa halali tu iwapo yatafuata msingi huu.

HITIMISHO:

Haya kimsingi ndiyo mapendekezo yetu Kamati ya Maridhiano. Tunayaleta kwenu muyapokee, muyajadili na kuwaomba muyaridhie ili yawe ndiyo msingi wa mwelekeo wa wananchi wa Zanzibar ambao wengi wao waliojitokeza mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba walitaka nchi yao iwe na mamlaka kamili.

Kwa mapendekezo haya, tunadhani Zanzibar na Tanganyika zitaendelea kuwa na mashirikiano ya kidugu kupitia mfumo mpya wa Muungano na wakati huo huo kila nchi mwanachama wa muungano ikibaki na mamlaka yake kamili katika yake maeneo ya msingi ambayo kila nchi hupenda kuwa nayo.

MPAKA KIWELEWEKEE !!!

Uamsho Zanzibar
Bismillahir Rahmanir Rahiim
TANGAZO LA DUA MAALUM
Jumuiya ya UAMSHO na Mihadhara ya Kiislamu-Zanzibar inapenda kuwatangazia Waislamu wote wanawake na wanaume kua, kutasomwa DUA MAALUM siku ya Ijumaa tarehe 31 Mei, 2013 katika msikiti wa Afraa-kidongo chekundu, mara baada ya sala ya Ijumaa insha Allah.
Lengo la DUA hii ni kumuomba Mwenyezi Mungu awape Shekhe zetu ithbati kwa dhulma wanazofanyiwa na kuwa na subira pamoja na familia zao katika wakati huu mgumu. Dua hii itasomwa vile vile katika mikoa yote ya Unguja na Pemba Inshaa Allah. Shime sote tuhudhurie.
TUNATAKA ZANZIBAR YETU HURU, YENYE MAMLAKA YAKE KAMILI, KITAIFA NA KIMATAIFA
WABILLAH TAUFIQ
UAMSHO MEDIA CENTER
19 Rajab, 1434 – 29 Mei, 2013
Email: jumiki@hotmail.com
Facebook: Uamsho Zanzibar
Twitter: @Uamsho1

Monday 27 May 2013

WABUNGE TANGANYIKA WASUTANA KWA UROHO WA MADARAKA !!!

ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, amewashutumu wanasiasa wenzake kuwa siasa zao zimezorotesha ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Ngeleja ambaye ni mbunge wa Sengerema aliwasuta wanasiasa hao bungeni juzi wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Alitolea mfano wa ubishi uliojitokeza baina ya wanasiasa wakati akiwa Waziri wa Nishati na Madini ambapo taifa lilikuwa kwenye hali tete ya mgawo wa umeme.

Ngeleja alisema kuwa baadhi ya wanasiasa hao licha ya kutambua hali mbaya ya mgawo uliokuwa ukilikabili taifa, walikataa nchi isinunue mitambo ya kampuni ya Dowans kwa madai kuwa ni ya kifisadi.

Licha ya kutotaja majina ya wanasiasa aliowalenga, lakini katika kundi hilo walikuwemo mawaziri Samuel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe ambao mpaka sasa wanapinga serikali kulipa deni la kampuni hiyo baada ya kuvunja mkataba nayo kinyume cha utaratibu.

Dowans ambayo ilirithi mkataba wa kampuni ya Richmond LLC iliibuka wakati wa Bunge la Tisa chini ya Spika Sitta ambaye aliunda Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Mwakyembe kuchunguza uhalali wa kampuni hiyo.


Februari mwaka 2008, kamati ya Mwakyembe ilitoa ripoti yake ikionyesha kuwa Richmond ni kampuni hewa ya kufua umeme ambayo ilipewa mkataba kijanja, hatua iliyomlazimu aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa kujiuzulu.

Tangu wakati huo, Sitta na Mwakyembe pamoja na wanasiasa wengine wa vyama tofauti wamekuwa wakiishambulia kampuni ya Richmond hata baada ya kurithiwa na Dowans.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), ni miongoni mwa wanasiasa wachache walioshambuliwa na kundi kubwa pale alipoishauri serikali kuinunua mitambo ya Dowans wakati huo ikiuzwa kwa dola milioni 59.

Wazo hilo lilipata upinzani mkubwa na baadhi ya watu wakidai mbunge huyo ametumwa na serikali au kampuni hiyo ili kuhalalisha ufisadi wa Richmond.

Kundi hilo lililokuwa likipinga mitambo hiyo kununuliwa lilikuwa likijiegemeza kwenye sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004 inayokataza kununua mitambo chakavu lakini Zitto alishauri kuwa wanaweza kufanya marekebisho wakainunua ili kupunguza gharama za kuendelea kuikodi.

Vuta ni kuvute hiyo iliendelea hadi mitambo hiyo ikanunuliwa kampuni ya Symbion Power ya Marekani kwa dola milioni 159 na sasa inazalisha umeme na kuiuzia TANESCO.

Ni katika msingi huo, Ngeleja alidai kuwa wakati mwingine siasa kama hizo zimezorotesha uchumi na hivyo kuwaasa wanasiasa kuwa makini ili kuepuka kuikosesha nchi fursa.

“Sisi hapa tulikataa nchi isinunue mitambo ya Dowans kwa gharama nafuu tukiitwa ni mafisadi, tumehongwa lakini mitambo hiyo imenunuliwa na Symbion sasa inazalisha umeme na kutuuzia,” alisema.

Amtetea Kinana

Wakati huohuo, Ngeleja alimsafisha Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kutokana na tuhuma za kampuni yake ya uwakala wa meli kuhusishwa katika biashara haramu ya pembe za ndovu mwaka 2009.

Tuhuma hizo zimeibuliwa bungeni mara mbili tofauti na CHADEMA, kupitia mawaziri vivuli wao wa wizara za Maliasli na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa na Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ezekiel Wenje.

Katika juhudi za kumsafisha kiongozi huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi, Aprili 30 mwaka huu, baada ya Msigwa kuibua tuhuma hizo alichangia hoja hiyo akisema ni tuhuma za uongo.

Wiki iliyopita Msemaji Mkuu wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika, alimgusa Kinana akisema anatajwa na vyanzo mbalimbali kwamba amewahi kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya Artumas.

Mnyika alisema kuwa kampuni hiyo iliingia mkataba na serikali wa kuzalisha megawatt- 300 za umeme Mtwara eneo la Mnazi Bay.

Mkataba huo ulikuwa wa misingi ya mabadilishano ya gesi kwa nishati ya umeme; kwamba Artumas ingechimba na kuuza gesi asilia na kuilipa serikali kwa pamoja na mambo mengine kuizalishia umeme wa 300MW.

Mnyika alisema baadaye mwaka 2010 Artumas baada ya kufaidika vya kutosha kutokana na uvunaji na uuzaji iliacha kuendeleza mradi huo kwa kisingizio cha madai ya mdororo wa uchumi mwaka 2009 na kuuza hisa zake kwa kampuni ya Wentworth ya Ufaransa.

Katika utetezi wake, Ngeleja alisema uwepo wa Kinana kwenye kampuni hiyo ni jambo la kawaida lenye heshima kubwa ya kuaminika kwa kampuni kubwa.

Alitolea mfano viongozi wengine wakuu wastaafu wa kitaifa ambao wamewahi kuwa ama wanaendelea kuwepo kwenye bodi mbalimbali za kampuni tofauti kama wajumbe wa bodi au wenyeviti na kuhoji kwa nini taabu iwe kwa Kinana.

Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, naye wakati wa kuhitimisha hoja za wabunge waliochangia bajeti yake, alimtetea Kinana na kudai kuwa kiongozi anaonekana kuwakera CHADEMA ndio maana hawaishi midomoni mwao.

“Kwa hiyo, mimi nadhani mambo haya tuyaache tu, mwacheni Kinana afanye kazi yake tutapambana majukwaani na mwisho wa yote majibu mtayapata kwa wananchi mwaka 2015.

Naye Sitta Tumma toka Mwanza anesema Ngeleja akiwashambulia wanasiasa wenzake, Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema watuhumiwa wa kashfa ya ufisadi wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond na Dowans ni hatari na hawastahili kuungwa mkono katika uongozi.

Ingawa hakutaja majina, Sitta alisema watu hao wameanza kuhaha kutafuta uungwaji mkono katika safari yao ya kutaka madaraka.

Sitta alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph Bakita, katika Parokia ya Igoma jijini Mwanza.

Aliwataka Watanzania kujihadhari na watu hao kwa kuchagua watu waadilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwaka 2015.

Sitta alisema yeye na mawaziri wenzake watatu wameungana kifikra katika kupambana na uonevu na ufisadi dhidi ya rasilimali za nchi.

Kwa mujibu wa Sitta, mikataba ya kinyonyaji na kifisadi ya Richmond imeliingizia taifa hasara kubwa sana, kwani kwa sasa nchi inadaiwa mamilioni ya fedha kutokana na mikataba hiyo mibovu.

“Nchi ikiingia kwenye wimbi la ufisadi, fisadi atatafuta watu wa kumuunga mkono kupata uongozi. Atataka aungwe mkono na mkuu wa mkoa mwenye mtazamo wa kifisadi, na mkuu wa mkoa atamtaka mkuu wa wilaya kumuunga mkono fisadi.

“Na leo nawaambieni wananchi kwamba kura yako ni silaha ambayo ukiitumia vizuri italeta matumaini na utawala bora! Kwa hiyo, msidanganyike kuchagua walafi mwaka 2015, maana nchi itaingia kwenye matatizo makubwa ya ufisadi,” alisema Sitta.

Ingawa hakutaja jina la mtu, ni wazi kwamba Waziri huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pengine alikuwa anamlenga Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye mwaka 2008 alilazimika kujiuzulu kutokana na kashfa hiyo ya Richmond.

Alisema yeye na mawaziri hao watatu wako pamoja katika fikra za kupambana na vitendo vya kifisadi, uonevu na mikataba tata inayoliangamiza taifa na kwamba wako mstari wa mbele kutetea wanyonge.

Aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe pamoja na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.

Sunday 26 May 2013

LIPUMBA ASEMA WAISLAMU TUUNGANE !!!


MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameibua suala zito akikihusisha chama chake na “kumnusuru” Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu uliopita.

Profesa Lipumba alitoboa siri hiyo katika Msikiti wa Idrissa, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, alikokwenda kuswali swala ya Ijumaa.

Huku akisisitiza juu ya umuhimu wa mshikamano wa kiimani, Profesa Lipumba alianza kwa kuzungumzia matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2010, na ushindani mkali wa kisiasa uliokuwapo.

Alisema hawaoni matunda ya jitihada walizofanya kumnusuru Rais Kikwete asishindwe, kwani hata chini ya uongozi wake, Waislamu wameendelea kutothaminiwa.

“Ninyi masheikh mnajua vizuri zaidi hali ya kisiasa ilivyokuwa, kwamba ilibidi zifanyike juhudi za makusudi ili kuokoa jahazi. Lakini pamoja na kuliokoa jahazi, hali halisi inaonyesha mpaka sasa hakuna matunda yoyote yaliyopatikana, na tupo katika mtihani mgumu zaidi,” alisema.

Katika hali ambayo inasemekana ushindi wa Rais Kikwete ulipatikana kwa mbinu, huku wengine wakiituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa ilimnusuru mgombea wa CCM, kauli hii ya Profesa Lipumba inadokeza kwamba anajua mkakati zaidi wa kazi ya Tume ya Uchaguzi.

Katika hali isiyo ya kawaida, Profesa Lipumba anaonekana kuhamasisha Waislamu kujipanga akisema “wenzetu wameanza kujipanga” kuelekea 2015.

“Kwahiyo kama Waislamu tunataka kupata haki zetu, kama tunataka kuishi kama raia wa daraja la kwanza katika nchi yetu, lazima tujipange kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015; na sisi tuanze kujipanga kwa sababu wenzetu wameanza kujipanga, vinginevyo tutaendelea kubaki maskini na raia wa daraja la nne katika nchi yetu wenyewe.

“Mwaka 2010 wakati mshindi wa uchaguzi wa rais alipotangazwa, mimi nilikwenda kwenye hafla ya kutangazwa matokeo, na nilikwenda makusudi tu, siyo kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, ila nilikwenda makusudi kwa kujua hali ya kisiasa ilivyokuwa wakati huo.

“Huku nilikutana na Sheikh Basaleh. Nilipokutana naye, alinipongeza; sijui kama yeye anakumbuka, akaniambia ‘umeweka mbele imani yako na umekuwa mwelewa wa mambo.’”

Hata hivyo, licha ya Profesa Lipumba kuwaambia Waislamu wajipange kwa ajili ya uchaguzi mkuu, hakusema wajipange kupitia chama kipi.

Lakini alisisitiza kwamba uchaguzi ujao ni zaidi ya siasa au rais yupi anafaa, bali maslahi, hasa ya rasilimali nyeti zinazopatikana katika ukanda wa Pwani ya Mashariki, eneo ambalo alisema linakaliwa zaidi na watu wenye imani ya Kiislamu.

Katika moja ya kauli zake, Profesa Lipumba alisema kwamba kuna chama kimoja kinataka kuchukua madaraka ya nchi, lakini kinasaidiwa na mataifa ya magharibi, yasiyoenzi wala kuthamini imani ya Kiislamu.

Kwa muda sasa, zimekuwapo tetesi kwamba CCM imekuwa inafanya siasa za udini dhidi ya vyama vya upinzani, hasa inapoona maslahi yake yapo hatarini.

Mwaka 2010 makada kadhaa wa CCM walitumia mitandao ya simu kuchonga (spoofing) ujumbe wa simu ulioshambulia mgombea mmoja wa upinzani, ukimhusisha na imani yake.

Kauli ya Lipumba imethibitisha pia minong’ono iliyokuwapo muda mrefu kuwa baadhi ya kura za Profesa Lipumba zilipotelea kwa Rais Kikwete.

Katika uchaguzi huo, Lipumba alitangazwa kushika namba ya tatu, nyuma ya Rais Kikwete na Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA.

Alipoulizwa kuhusu ziara yake msikitini na kauli aliyotoa, Profesa Lipumba alikiri kwamba alikwenda kuzungumzia hali ya kisiasa nchini.

MAALIM SEIF ASISITIZA ZANZIBAR YENYE MAMLAKA KAMILI !!!



Zanzibar: Kongamano la “Maridhiano ya Wazanzibari” limefanyika mjini hapa huku Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akitaka Zanzibar kujitawala wenyewe na kuwa na mamlaka kamili kwani ndiyo dhamira ya msingi wa ukombozi wa Mapinduzi ya Zanzibar.
Maalim Seif akifungua kongamano hilo mjini hapa jana, alisema kuwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yalikuwa na lengo la kuwafanya Wazanzibari wajitawale wenyewe na wawe na uamuzi wao kwa kila jambo.
Alisema dhamira hiyo ya Mapinduzi ilianza kukiukwa baada ya kutiwa saini kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao uliipunguzia Zanzibar mamlaka.
Alisema kwamba siyo kweli kuwa Wazanzibari hawataki Muungano bali wanataka muundo wa muungano uwe wa mkataba ili kuwapo Serikali za Tanganyika na Zanzibar zenye mamlaka kamili.
“Kuwa na mamlaka kamili siyo kwa maslahi ya watu wachache bali kwa watu wote. Ni kama mvua, yaani inaponyesha mimea yote inanawirika,” alisema Maalim Seif na kuongeza;
“Tunataka kurejesha heshima ya nchi yetu, tuwe Wizara yetu ya Mambo ya Nje, bendera yetu ipepee nchi za kigeni, Umoja wa Mataifa na Jumuiya zingine za Kimataifa zikiwamo Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki”.
Aidha, Maalim Seif aliipongeza Kamati ya Maridhiano chini ya Mwenyekiti wake, Hassan Nassor Moyo kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuyaendeleza maridhiano hayo na umoja wa Wazanzibari.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ambaye ni mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar, Hassan Nassor Moyo alisema maridhiano hayo yaliyoasisiwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, yameondoa fitina na chuki zilizodumu kwa muda mrefu miongoni mwa wananchi.
Kamati ya Maridhiano iliyoratibu kongamano hilo ilitoa mapendekezo yake ikitaka Zanzibar iwe na mamlaka yake kamili kwa kuwa na sarafu yake, mamlaka ya Mambo ya Nje, uraia wake, pasi yake ya kusafiria na wametaka Jeshi la Polisi lisiwemo kwenye mambo ya Muungano, gesi na mafuta yatakayopatikana Zanzibar yawe mali ya Zanzibar na pia suala la vyama vya siasa lisiwe la Muungano.
“Haya si maagizo bali ni mashauri yetu pindi mkiyakubali tunakuombeni kuyafanyia kazi katika kujadili na kupitisha Katiba Mpya,” alisema Mwenyekiti huyo katika taarifa iliyosomwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu.
Pia walitaka mipaka ya Zanzibar itambulike katika Katiba Mpya kama ilivyokuwa kabla ya Muungano Aprili, 1964.

Friday 24 May 2013

ASKARI WA UK AULIWA MJINI LONDONI, WAUAJI WAACHA UJUMBE MZITO !!!

Askari wa Kiingereza Auliwa Mjini London Wauaji Waacha Ujumbe.
Ilikuwa si kitu cha kutegemea ingetokea Mchana kwepu katikati ya jiji la London Uingereza kuwa angeuliwa Askari wa Jeshi la Britain inayoendeleza mradi wa kupambana na uislaam.
Habari kutoka Uingereza zinaeleza kuwa mtu aliyejihami na Panga amemshambulia Askari wa Kiingereza karibu na kituo cha Polisi Kusini mashariki mwa jiji la london.
Vyombo vya habari vya hapa uingereza zinaeleza mtu mmoja muislaam amemshambulia kwa Panga na hatimae kuzitenganisha Kichwa na kiwiliwili cha Askari wa kiingereza,picha ya askari aliyeuliwa inaonyesha kichwa chake kupigwa panga vibaya na kusababisha kifo chake.
Watu walioshuhudia wanasema mwuaji alikuwa akitamka maneno kama "Mauaji mnayowafanyia ndugu zetu Afghanistan na waislaam ndio kilichonisukuma kufanya kitendo hichi,na wala hamtoishi kwa usalama kama mnaenedela kuwashambulia Waislaam,na namwua Askari huyo kwajili ya kulipiza kisasi kwa ndugu zangu waislaam wanaouliwa huko Afghanistan"alisema shujaa aliyefanya mauaji ya Askari.
Polisi mjini London wanasema watu wengine 3 wamejeruhiwa na haijulikana watu hao walijeruhiwa kwa risasi au la,na Sirikali ya Nchi hiyo wanaficha kitendo hicho na wapi aliko Mwauaji wa shambulio la Askari.
Mtaa uliofanyika tukio la mauaji wakazi wake wengi ni Jamii ya kisomali na mtaa huo unajulikana kwa Woolich,Magazeti ya nchi hiyo wameandika na kuizungumzia saana tukio la jana la kuuliwa kwa Askari wa Kiingereza,Baadhi ya Magazeti ya nchi hiyo wanaihusisha kitendo hicho na wasomali waishio mtaa huo lakini mpaka sasa hakuna uthibitisho wa nani aliyehusika.
Sirikali ya Uingereza imelitaja shambulio hilo kuwa ni kitendo cha Kigaidi,nae waziri mkuu wa Nchi hiyo Davi camiron ameilaani mauaji ya askari wake.
Watu waliokuwa karibu wamesema waliwaona watu hao waliofanya mauaji ya askari na huko mikono yao ikiwa imejaa damu na baadae kusema "tunasikitika muyashuhudie tukio kama hili nyinyi wanawake lakini kila siku wanajeshi wenu wanaua kama hivi kule Afghanistaan muyalaumu sirikali yenu isiyo na manufaa kwenu"
Tukio hili limewakumbusha wengi kule France mwaka jana aliposhambulia Mohamed Al Marah ktk mji Talooz Nchini France

Thursday 23 May 2013

SHEHA WA SHEHIA YA TOMONDO AMWAGIWA TINDI KALI !!!



VITENDO vya uhalifu vinavyoendelea kujitokeza hapa nchini kila kukicha huku mamlaka zinazohusika na suala la ulinzi na usalama zinaonekana kukaa kimya kwa kushindwa kudhibiti vitendo hivyo.

Hayo yamebainika baada ya sheha wa shehia ya Tomondo Mohammed Saidi (Kidevu) jana kumwagiwa tindi kali akiwa nyumbani kwake Tomondo Wilaya ya Magharibi Unguja.

Tukio la kumwagiwa kwa tindi kali sheha huyo lilitokea mnamo majira ya saa 2:30 usiku, wakati akiwa katika harakati za kuchota maji.

Akizungumza katika hospitali ya Mnazimmoja ambayo ndio anayopatiwa matibabu sheha huyo alisema kabla ya tukio hilo kutokea alitokea kijana mmoja ambae hakumfahamu na kusalimiana nae na baadae kumwagia.

Alisema mara baada ya kumwagia acid alimfukuza kijana huyo huku akimnadia mwizi lakini alishindwa kupata msaada wowote kutoka kwa wananchi.

Awali sheha huyo alikua akipokea vitisho kutoka kwa watu mbalimbali ambao hawafahamu, ambavyo vimeanza wakati wa chaguzi za wilaya za kuwapata wajumbe wa baraza la katiba.

Kwa upande wake wake Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi,Mkadam Khamis amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kuwa Jeshi la Polisi litafanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha kuwa wanawakamata wale wote waliohusika na tukio hilo.

kamanda huyo ameyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu alipokuwa ofisini kwake Madema.

Pia ametowa wito kwa wananchi kutokujichukulia sheria mikononi mwao kwani mara nyengine hupelekea matatizo zaidi.

Nae Daktari anaempatia matibabu hospitalini hapo Dk Saidi Ali amesema kuwa sheha huyo amepata majeraha katika jicho la upande wa kulia ,kifuani na mgongoni na hali yake inaendelea vizuri huku akisisitiza kuwa ataendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo mpaka Serikali itakapoamuwa kama asifirishwe au la.

Mapema Makamo wa pili wa Raisi Balozi Seif Ali Iddi alifika hospitalini hapo na kulitaka jeshi la polisi kuchuku hatua za kisheria na kufanya uchunguzi wa kina ili kuhakikisha muhusika wa tukio hilo anakamatwa.

“Tukio hili si lakwanza wala si lapili kwani mwezi wa disemba mwaka jana katibu wa mufti shehe Suleiman suraga alikubwa na kadhia hiyo”alisema Balozi Seif.

Hata hivyo amesema serikali imesikitishwa sana na vikitendo hivyo vinavyoashiria uvunjifu wa amani huku akisema serikali itagharamia matibabu yake.
 — with King Sujae and 5 others.

Wednesday 22 May 2013

MPAKA KIWELEWEKEE !!!

Jumuiya ya UAMSHO na Mihadhara ya Kiislamu-Zanzibar inapenda kuwatangazia Waislamu wote wanawake na wanaume kua, kutasomwa DUA MAALUM siku ya Ijumaa tarehe 24 Mei, 2013 katika msikiti wa Sokoni - Mwanakwerekwe, mara baada ya sala ya Ijumaa insha Allah.

Lengo la DUA hii ni kumuomba Mwenyezi Mungu awape Shekhe zetu ithbati kwa dhulma wanazofanyiwa na kuwa na subira pamoja na familia zao katika wakati huu mgumu. Dua hii itasomwa vile vile katika mikoa yote ya Unguja na Pemba Inshaa Allah. Shime sote tuhudhurie.

TUNATAKA ZANZIBAR YETU HURU, YENYE MAMLAKA YAKE KAMILI, KITAIFA NA KIMATAIFA
WABILLAH TAUFIQ

UAMSHO MEDIA CENTER
12 Rajab, 1434 – 22 Mei, 2013
Email: jumiki@hotmail.com
Facebook: Uamsho Zanzibar
Twitter: @Uamsho1

MAALIM SEIF NITAOMBA KUGOMBANIA TENA URAIS WA ZANZIBAR !!!


 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad amesema ataomba tena kugombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
 
Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV, Maalim Seif alisema kuwa anachoomba tu Mwenyezi Mungu ampe afya njema.
 
“Ni uamuzi wa wananchi na wanachama wenyewe wa CUF lakini kama Mwenyezi Mungu akinipa afya na uzima bado nia ipo,” alisema Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
 
Alisema hivi sasa chama hicho kimekuwa kikijiimarisha visiwani huko kwa kufanya mikutano Pemba na Unguja ili kuhakikisha kinaendelea kukubalika kwa wananchi.

Kauli hiyo ya Maalim Seif ambaye amekuwa akiwania nafasi hiyo tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi, ilipokewa kwa hisia tofauti ambapo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bashiru Ali alisema vyama vya siasa ni lazima viwe vinatayarisha viongozi wa baadaye ambao watafahamu kwamba uongozi ni dhamana wanayopewa na wananchi.
 
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema Maalim Seif kama mwanachama wa chama hicho anaruhusiwa kwa mujibu wa Katiba kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa dola.

KESI YA UAMSHO KUENDELEYA DSM !!!


 
Kesi ya uchochezi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu ya Zanzibar (Jumiki),Sheikh Faridi Hadi Ahmed (41), na wenzake 9, sasa imepangwa kuunguruma katika Mahakama ya Rufani Dar es Salaam, Juni 10, mwaka huu.
 
Sheikh Faridi na wenzake wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama Kuu ya Zanzibar. Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mselem Ali Mselem, Mussa Juma, Azzan Khalid Hamdani, Suleiman Juma, Khamis Ali na Hassan Bakari, Ghalib Hamada Juma, Abdallah Saidi na Fikirini Fikirini.
 
Washtakiwa hao kupitia kwa mawakili wao, wamewasilisha maombi katika Mahakama ya Rufani Tanzania, wakiomba mahakama hiyo itupilie mbali rufaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Zanzibar, dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, wa Machi 11, mwaka huu.
 
Mahakama hiyo, katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Abrahamu Mwampashi, ilitengua mwenendo wa maombi ya dhamana ya washtakiwa yaliyotolewa na na mawakili wao kwa Msajili wa Mahakama Kuu, Oktoba 25, siku washtakiwa hao waliposomewa mashtaka.


Pia Mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi ya marejeo ya washtakiwa hao kuhusu uamuzi wa Msajili wa Mahakama Kuu kuwakatalia dhamana na kuamuru warejeshwe rumande hadi tarehe iliyopangwa kutajwa kwa kesi hiyo, pamoja na pingamizi la awali (PO) la upande wa mashtaka.
Katika maombi yao kwa Mahakama ya Rufani, washtakiwa hao wanaiomba Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa hiyo ya DPP, kwa madai kuwa hakuna rufaa iliyofunguliwa na mjibu maombi (DPP) dhidi ya uamuzi na amri ya Mahakama Kuu anayoipinga.
 
Washtakiwa hao wanabainisha kuwa taarifa ya kusudio la kukata rufaa iliyowasilishwa mahakamani hapo na mjibu maombi haihusiani na uamuzi huo wa Mahakama Kuu wa Machi 11, mwaka huu.
 
Wanafafanua kuwa uamuzi huo wa Mahakama Kuu wa Machi 11, mwaka huu hauwezi kupingwa kwa rufaa wala kwa maombi ya marejeo katika Mahakama ya Rufani
 
 Maombi haya yamepangwa kusikilizwa na jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Juni 10, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
 
Jopo hilo la majaji watakaosikiliza maombi hayo linaongozwa na Jaji January Msiffe, akisaidiana na Jaji Salum Massati na Jaji William Mandia.
 
Maombi hayo yamewasilishwa chini ya hati ya dharura wakiomba mahakama iyasikilize mapema .
Dar es Salaam. Kesi ya uchochezi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu ya Zanzibar (Jumiki),Sheikh Faridi Hadi Ahmed (41), na wenzake 9, sasa imepangwa kuunguruma katika Mahakama ya Rufani Dar es Salaam, Juni 10, mwaka huu.
 
Sheikh Faridi na wenzake wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama Kuu ya Zanzibar.
 
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mselem Ali Mselem, Mussa Juma, Azzan Khalid Hamdani, Suleiman Juma, Khamis Ali na Hassan Bakari, Ghalib Hamada Juma, Abdallah Saidi na Fikirini Fikirini.
 
Washtakiwa hao kupitia kwa mawakili wao, wamewasilisha maombi katika Mahakama ya Rufani Tanzania, wakiomba mahakama hiyo itupilie mbali rufaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Zanzibar, dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, wa Machi 11, mwaka huu.