Saturday 31 August 2013

DR SHEIN NUSKI HANA SHUKURANI MSHENZI . EDDIE RIYAMI ASEMA

MJUMBE wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Eddie Riyami, amesikitishwa na hatua ya kuvuliwa uanachama kwa aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mansour Yussuf Himid. Hata hivyo, mjumbe huyo amemshutumu Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, akisema kuwa ni mmoja kati ya wajumbe wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kutoka Zanzibar walioshiriki kikao hicho cha kumvua uanachama.

Akihojiwa na Radio ya Sauti ya Ujerumani (Deutsche Welle), katika kipindi Maalumu cha ‘Meza ya Duara’, Riyami alimtuhumu vikali Dk. Shein, akidai amekosa shukurani kwa Mansour na kumtaka kumuomba radhi.

“Shein amesahau kama Mansour ni mmoja kati ya Wazanzibari waliokwenda Dodoma kuhakikisha Dk. Shein anapita kuwania kiti cha urais wa Zanzibar, ili aendeleze maridhiano, namshangaa leo hii, Dk. Shein kuwa wa kwanza kupigania Mansour afukuzwe,” alisema Riyami.

Katika mahojiano hayo, Riyami alimsifu Mansour kuwa ni miongoni mwa vijana shupavu ndani ya CCM waliohakikisha Zanzibar inaingia katika siasa za maridhiano na chama cha upinzani cha CUF na hivyo kuondokana na siasa za chuki na uhasama zilizodumu kwa muda mrefu visiwani humo.

Riyami alisema Mansour hakustahili kufanyiwa aliyofanyiwa, na kusisitiza maoni aliyokuwa akiyatoa akiitaka Zanzibar kuwa na dola yake kamili, yalikuwa ni maoni yake akiwa kama Mzanzibari.

Kauli hiyo ya Riyami imekuja siku chache baada ya Mansour kufukuzwa uanachama wa CCM na kikao cha NEC, kilichokaa wiki hii mjini Dodoma, akituhumiwa kutamka hadharani misimamo yake inayokinzana na CCM.

Mansour alituhumiwa na kikao hicho kwa kushindwa kusimamia malengo, madhumuni na masharti ya chama pamoja na kukiuka maadili ya kiongozi kwa kukiuka Ilani ya chama hicho ya mwaka 2010.

Hata hivyo, kabla ya hukumu ya Mansour mjini Dodoma, kulikuwa na hali ya mvutano wa chini uliokuwa ukiendelea kati ya Dk. Shein na wajumbe wa Kamati ya Maridhiano, inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Mzee Hassan Nassor Moyo. 

Dk Shein aliwatuhumu wajumbe wa kamati hiyo kutoka CCM, akidai inakwenda kinyume na msimamo wa CCM unaotaka serikali mbili.

Dk. Shein anawatuhumu wajumbe wa kamati hiyo kutoka CCM ambao ni Mzee Moyo, Mansour na Riyami, pamoja na Aboubakar Khamis, Ismail Jussa na Salim Bimani, kwamba inawapotosha Wazanzibari juu ya muundo wa Muungano.

Katika moja ya mikutano yake ya kisiasa, Dk. Shein aliikana kamati hiyo na kusema haitambui na kuwataka wajumbe wake kuacha mara moja kile alichodai kutumia ‘mgongo’ wake katika kufikia malengo yao.

Katika mahojiano na Sauti ya Ujerumani, Riyami alisema kilichofanyika mjini Dodoma ni juhudi zinazoendelezwa na Dk. Shein za kutaka kuwaumiza wajumbe wa Kamati ya Maridhiano.

Riyami aliwatuhumu wajumbe wa NEC kutoka Zanzibar akisema, wamepatwa na ‘kihoro’ cha maridhiano yaliyofikiwa kati ya CCM na CUF, baada ya kuundwa kamati nyingi za muafaka ambazo hazikuzaa matunda.

“Hawa ndio wale wahafidhina waliokaa Dodoma kumfukuza Mansour, wamepatwa na kihoro, ziliundwa kamati za muafaka nyingi hazikuzaa matunda, kinachofanyika ni kisingizo cha kuwaumiza wajumbe wa kamati ya maridhiano,” alisema Riyami.

Riyami alisema kitendo alichofanyiwa Mansour hakiwashangazi, akidai vikao vinavyofanyika mjini Dodoma ni sehemu ya ‘machinjio’ ya kuwamaliza Wazanzibari.

Alitaja baadhi ya vikao vya NEC vilivyowahi kufanyika mjini Dodoma na kuamuru kuwafukuza unachama wa CCM, Maalim Seif Sharrif Hamad, Marehemu Shaban Mloo, Haji Duni, Marehemu Soud Yusuf Mgeni na aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi Zanzibar, Ramadhan Fakih.

Riyami alikumbusha tukio la mwaka 1984, ambako kulifanyika vikao vya NEC na kuamuru kumvua nyadhifa zake zote za urais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, akidaiwa kutaka kuusaliti Muungano.

“Haya ya Mansour wala hatuyashangazi…wala si ya ajabu na hili nalisema wazi pasipo na shaka, sitanii, Shein amwite Mansour amuombe radhi hadharani kwa kumdhalilisha mwanasiasa shupavu.

Leo wajumbe wa Kamati ya Maridhiano wanakutana katika Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar, kuzungumzia hatima ya kufukuzwa mjumbe mwenzao, Mansour, huku katika kikao hicho kitakachohudhuriwa na wajumbe wa CUF, Mansour anatarajiwa kutoa yaliyo moyoni mwake juu ya kadhia ya kufukuzwa kwake uanachama wa CCM.

Wednesday 28 August 2013

VIJANA WASEMA POPOTE PALE AENDAPO TUKO NAYE !!!


Wananchi mbali mbali wa jimbo la Kiembe Samaki wameelezwa kusikitishwa kwao na kitendo kilichofanywa na halmashauri kuu ya CCM NEC ya kumvua uanachama mwakilishi wa jimbo hilo hivi karibuni.

Mazrui media ilifanya jitihada za kuwatafuta wananchi wa jimbo hilo ili kuweza kujua wameipokeaje taarifa hii.

Mmoja miongoni mwa waliowahi kushika nyadhifa ya katibu wa tawi ndani ya jimbo hilo Bwana Sleiman Haroub Sleiman amesema kitendo cha kufukuzwa Mansour kimefanywa na baadhi ya timu maalumu ndani ya chama hicho ambayo inapingana na Raisi mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid karume.

Alisema kuwa ndani ya jimbo hilo kuna baadhi ya watu tena walio wengi sana hususani vijana walikuwa karibu sana na Mwakilishi huyo hivo kutokana na ukaribu wao hule lololote lile linaweza kutokea katika kipindi hichi ambacho nikigumu zaidi kwa wananchi wa kiembe samaki waliomchagua Mansur kuwa mwakilishi wao.

Alisema wananchi mbali mbali hivi sasa ni wazi kuwa wanalichukulia suala hili kuwa ni lakawaida ndani ya chama lakini mambo yanaweza kugeuka na kuathiri zaidi tofauti na tunavofikiria.

Kuhusu shutuma zinazosambazwa na baadhi ya watu kuwa Dodoma ni machinjio tu ya wazanzibar alieleza kuwa sio kweli inawezekana wanaofukuzwa wanakila sababu za kufanyiwa hivo.

Kwa upande alieleza kuwa yeye binafsi anaumwa sana na suala hili lakini yupo tayari kumuunga mkono kiongozi yoyote yule atakaeteuliwa na chama chake cha CCM ndani ya jimbo hilo.

Akifafanua kuhusu suala la kutokurudisha kadi za chama cha ccm sikumsaliti Mansour bali nikukiunga mkono chama chao kwani hata huyo Mansour aligombea kwa chama hicho hicho yeye yupo tayari kumuunga mkono kiongozi yoyote yule atakaependekezwa na chama.

Nae Katibu wa Vijana CCM katika jimbo hilo la kiembe samaki ambae hakutaka jina lake litajwe.
Alieleza kuwa hali ya kufukuzwa kwa Mansour imemuuma sana sana na aliposikia taarifa hii alikuwa chuoni Tunguu kutokana na hali yake kubadilika mara moja aliamua kutoka nje ya darasa na kushindwa kabisa kuendelea na masomo kwa siku hio.

Alisema kuwa kila mmoja anajuwa wazi kuwa chama kimekurupuka juu ya hili na kilitakiwa kitulize wananchi kwanza hata kama Mansour alikuwa na kosa ndani ya chama hicho,cha msingi zaidi wangetumia busara kwa kumuangali mtu wenyewe ana umuhimu gani ndani ya jimbo lake.



Hata hivyo licha ya mwakilishi huyo kuwa na msimamo wa kuwepo serikali tatu sikosa kisheria kwani hayo yalikuwa mawazo yake na hakuna asiejua kwamba Mansour hakuwa pekeake mwenye msimamo huo ndani ya CCM kwanini afukuzwe yeye tu.

‘’Mh,Mansour siku zote alikuwa karibu na vijana na alitusaidia kwa hali na mali unadhani leo ni mwakilishi gani au kiongozi gani atakaekuwa kama yeye ndani ya jimbo hili’’alieleza.

Nae Nassra Mwinyi Chumu ambae ni mkaazi wa jimbo hilo alieleza wazi kwamba yeye binafsi hakuridhishwa kabisa na kitendo hicho na yupo tayari kumfata Mansour popote pale atakapokwenda kwani tayari amekuwa msaada mkubwa kwa jimbo hilo.

Aidha kwa upande wao vijana wa Manour maskani iliopo Chukwani wamesema kwamba wao binafsi hawataki kusikia lolote isipokuwa wanasubiri kauli yake yeye mwenyewe atasemaje na watamfuata kwa halili yoyote hile.

‘’Unajua nini kaka jamaa alikuwa na moyo wa imani sana na mpenda watu wote hususan vijana hapa maskani petu palikuwa kama nyumbani kwake’’walieleza vijana hao ambao hawakutaka watajwe majina yao.

Kwa upande wake Bwana Mansour Yussuf Himed wakati akifanya mahojiano na kituo cha habari cha DW cha Ujerumani alisema kuwa kwa sasa bado ni mapema mno kutoa tamko lolote lakini yeye ameyapokea maamuzi yalioamuliwa na chama kama yalivotolewa na chama hicho.

Akieleza kuhusu suala lakuvuliwa uanachama na hali yakuwa Bababa yake ni mmoja miongoni mwa waasisi wa mapinduzi ameleza kwamba wenzake ndio wameamua kufanya hivo hivo hana budi kukubaliana nayo maamuzi hayo.

Alieleza kwamba nchi yoyote hile yenye kuheshimu sheria ni lazima katiba yake ikushanye mawazo ya wananchi wake katika utungwaji wa katiba na hatimae mawazo ya waliowengi kusikilizwa nanadhani hio ingekuwa busara zaidi.

Licha ya hayo Mansour alifafanua kwamba muda ukifika atasema hadharani kwani ana mingi yakusema.

CCM ZANZIBAR WAZUSHI FITNA !!!

Na Ismail Jussa. MANSOOR Yussuf Himid. Jina hili sasa huwezi kulitenganisha na matakwa halali ya Wazanzibari walio wengi wanaotaka Zanzibar irejeshe hadhi yake kama nchi yenye MAMLAKA KAMILI kitaifa na kimataifa. Kitendo cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumfutia uanachama wake jana ni kitendo cha kujiangamiza chenyewe katika siasa za sasa za Zanzibar ambazo zimetawaliwa na hoja moja kuu ambayo ni Mamlaka Kamili.
Tangu hapo vijana wengi wa CCM/Zanzibar wa kizazi kipya walishaonesha mwelekeo wa kupoteza imani na chama chao kutokana na ukakasi wa viongozi wake muflisi kushindwa kusimamia matakwa na maslahi ya Wazanzibari na badala yake kuonekana kama ni mawakala wa ukoloni wa Tanganyika dhidi ya Zanzibar.
Rais Ali Mohamed Shein, Balozi Seif Ali Iddi, Vuai Ali Vuai na Sekretarieti ya akina Haji Mkema, Hamad Masauni na Waride Bakari Jabu hawaonekani kuwakilisha hisia za Wazanzibari.
Kielelezo thabiti cha hali hiyo kilionekana pale mamia ya vijana wa CCM walipoonekana kupanga misururu mirefu huko Matemwe na Kitope kurejesha kadi za kijani kwa kiongozi waliyempa matumaini yao Maalim Seif Sharif Hamad.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula. Yeye anataka Muungano wa Serikali Moja. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula. Yeye anataka Muungano wa Serikali Moja. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Hali kama hiyo ikajitokeza kwa wazee wa CCM wa maeneo yenye ngome zao Pemba kama Kangagani ambao nao walirudisha kadi huku wakiomba msamaha kwa kuchelewa kufahamu kuwa kumbe CCM hakipo kwa maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari.
Katika hali kama hiyo ungetegemea chama makini na kinachojikosoa kingejirudi na kujitazama upya. Lakini wapi? Wahenga walisema: La kuvunda halina ubani.
Ni juzi tu nilipokuwa nikihutubia mkutano wa hadhara hapo katika viwanja vya Komba Wapya niliwaambia wanachama wa CCM na hususan vijana kwamba mpaka lini wataendelea  kukubali Dodoma kuwa machinjio ya kisiasa ya viongozi wa Zanzibar?
Alianza Aboud Jumbe mwaka 1984, akafuata Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake sita mwaka 1988, akaja Dk. Salmin Amour alipojiunga na OIC mwaka 1993 na sasa tena mwaka 2013 anadhalilishwa Mansoor Yussuf Himid kwa sababu tu amethubutu kukhitilafiana na watawala wa Dodoma kwa kusimamia kidete hoja ya Mamlaka Kamili.
Nikasema umefika wakati wana-CCM wa Zanzibar na hasa vijana kujiuliza hichi kweli ni chama chao na kipo kwa maslahi yao? Hichi kweli ndicho mzawa na mrithi wa kisiasa wa Afro-Shirazi Party (ASP)?
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai (Mbunge wa CCM). Naye anataka Serikali Tatu. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai (Mbunge wa CCM). Naye anataka Serikali Tatu. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wa kumfuta uanachama Mansoor ni ujumbe tosha kwamba yeyote atakayesimamia maslahi ya Zanzibar hana nafasi kwenye chama hicho. Kwa lugha nyingine, Zanzibar na CCM ni Lila na Fila, hazitangamani.
Na tazama hata majibu ya Katibu Mwenezi wa CCM wa upande wa Tanganyika, Nape Nnauye, alipoulizwa autaje usaliti wa Mansoor anaodaiwa kuufanya dhidi ya Chama. Alisema ni pale Mansoor aliposimama ndani ya Baraza la Wawakilishi mwaka 2009 na kusema Serikali ya Muungano ni wizi wa mchana kweupe wa rasilimali za Zanzibar. Swali la kumuuliza Nape ni kwamba je, madai hayo ni uongo?
Lakini hebu tuje kwenye hilo la kutetea msimamo wa muundo wa Muungano wa Mkataba unaokwenda kinyume na sera ya CCM ya Serikali Mbili. Kama hilo ni kosa mbona aliyeadhibiwa ni Mansoor peke yake?
Wajumbe vigogo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ndiyo iliyokuja na pendekezo la muundo wa Shirikisho la Serikali Tatu, wakiwemo Jaji Joseph Warioba, Salim Ahmed Salim na Joseph Butiku, ni wanachama wa CCM mbona hawakufukuzwa?
Beatrice Shelukindo, Mbunge wa CCM. Serikali Tatu. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Beatrice Shelukindo, Mbunge wa CCM. Serikali Tatu. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Mwaka 1994 Kundi la Wabunge 55 maarufu kama G-55 walipeleka hoja Bungeni na hoja ikapitishwa na Bunge zima ya kuanzisha Serikali ya Tanganyika kinyume na sera ya CCM. Mbona hawakufukuzwa?
Katika huu mjadala unaoendelea wamejitokeza wabunge kama Esther Bulaya na Beatrice Shelukindo na hivi karibuni Naibu Spika Job Ndugai kutetea mfumo wa Shirikisho la Serikali Tatu. Mbona hawakufukuzwa?
Achilia mbali hao, hata Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula alisema yeye msimamo wake ni kutaka mfumo wa Serikali Moja tu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jambo ambalo ni kinyume na sera ya Chama chao mbona hakufukuzwa?
Kwa nini Mansoor Yussuf Himid peke yake? Kwa mtazamo wangu mimi Mansoor ameadhibiwa kwa sababu ya msimamo wake aliouchukua katika kuleta amani kupitia Maridhiano ya Wazanzibari ambayo wahafidhina wa CCM/Zanzibar na wale wenye kujali matumbo yao tu hawakuyataka na mpaka leo hawajayaridhia na wakipata nafasi wanayamezea mate wayavuruge.
Wanaona Maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyopatikana kupitia Maridhiano hayo yamewatiribulia nafasi za kuwa Mawaziri au Manaibu Waziri na pia kufanya watakavyo kujinufaisha wao na aila zao huku watoto wa wanyonge, wakwezi na wakulima wakiendelea kusaga meno.
Esther Lubaya, Mbunge wa CCM. Anataka Serikali Tatu. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Esther Lubaya, Mbunge wa CCM. Anataka Serikali Tatu. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Na la pili ndilo hili la kusimama bila ya kuyumba kwenye hoja ya MAMLAKA KAMILI kwa Zanzibar, msimamo ambao unakwenda kinyume na misingi ya CCM iliyoachwa na mwasisi wake Julius Nyerere.
Ala kulli hali, hukumu imeshapitishwa na Mansoor Yussuf Himid siyo tena mwanachama wa CCM.
Kwa jinsi nimjuavyo Mansoor hakuyumbishwa na uamuzi huu na kwa hakika akiutarajia. Natambua jinsi alivyo jasiri, shupavu, mkweli na mzalendo na hivyo najua hatotetereka katika kuendeleza msimamo wake na kuendeleza harakati za Mamlaka Kamili kwa Zanzibar.
Nilikuwa namheshimu sana na kwa kule kuonesha kwake mfano katika kusimamia anachokiamini. Sasa namheshimu zaidi.
Sina shaka kwamba huu si mwisho wa Mansoor kisiasa bali naamini kwa dhati kuwa hatua ya leo ndiyo mwanzo wa kupaa kisiasa Mansoor Yussuf Himid. Nilicho na uhakika nacho ni kwamba huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM katika medani za siasa za Zanzibar. Kwa sababu ya chuki, choyo na visasi wamechukua maamuzi ya hasira ya kujipiga wenyewe risasi mguuni.
Mwaka 1988, CCM iliwatengenezea Wazanzibari shujaa Maalim Seif Sharif Hamad. Tuna furaha kuwa sasa 2013 imetutengenezea shujaa mwingine wa Zanzibar, Mansoor Yussuf Himid. Wazanzibari tumempokea kwa mikono miwili. Wakiungana mashujaa wawili hawa hakuna wa kuzuia wimbi kubwa la mabadiliko linalokuja. A’luta Continua!
Ismail Jussa ni mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe. Naye, kama alivyo Mansoor Yussuf Himid, ni mjumbe wa Kamati ya Maridhiano inayoongozwa na mwanaCCM Hassan Nassor Moyo.

TANGAZO KWA WAZANZIBAR WAPENDWA WENYE KUTAKA ZANZIBAR YENYE MAMLAKA KAMILI !!!

Tulikua kwenye kona sasa tupo kwenye barabara kuu,mwendo mdundo.

Ile safari ya kuelekea jamuhuri ya wati wa zanzibar yenye mamlaka kamili inaendelea.

Usikose kuhudhuria ukimbi wa Salama Hall Bwawani jumamosi ya tarehe 31/08/2013 saa 2:00 asubuhi.

Shujaa wa Zanzibar mtoto wa mwana mapinduzi Mansour Yussuf Himed atanguruma akishindikizwa na Ismail Jussa Ladhu .

Mzee Hassan Nassour Moyo atakuwepo na kamati ya maridhiano itatoa tamko lake juu ya mamlaka kamili ya Zanzibar.

Zanzibar jamuhuri inachomoza.
Jamuhuri ya watu wa Zanzibar kwanza.

CHINJIO DODOMA KWA WAZANZIBAR LINAMAKALI.KWA WATANGANYIKA BUTU !!!

CCM inaenda kinyume na Mapinduzi ya Zanzibar

Waasisi wa Mapinduzi ambao leo watoto wao wanafukuzwa

Na Salim Salim

MACHINJIO ya Wazanzibari yameendelea kuwachinja Wazanzibari, mara hii wamemchinja Mtoto wa MwanaMapinduzi, Mansour Yussuf Himid,Mzanzibari Kindakindaki, Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki ambako mimi ni mkaazi. 

Sababu kuu ya kumchinja Mansour ni ile kauli yake ya kuunga mkono Muungano wa Mkataba ambao utarudisha Mamlaka Kamili Zanzibar katika mfumo wa Muungano.

Sisi wananchi wa Jimbo la Kiembesamaki tumefadhaika, tumeduwaa, tumeachwa mdomo wazi, huku tukisubiri kauli ya Mwakilishi wetu ili tuifanyie kazi.

Sio sisi wananchi wa Kiembesamaki peke yetu tulioduwaa na kufadhaishwa na wanaoisubiri kauli ya Mansoor ili waifanyie kazi, ni wananchi wote Wazanzibari, Unguja na Pemba, mashamba na Mjini.

Watu wamekata tamaa na CCM na wengi wana CCM wametamka hadharani watarudisha kadi CCM. 

Wazanzibari wamechoshwa na Machinjio ya Dodoma, leo ni Mansour, kesho Mwana CCM Zanzibari mwengine.

Swali lipo hapa, kwa nini ni Wazanzibari peke yetu tunaochinjwa Dodoma? Hatujapata kusikia chinjio hili likimchinja Mtanganyika.

Huenda labda kwa Watanganyika chinjio hiloni butu.

Tumeyashuhudia ya Aboud Jumbe, ya MaalimSeif na wenzake, ya Salmin Amour kutakiwa aitoe Zanzibar kutoka Jumuiya ya Organization of Islamic Conference na leo kufukuzwa Mansoor Yussuf Himid.

Tayari pia kuna wito wa kudai Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, afukuzwe Serikalini kwa kuunga mkono Rasimu ya Katiba yenye mfumo wa Muungano wa Serikali Tatu.

Maneno yanafika mbali zaidi kuwa hata Maalim Seif, Makamu wa Kwanza wa Rais, ambaye ameekwa Serikalini na Katiba ya Zanzibar pia afukuzwe kazi.

Kikubwa zaidi wenye kuchongea mambo yote hayo wanatamani Umoja wa Kitaifa Zanzibar uvunjike ili turudi nyuma tulipotokaambapo kila mwananchi wa Zanzibar hataki turudi huko.

Na kuibadili Katiba ya Zanzibar hawawezi. Kwanza hawana thuluthi mbili ndani ya Baraza la Wawakilishi lakini pia ni lazima waitishe Kura ya Maoni kuiondoa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hakuna mwananchi hata mmoja wa Zanzibar atakaye sema “Ndio Serikali ya Umoja wa Kitaifa iondoke”, isipokuwa labda wao, nao ni wachache.

Lakini yote haya yanatokea wakati Bunge Maalum la Katiba linakaribia kuundwa. Ni dhahiri kwamba lengo ni kuwatisha Wawakilishi na Wabunge watakaoteuliwa katika Bunge hilo wasende kusimamia hoja ya Mamlaka Kamili Zanzibar. 

Wahafidhina wa CCM/Zanzibar wanajidanganya; hakuna atakayetishika kuhusu hili.

Kufanya hivi wanadhani watawanyamazisha Wazanzibari; kufanya hivi wanadhani watairudisha haki nyuma; haki haijawahi kurudi nyuma. Siku zote haki huenda mbele hata ukiichelewesha kwa miaka mia.

Wazanzibari tulifanya Mapinduzi ili tuwe Huru. Wazanzibari hatukufanya Mapinduzi ili tuungane na Tanganyika. Tulifanya Mapinduzi ili tujitawale na lengo kuu ili tuweHuru, kukataa Zanzibar yenye Mamlaka Kamili ni kuyapinga Mapinduzi ya Zanzibar.

Mansoor na wenzake wanayalinda Mapinduzi ya Zanzibar kwani wanaujua msingi, malengo na sababu ya kufanyika kwake.
Suala la kutoa maoni ni haki ya kila mmoja wetu. Ni haki yetu ya kimaumbile na ni haki ya Kikatiba.

Wakati mchakato wa Katiba mpya ulipoanza viongozi wetu walituhimiza tusema chochote tunachokitaka. Rais Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo sehemu tafauti. Mara mbili alitwambia hayo uwanja wa Aman na wakati wa kuizindua Tume ya Katiba, Rais Jakaya Kikwete naye kayasema hayo mara kadhaa na hata alipokuwa analifungua Baraza la Katiba la CCM alisema wastahamiliwe wenye maoni tofauti na Chama. 

Nashangaa leo kumwona mwenye maoni tofauti na wao wamemfukuza CCM.

Rais Kikwete wakati anaizindua Tume ya Katiba alisema hata watakaotoa maoni ya kipuuzi wasikilizwe. Hiyo ndiyo CCM.

Uzuri wa mambo Mansoor amefukuzwa Chama, hajapokonywa Uzanzibari wake.

Kufukuzwa kwa Mansoor ni ushindi kwa wanaopigania Zanzibar irejeshewe Mamlaka Kamili na wananchi wote wa Zanzibar kwa ujumla. Huyu ni Shujaa wa Zanzibar, na mtetezi wa haki ya Zanzibar.

Hongera Mwana Mapinduzi, Hongera Shujaa wetu Mansoor Yussuf Himid. Mamlaka Kamili yatasimama japokuwa wapinzani wanachukia.

Sunday 18 August 2013

CCM ZANZIBAR IMECHACHA !!!

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimemeguka baada ya Kamati Maalumu kumvua uanachama Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mansoor Yussuf Himid, akidaiwa kukiuka maadili ya chama hicho. Uamuzi huo umekuja baada ya Mansoor kudaiwa kupingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, inayoamini katika muundo wa Serikali mbili.

Chanzo cha kuaminika kutoka katika kamati hiyo, kiliiambia MTANZANIA jana kuwa uamuzi wa kumvua uanachama Mansoor uliwasilishwa katika kikao kilichofanyika CCM Kisiwandui chini ya Makamu Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Kwa mara ya kwanza, tuhuma za Mansoor zilifikishwa katika kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM Zanzibar, kilichoketi Agosti 16, 2013 katika Ofisi za CCM Kisiwandui ambapo wajumbe wa kamati hiyo kwa kauli moja walitoka na azimio la kumfuta uanachama mwakilishi huyo.

Dk. Shein ndiye aliyeongoza kikao cha Kamati ya Maadili, huku wajumbe wakiwa ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, Mohamed Hija, Mbaruk Rashid Omari na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd.

Chanzo hicho kutoka ndani ya CCM Zanzibar, kilisema tuhuma za Mansoor zilizowasilishwa zilikuwa tatu, huku ya kwanza ikiwa ni kushindwa kusimamia malengo, madhumuni na masharti ya chama.

Aidha, Mansoor anadaiwa kutokusimamia wajibu wa mwanachama kwa kukiuka maadili ya kiongozi wa CCM, kwa kukiuka Ilani ya chama hicho ya mwaka 2010.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa suala la kufukuzwa uanachama kwa mwakilishi huyo lilizua mjadala mzito katika kikao cha jana, lakini baadaye wajumbe walikubaliana kwa kauli moja kufukuzwa kwake.

Mansoor amekuwa miongoni mwa Wazanzibari walio katika safu ya mbele kutetea muundo wa Muungano utakaoipa Zanzibar mamlaka kamili ya dola.

Chanzo hicho kilizidi kusema kuwa suala la mwakilishi huyo kutakiwa kuwasilisha utetezi dhidi ya tuhuma zake, lilianzia katika kikao cha CCM Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo alisema kama kufungwa afungwe lakini atasimamia Muungano wa mkataba pamoja na mamlaka kamili.

“Katika kikao cha mkoa alitoa utetezi wake na kusema kama kufungwa afungwe, kama kunyongwa anyongwe na kama kufukuzwa afukuzwe, lakini anataka Serikali ya mkataba.

“Wakati anatoa utetezi wake, Mansoor, alikuwa anatumia nakala moja ya gazeti la wiki la Julai 26, mwaka huu na kumtuhumu Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, kuwa naye anavunja Katiba ya CCM,” kilisema chanzo hicho.

Kutokana na misimamo yake, Mansoor, anaaminika zaidi kwa Wazanzibari hususani wale wanaoamini katika Muungano wa mkataba pamoja na madaraka kamili ya dola ya Zanzibar.

MTANZANIA ilipomtafuta Msemaji wa CCM upande wa Zanzibar, Waride Bakari Jabu, atoe ufafanuzi wa suala hilo, alisema yupo katika kikao.

“Kwa sasa siwezi kusema jambo lolote mwanangu, nafikiri unasikia sauti za wajumbe wakizungumza, nipo katika kikao na siwezi kusema jambo lolote kwa sasa,” alijibu kwa kifupi Waride.

Historia yake

Katika uchaguzi wa mwaka 2005, Mansoor, alichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki kupitia CCM, nafasi ambayo amedumu nayo hadi sasa.

Pia ni mwanachama wa CCM aliyewahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu (NEC) na Mweka Hazina wa CCM upande wa Zanzibar kati ya mwaka 2002 hadi mwaka 2012.

Nje ya CCM, ameshika nyadhifa mbalimbali za uwaziri katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Mwaka 2000 hadi mwaka 2004, alikuwa Naibu Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, na kati ya mwaka 2004 hadi mwaka 2010 alikuwa waziri kamili katika wizara hiyo na baadaye mwaka 2010 hadi mwaka 2012, alikuwa Waziri wa Kilimo na Rasilimali.

Aidha, alihudumu kama mjumbe wa Baraza la Biashara la Zanzibar kati ya mwaka 2002 hadi 2012.

Kutokana na misimamo yake ndani na nje ya chama na Serikali, Oktoba 15, 2012, Dk. Shein ilimlazimu kufuta uteuzi wake kwa Mansoor kuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi.

Mansoor ni mwanasiasa na mfanyabiashara aliyezaliwa Novemba 3, 1967 kisiwani Unguja. Alisoma masomo yake ya msingi na sekondari nchini India kati ya mwaka 1976 na 1987.

Kabla ya kuingia rasmi katika siasa mwaka 2000, aliteuliwa kuwa mjumbe katika Baraza la Wawakilishi na alijihusisha katika biashara ya hoteli.

Mwanasiasa huyo ni mtoto wa Mkuu wa Kwanza wa Jeshi la Zanzibar baada ya Mapinduzi, Brigedia Jenerali Yussuf Himid.

Amekuwa akisimamia maridhiano ya Wazanzibari na Umoja wa Kitaifa akiwa mmoja wa wajumbe sita wa Kamati ya Maridhiano aliyoshiriki kikamilifu kuyaanzisha mwaka 2009.

Pia ni miongoni mwa Wazanzibari walio mstari wa mbele kutetea muundo wa Muungano, utakaoipa Zanzibar mamlaka kamili ya dola.

Wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni Mwenyekiti Hassan Nassor Moyo (CCM), Eddie Riyami (CCM), Abubakar Khamis Bakari (CUF), Ismail Jussa Ladhu (CUF) na Salim Bimani (CUF).

Saturday 17 August 2013

AWASHANGAA WANAOTAKA ZANZIBAR IENDELEE KUWA MANISPAA !!!



Mwanasheria Mkuu SMZ: Serikali Mbili zitavunja Muungano

Awashangaa wanaotaka Zanzibar iendelee kuwa manispaa

Asema kutokuwepo Serikali ya Tanganyika ndio kero Kuu ya Muungano

Awasuta wanaotaka Serikali Mbili

Na Salim Salim

Mwanaseria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar leo amesema lengo la kuandikwa kwa Katiba Mpya si kuyafanyia Marekebisho katiba iliyokuwepo sasa bali ni kandika Katiba Mpya katiba ambayo itakuwa Muarubaini kwa kero za Muungano na Muungano wenyewe.

Mwanaseheria Mkuu liyasema hayo leo asubuhi alipokwa akifunguwa Baraza la Katiba la Vyuo Vikuu liliondaliwa na ZAHILFE Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Zanzibar liliofanyika katika Ukumbi wa Salama Hal Bwawani.

Alilisifu Baraza hilo na kusema kuwa ni Baraza la Vijana wasome na kuwasifu Vijana kwa ile sifa yao kubwa ya kuleta mapinduzi katika jamii yeyote.

Alimtaja kijana Sir King ndie waliosababisha Zanzibar iiteme Tanganyika mwaka 1895 Ogast na Tanganyika kuangukia katika mikono wa Wajerumani.

Na kumtaja Gerald Pota alietumwa na Waingereza kuja kuunda Serikali na kumpangia Mfalme mshahara ambako alikuwa akilipwa paund 250 kwa mwaka.

Msingi wa Muungano wa Tanzania ni kuungana kwa Nchi mbili huru Tanganyika na Zanzibar lengo la kuungana kwa nchi mbili hizi ni kufanya mambo yao pamoja na kupata faida zaidi na sio Nchi moja kuitawala Nchi nyengine alisema, hukua akiendela kusema:

Zanzibar si mkowa wala wilaya, Zanzibar ni Nchi, katika Muungano tulikubaliana baadhi ya mambo kufanya pamoja na sio Zanzibar kuwa Jimbo la Tnganyika.

Alisema duniani kuna miungano mingi mizuri akiutolea mfano Muungano wa Uswis ambao una Serikali 24 na ule wa Muungano wa Maerkali wenye Serikali 52 na kusema kuwa ni uongo kuwa Serikali Tatu zitavunja Muungano na kusema Serikali Mbili ndizo zitakazovunja Muungano, na hata Muungano wa Serikali Tatu ukivunjika si kioja.

Serikali Tatu hazitovunja Muungano Serikali Mbili ndizo zitakazo vunja Muungano.

Alisema Uruhani wa Serikali ya Tanganyika ndio kero kubwa ya Muungano na Serikali tatu itairudisha Serikali ya Tanganyika ambako kero kubwa itakuwa ishatatuliwa.

Aliitaja Sheria ya Kuanzishwa na Bank Kuu ya Tanzania kuwa aliisaini Karume mwenyewe lakini Karume alipoona mapungufu ya Seria hiyo ndio maana akaanzisha PBZ.

Aidha alisema kama Zanzibar inataka kuishtaki TFF itashinda na TFF haitokuwemo FIFA kwani TFF haiwakilishi Tanzania kama ilivyokuwa ZFA ilivyokuwa haiwakilishi Tanzania.

Hivi hatuoni haya kubakia hivi hivi kuwa Manispaa wakati Zanzibar ilikuwa Empire alihoji Mwanasheria Mkuu na kuendelea kusema hivi tutamuamini vipi mtu ambae leo anasema Zanzibar si Nchi atakapokuwa Rais wa Tanzania ambao Zanzibar haitokuwa na Mamlaka atasema Zanzibar ni jimbo la Tanganyika na kumalizia kusema wengi wa Watanganyika wanachuki na Zanzibar.

Aliwataka wanafunzi hao kuzungumzia mambo ya Muungano na kutaka kuwe na usawa "Bila ya kuwa na usawa katika Mungano huu huo si Muungano bali ni ukoloni" alisema, na kutaka kuwe na mfumo wa usawa katika Baraza la Mawaziri na Bunge na kuwe na makubaliano ya thuluthi mbili kila upande katika kupitisha sheria na kuengezwa au kupunguzwa mambo ya Muungano.

Alisema katika Muungano wa Serikali Tatu ni lazima Rasilimali zitumike kwa Usawa na sio kama hivi sasa Tanganyika inavyotumia Rasilimali za Muungano wao peke yao katika kusoma na kuinyima Zanzibar.

Tume ya Pamoja ya Fedha haijaanza kazi mpaka leo, na katika Muungano kuna mapato ya Muungano na Matumizi ya Muungano na Mapato ya Muungano siku zote huwa mengi ambako Tnganyika hawataki tugawane.

Alisema si kweli kama Muungano wa Serikali tatu una harama bali Muungano wa Serikali Mbili ndio wenye gharama na Zanzibar ndio inaharamika zaidi, aliwataka viongozi wawe wakweli na waache kuwapotosha wananchi.

Aliwaonya Wazanzibar kuwacha kulumbana na badala yake kukaa pamoja kuidai nchi yao.

Alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliundwa ili kuondowa tofauti kwa Wazanibar na kusema kuwa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kuala gumu kuliko mabadiliko ya Muungano.

Alisema Wanaotaka Seriakali Mbili hoja zao hazina msingi na hakuna haja ya kubakia kwenye Serikali mbili na wengi wanaotaka Serikali Mbili wanalinda maslahi yao ya kidunia.

Hoja yangu nawataka wanaotaka Serikali Mbili na Wanaotaka Mkataba wakae pamoja wajadiliano Mfumo wa Muungano wa Serikali Tatu mfumo ambao utakuwa na Mslahi na Zanzibar.

Awali Mwenyekiti wa ZAHILFE alikanusha taasisi yake kuandaa kungamano la tarehe 6 mwezi wa 7 lililofanyika Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kingeni na badala yake kongamano hilo liliandaliwa na Mkowa wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vywa CCM na kusema Taasisi yake haina mafungamano na chama chochote cha siasa.

Kongamano hilo lilianza na Wimbo wa Taifa wa Zanzibar na lilihudhuriwa na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Marais 10 wa Serikali za Wanafunzi waliochangia katika Kongamano hilo walitaka Zanzibar yenye Mamlaka Kamili na Usawa Katika Muungano.

Sunday 11 August 2013

TAARIFA YA KIZUSHI YA JESHI LA POLISI KUHUSU SHEIKH PONDA !!!

Sheikh Ponda Issa Ponda Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, akiwa katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wizara ya Mambo ya Ndani.
Jeshi la Polisi Tanzania.
Dar es Salaam
Agosti 10, 2013
1. Mnamo tarehe 10, Agosti, 2013, majira ya saa 8 mchana, maeneo ya shule ya msingi ya kiwanja cha ndege manispaa ya Morogoro kulifanyika kongamano la Baraza la Eid lililoandaliwa na Umoja wa wahadhiri mkoani Morogoro,
Dakika chache kabla ya kongamano hilo kumalizika alifika Shekhe Ponda issa Ponda alizungumza kwa muda mfupi.
2. Kongamano hilo ambalo lilifungwa majira ya saa 12:05 jioni,
Ambapo watu walianza kutawanyika, baadhi yao wakiwa wamezingira gari dogo alilokuwa amepanda Shekhe Ponda baada ya kutoka katika eneo hilo, askari wa Jeshi la Polisi walilizuia gari hilo kwa mbele kwa nia ya kutaka kumkamata Shekhe Ponda ambaye anatuhumiwa kwa kosa la kutoa maneno ya uchochezi sehemu mbalimbali hapa nchini yenye mlengo wa kusababisha uvunjifu wa amani.
3. Baada ya askari kutaka kumkamata, wafuasi wake walizuia ukamataji huo kwa kuwarushia mawe askari wa Jeshi la Polisi, kufuatia na purukushani hizo askari walipiga risasi hewani kama onyo la kuwatawanya.
4. Katika vurugu hizo, wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha mtuhumiwa, hivi sasa imethibitishwa kuwa Shekhe Ponda yupo katika hospitali ya taifa ya Muhimbili akitibiwa majeraha katika bega la mkono wa kulia linalodaiwa alilipata katika purukushani hizo.
5. Kufuatia tukio hilo timu inayoshirikisha wajumbe toka jukwaa la haki jinai ikiongozwa na CP Issaya Mngulu imeanza kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

SSP Advera Senso
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania.