Sunday 18 August 2013

CCM ZANZIBAR IMECHACHA !!!

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimemeguka baada ya Kamati Maalumu kumvua uanachama Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mansoor Yussuf Himid, akidaiwa kukiuka maadili ya chama hicho. Uamuzi huo umekuja baada ya Mansoor kudaiwa kupingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, inayoamini katika muundo wa Serikali mbili.

Chanzo cha kuaminika kutoka katika kamati hiyo, kiliiambia MTANZANIA jana kuwa uamuzi wa kumvua uanachama Mansoor uliwasilishwa katika kikao kilichofanyika CCM Kisiwandui chini ya Makamu Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Kwa mara ya kwanza, tuhuma za Mansoor zilifikishwa katika kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM Zanzibar, kilichoketi Agosti 16, 2013 katika Ofisi za CCM Kisiwandui ambapo wajumbe wa kamati hiyo kwa kauli moja walitoka na azimio la kumfuta uanachama mwakilishi huyo.

Dk. Shein ndiye aliyeongoza kikao cha Kamati ya Maadili, huku wajumbe wakiwa ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, Mohamed Hija, Mbaruk Rashid Omari na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd.

Chanzo hicho kutoka ndani ya CCM Zanzibar, kilisema tuhuma za Mansoor zilizowasilishwa zilikuwa tatu, huku ya kwanza ikiwa ni kushindwa kusimamia malengo, madhumuni na masharti ya chama.

Aidha, Mansoor anadaiwa kutokusimamia wajibu wa mwanachama kwa kukiuka maadili ya kiongozi wa CCM, kwa kukiuka Ilani ya chama hicho ya mwaka 2010.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa suala la kufukuzwa uanachama kwa mwakilishi huyo lilizua mjadala mzito katika kikao cha jana, lakini baadaye wajumbe walikubaliana kwa kauli moja kufukuzwa kwake.

Mansoor amekuwa miongoni mwa Wazanzibari walio katika safu ya mbele kutetea muundo wa Muungano utakaoipa Zanzibar mamlaka kamili ya dola.

Chanzo hicho kilizidi kusema kuwa suala la mwakilishi huyo kutakiwa kuwasilisha utetezi dhidi ya tuhuma zake, lilianzia katika kikao cha CCM Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo alisema kama kufungwa afungwe lakini atasimamia Muungano wa mkataba pamoja na mamlaka kamili.

“Katika kikao cha mkoa alitoa utetezi wake na kusema kama kufungwa afungwe, kama kunyongwa anyongwe na kama kufukuzwa afukuzwe, lakini anataka Serikali ya mkataba.

“Wakati anatoa utetezi wake, Mansoor, alikuwa anatumia nakala moja ya gazeti la wiki la Julai 26, mwaka huu na kumtuhumu Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, kuwa naye anavunja Katiba ya CCM,” kilisema chanzo hicho.

Kutokana na misimamo yake, Mansoor, anaaminika zaidi kwa Wazanzibari hususani wale wanaoamini katika Muungano wa mkataba pamoja na madaraka kamili ya dola ya Zanzibar.

MTANZANIA ilipomtafuta Msemaji wa CCM upande wa Zanzibar, Waride Bakari Jabu, atoe ufafanuzi wa suala hilo, alisema yupo katika kikao.

“Kwa sasa siwezi kusema jambo lolote mwanangu, nafikiri unasikia sauti za wajumbe wakizungumza, nipo katika kikao na siwezi kusema jambo lolote kwa sasa,” alijibu kwa kifupi Waride.

Historia yake

Katika uchaguzi wa mwaka 2005, Mansoor, alichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki kupitia CCM, nafasi ambayo amedumu nayo hadi sasa.

Pia ni mwanachama wa CCM aliyewahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu (NEC) na Mweka Hazina wa CCM upande wa Zanzibar kati ya mwaka 2002 hadi mwaka 2012.

Nje ya CCM, ameshika nyadhifa mbalimbali za uwaziri katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Mwaka 2000 hadi mwaka 2004, alikuwa Naibu Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, na kati ya mwaka 2004 hadi mwaka 2010 alikuwa waziri kamili katika wizara hiyo na baadaye mwaka 2010 hadi mwaka 2012, alikuwa Waziri wa Kilimo na Rasilimali.

Aidha, alihudumu kama mjumbe wa Baraza la Biashara la Zanzibar kati ya mwaka 2002 hadi 2012.

Kutokana na misimamo yake ndani na nje ya chama na Serikali, Oktoba 15, 2012, Dk. Shein ilimlazimu kufuta uteuzi wake kwa Mansoor kuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi.

Mansoor ni mwanasiasa na mfanyabiashara aliyezaliwa Novemba 3, 1967 kisiwani Unguja. Alisoma masomo yake ya msingi na sekondari nchini India kati ya mwaka 1976 na 1987.

Kabla ya kuingia rasmi katika siasa mwaka 2000, aliteuliwa kuwa mjumbe katika Baraza la Wawakilishi na alijihusisha katika biashara ya hoteli.

Mwanasiasa huyo ni mtoto wa Mkuu wa Kwanza wa Jeshi la Zanzibar baada ya Mapinduzi, Brigedia Jenerali Yussuf Himid.

Amekuwa akisimamia maridhiano ya Wazanzibari na Umoja wa Kitaifa akiwa mmoja wa wajumbe sita wa Kamati ya Maridhiano aliyoshiriki kikamilifu kuyaanzisha mwaka 2009.

Pia ni miongoni mwa Wazanzibari walio mstari wa mbele kutetea muundo wa Muungano, utakaoipa Zanzibar mamlaka kamili ya dola.

Wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni Mwenyekiti Hassan Nassor Moyo (CCM), Eddie Riyami (CCM), Abubakar Khamis Bakari (CUF), Ismail Jussa Ladhu (CUF) na Salim Bimani (CUF).

No comments:

Post a Comment