Sunday 26 May 2013

MAALIM SEIF ASISITIZA ZANZIBAR YENYE MAMLAKA KAMILI !!!



Zanzibar: Kongamano la “Maridhiano ya Wazanzibari” limefanyika mjini hapa huku Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akitaka Zanzibar kujitawala wenyewe na kuwa na mamlaka kamili kwani ndiyo dhamira ya msingi wa ukombozi wa Mapinduzi ya Zanzibar.
Maalim Seif akifungua kongamano hilo mjini hapa jana, alisema kuwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yalikuwa na lengo la kuwafanya Wazanzibari wajitawale wenyewe na wawe na uamuzi wao kwa kila jambo.
Alisema dhamira hiyo ya Mapinduzi ilianza kukiukwa baada ya kutiwa saini kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao uliipunguzia Zanzibar mamlaka.
Alisema kwamba siyo kweli kuwa Wazanzibari hawataki Muungano bali wanataka muundo wa muungano uwe wa mkataba ili kuwapo Serikali za Tanganyika na Zanzibar zenye mamlaka kamili.
“Kuwa na mamlaka kamili siyo kwa maslahi ya watu wachache bali kwa watu wote. Ni kama mvua, yaani inaponyesha mimea yote inanawirika,” alisema Maalim Seif na kuongeza;
“Tunataka kurejesha heshima ya nchi yetu, tuwe Wizara yetu ya Mambo ya Nje, bendera yetu ipepee nchi za kigeni, Umoja wa Mataifa na Jumuiya zingine za Kimataifa zikiwamo Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki”.
Aidha, Maalim Seif aliipongeza Kamati ya Maridhiano chini ya Mwenyekiti wake, Hassan Nassor Moyo kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuyaendeleza maridhiano hayo na umoja wa Wazanzibari.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ambaye ni mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar, Hassan Nassor Moyo alisema maridhiano hayo yaliyoasisiwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, yameondoa fitina na chuki zilizodumu kwa muda mrefu miongoni mwa wananchi.
Kamati ya Maridhiano iliyoratibu kongamano hilo ilitoa mapendekezo yake ikitaka Zanzibar iwe na mamlaka yake kamili kwa kuwa na sarafu yake, mamlaka ya Mambo ya Nje, uraia wake, pasi yake ya kusafiria na wametaka Jeshi la Polisi lisiwemo kwenye mambo ya Muungano, gesi na mafuta yatakayopatikana Zanzibar yawe mali ya Zanzibar na pia suala la vyama vya siasa lisiwe la Muungano.
“Haya si maagizo bali ni mashauri yetu pindi mkiyakubali tunakuombeni kuyafanyia kazi katika kujadili na kupitisha Katiba Mpya,” alisema Mwenyekiti huyo katika taarifa iliyosomwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu.
Pia walitaka mipaka ya Zanzibar itambulike katika Katiba Mpya kama ilivyokuwa kabla ya Muungano Aprili, 1964.

No comments:

Post a Comment