Monday 8 June 2015

AKAAA AKUTANA NA MEYA RAIS WA NCHI ?AMA KWELI WAMESHAUZWA WAZANZIBAR

Hapa ndipo Zanzibar tulipofikishwa katika mfumo wa Muungano uliopo. Rais wa Zanzibar anakwenda katika ziara tuliyoambiwa ni ziara rasmi nchini Ujerumani lakini anaishia kukutana na Meya wa Wurzburg.
Zanzibar iliyokubali kuchanganya (na siyo kusalimisha) mamlaka yake kuhusu mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa na Tanganyika ili yasimamiwe kwa pamoja na inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maslahi na manufaa ya nchi zote mbili (Zanzibar na Tanganyika) leo haiwezi kutumia fursa zilizopo kuinua uchumi wake na kubadilisha maisha ya watu wake.
Tanganyika imevaa koti la Muungano na inazitumia kikamilifu fursa zote za mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa na Zanzibar inaishia kutembelea Meya. Ubalozi wa inayoitwa Jamhuri ya Muungano ambao unapaswa kuzihudumia Zanzibar na Tanganyika kwa usawa umeshindwa kusimamia maslahi ya Zanzibar na badala yake unaendeleza mahusiano ya kimataifa kwa maslahi ya Tanganyika tu. Huu si Muungano; ni Ukoloni.
Madalali wa CCM Zanzibar wanasema mfumo huu ndiyo unaoifaa Zanzibar na wakaona fakhari kutuuza Dodoma. Wazanzibari tutafanya maamuzi ya kuwahukumu Madalali hawa Oktoba 25, 2015. Lugha ni moja tu: DELETE, FUTA KABISA

Wednesday 3 June 2015

MAONI YA MSOMAJI KTK FACEBOOK KWA ZIARA YA RAIS SHEIN UGERUMAN !

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 03 Juni 2015 na ZANZINEWS yenye kichwa cha maneno "Dk Shein ziarani Ujerumani", mwandishi ameandika kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameondoka nchini leo kwenda nchini Ujerumani kwa ziara ya kikazi ya siku nane.
Akiwa nchini humo siku ya Alhamisi ijayo, Dk. Shein atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Muziki yanayofanyika katika mji wa Wurzburg pamoja na kuhudhuria utoaji wa zawadi kwa mwaka 2015. Zanzibar inashiriki katika Maonesho hayo yanayofanyika kila mwaka ambayo yanajumuisha wanamuziki na wasanii mashuhuri kutoka nchi za kiafrika pamoja na nchi za mabara mengine ulimwenguni.
Siku inayofuata Dk. Shein atakutana na kufanya mazungumzo na Mstahiki Meya wa Wurzburg na baadae atatembelea Taasisi ya Utibabu ya mji huo(Medical Mission Institute). Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ataendelea na ziara yake nchini humo ambapo siku ya Jumapili tarehe 07 Juni, 2015 atakwenda katika mji wa Frankfurt ambako jioni atakutana na watanzania wanaoishi nchini Ujerumani.
Siku inayofuata atakwenda katika mji wa Postdam ambako atatembelea skuli ya msingi ya Bruno-H-Burgel ambayo ina ushirikiano na skuli ya Mwanakwerekwe Unguja. Siku hiyo hiyo jioni atakutana na mabalozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walioko nchini Ujerumani. Tarehe 09 Juni, 2015 Dk. Shein atakutana na wanachama wa Chama cha Wafanyabiashara wa Ujerumani ambako atatoa hotuba rasmi.
Katika ziara hiyo Dk. Shein amefuatana na mke wake, Mama Mwanamwema Shein; Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Mhe. Said Ali Mbarouk; Waziri wa Kilimo na Maliasili, Dk. Sira Ubwa Mamboya; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Dk. Mahadhi Juma Maalim; na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Wengine ni Mshauri wa Rais (Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa; na Katibu Mkuu wizara ya Biashara,Viwanda na Masoko, Julian Banzi Raphael.
Dk Shein anatarajiwa kurejea nchini tarehe 10 Juni, 2015. Katika uwanja wa ndege wa Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliagwa na viongozi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi.
MAONI: Nimeisoma kwa makini kabisa Ratiba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Mohammed Ali Shein, kuhusu ziara yake uchini Ujerumani. Ikiwa ratiba hii ni sahihi, inasikitisha sana kuona kuwa hapana popote katika ratiba yake panapoonyesha kuwa Rais Shein atakuwa mgeni rasmi wa kiongozi yoyote wa ngazi ya juu wa Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani au hata kiongozi wa moja kati ya Landers (nchi) 16 za Ujerumani zinazofanya Shirikisho la Ujerumani. Kiongozi wa juu kabisa wa kisiasa ambaye Dk. Shein amepangiwa kukutana na kufanya mazungumzo naye ni Mstahiki Meya wa Wurzburg!
Kusema kweli, ikiwa hii ndiyo ratiba aliyopangiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika ziara yake huko Ujerumani, basi mimi kama ningelikuwa mshauri wake wa masuala ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ningelimshauri asifanye ziara hiyo huko Ujerumani. Ningelimshauri hivi kwa sababu iweje Rais mzima wa Zanzibar, tena akiongoza ujumbe uliyosheheni mawaziri na watendaji wa ngazi ya juu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, aridhike kukutana na kufanya mazungumzo na Meya wa Wurzburg na kutembelea taasisi ya utibabu, skuli, kuhudhuria ufunguzi wa maonyesho ya muziki, na kumalizikia kukutana na kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi nchini Ujerumani. Hivi kweli Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania imeshindwa hata kumpangia kukutana na kufanya mazungumzo mafupi na Rais wa Ujerumani, japo kwa maamkizi (courtesy call) tu? Inasikitisha sana.
Kwa hivyo, kama ratiba hii kuhusu ziara ya Rais wa Zanzibar nchini Ujerumani ni sahihi, basi hapana shaka yoyote ile kuwa Zanzibar inahitaji kupata mamlaka kamili.

Monday 30 March 2015


CCM KIEMBESAMAKI
                                       CUF KAEE MAKUNDUCHI

Thursday 12 March 2015

Tuesday 18 February 2014

WATU 13 WAZAMA BAHARINI , WENGINE INAVYO SEMEKAMA WAMEPOTEZA MAISHA !!!

WATU watatu hawajulikani walipo na wengine 10 wamenusurika kufa, kufuatia chombo walichokuwa wakisafiria kupigwa dhoruba na kuzama baharini katika maeneo ya Bumbwini wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja.

Majeruhi hao wakiwemo ndugu wawili wa familia moja na raia wawili wa Kenya, walifikishwa hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa matibabu baada ya kuokolewa na wawili kati yao wanasadikiwa wamekokotwa na maji hadi Bagamoyo.

Akithibitisha tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, SSP Issa Juma Suleiman, alisema, tukio hilo lilitokea majira ya saa 8:30 mchana wa Februari 14 mwaka huu.

Alisema, ajali hiyo ilitokea wakati watu wapatao 13 wakiwa ndani ya jahazi lijulikanalo kwa jina la Mv Hakim kuzama baharini baada ya kupigwa na wimbi lililoambatana na upepo.

Alisema taarifa za kuzama chombo hicho zilipatikana kutoka kwa mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Kheri Juma Nahoda mkaazi wa Amani.

Alisema, mtu huyo aliielezea polisi wanamaji kuhusu kuwepo tukio la kuzama kwa jahazi, ndani yake mkiwa na mabaharia 13 na mizigo ya aina mbali mbali.

Alisema kufuatia ajali hiyo mabaharia wanane waliogelea na baadae kuokolewa katika maeneo mbali mbali.

Alisema baada ya uokozi huo, majeruhi wanane walikimbizwa hospitali kwa matibabu na wawili waliokotwa Bagamoyo huku watatu wakiwa hawajulikani walipo.

Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Idd Hassan Hamadi mkaazi wa Nyerere ambae ndie nahodha wa jahazi hilo, Hamadi Bakari Hassan mkaazi wa Shumba Mjini kisiwani Pemba na Salum Bakari Hamadi wa Mtopepo.

Wengine ni Saburi Juma Hija wa Muange Kaskazini Unguja, Khamis Juma Hija wa Mkwajuni ambao ni ndugu wa familia moja, Juma Haroub Said anaeishi Mkokotoni na raia wawili wa Kenya Bos Horizoba Okash wa Paje na Khamis Mohammed Ali.

Waliokuwa hawajulikani walipo ni Hamadi Juma pamoja na watu wengine wawili waliojulikana kwa majina moja moja la Bakari na Thomas.


Kufuatia tukio hilo, Kaimu Kamanda huyo aliwasihi watumiaji wa bahari kufuatilia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.

POLISI WASHINDWA KUELEZA ALIPO HEMED BAADA YA FUJO MSIKITINI !!!

POLISI Jumatatu walishindwa kutekeleza agizo la Mahakama Kuu la kuwataka wamfikishe mahakamani mwanamume aliyeripotiwa kupotea baada ya kukamatwa wakati wa fujo zilizotokea katika msikiti wa Musa Masjid, mjini Mombasa, wiki mbili zilizopita.
Hemed Salim Ahmed
Hemed Salim Ahmed, 42, akikamatwa na polisi Masjid Musa mjini Mombasa Februari 2, 2014. Picha/KEVIN ODIT 

Badala yake, Mwendesha Mashtaka mkuu wa serikali, Alexander Muteti, alimuomba Jaji Edward Muriithi ampe hadi Alhamisi aweze kurudi mahakamani na maelezo kamili kuhusu aliko Bw Hemed Salim Hemed.

Bw Muteti aliwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma, Keriako Tobiko, Insketa Mkuu wa Polisi David Kimaiyo na Huduma ya Kitaifa ya Polisi, ambao wameshtakiwa kwenye kesi hiyo iliyowasilishwa na Bw Masoud Salim Hemed, nduguye mdogo Bw Hemed.

“Tumekubaliana na wakili wa mlalamishi kwamba kesi itasikilizwa Alhamisi, Februari 20, ili niweze kutoa maagizo fulani kwa polisi kwa ajili ya kutayarisha majibu kamili,” akasema Bw Muteti.

Akaongezea: “Mpelelezi anayechunguza kesi ya msikiti Musa aliniletea stakabadhi kwa niaba ya washtakiwa wa pili na wa tatu na haikuwa na majibu ya maswala yote yaliyo kwenye stakabadhi ya mlalamishi,” akasema.

Hata hivyo, wakili huyo wa serikali aliambia mahakama pasipo kunukuliwa kwamba polisi tayari wamekana kumkamata Bw Hemed kabla ya jaji kumfahamisha kuwepo kwa agizo lake la siku ya Ijumaa lililotolewa baada ya mahakama kukubali kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba Hemed alikamatwa na polisi kwa mujibu wa picha zilizoambatanishwa na stakabadhi za kesi.

“Kama alikamatwa na polisi kama inavyodhihirishwa kwenye stakabadhi ya kesi, basi kuna uwezekano alipotea,” akaeleza Jaji Muriithi.

Maelezo

Bw Muteti akajibu: “Kama huyu bwana yuko katika kituo chochote cha polisi hapa nchini, mheshimiwa Jaji nitafanya hima kuhakikisha ameletwa kortini au kutoa maelezo ya kina kuhusu aliko. Nitafurahi kuwafikisha maafisa wahusika mahakamani kujibu maswali yote.”

Wakili wa mlalamishi, Bw Yusuf Abubakar, aliambia Jaji Muriithi kwamba mteja wake na shirika la Haki Afrika

wamemtafuta Bw Hemed katika vituo vyote vya polisi katika jimbo la Mombasa bila kufanikiwa.

“Polisi hawawezi kusema hawajamkamata ilhali kuna ushahidi wa kuonyesha walimtia nguvuni,” akaeleza BwAbubakar.

Wiki jana, mahakama iliwaachilia huru zaidi ya watu 33 waliokuwa wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo ambapo afisa mmoja wa polisi aliripotiwa kuuawa. Awali, mahakama hiyo hiyo iliagiza watoto wenye umri wa chini ya miaka 12 waliokuwa wamekamatwa waachiliwe huru.

Thursday 13 February 2014

WALEVI WENGINE HAYOOO !!!

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema kupitia gazeti la MTANZANIA la leo kwamba yeye anaamini katika mfumo wa Muungano wa Serikali Moja na kwamba muundo wa Serikali Moja ndiyo suluhisho pekee la kero za Muungano.

VIONGOZI WAJIZANA DR BILAL V/S WARIOBA


Leo kuna kikao kinaendelea katika Hoteli ya White Sands , ambacho KIMEANDALIWA na TCD , ambacho kimepewa jina la "Mkutano wa Tafakuri na Maridhiano kuelekea Katiba Mpya" ambacho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge na Vyama vya Siasa , Viongozi wa Dini, wabunge wapya wa Bunge la Katiba na Tume ya Mabadiliko ya Katiba .

Baadhi ya Viongozi wa Kitaifa waliohudhuria ni pamoja na Dr.Gharib Bilal, Mizengo Pinda, Anne Makinda, Pandu Kificho,Joseph Warioba,Pius Msekwa, Philip Mangula,Freeman Mbowe, Dr.Wilbroad Slaa, Prof.Lipumba, James Mbatia,Stephen Wassira, Asha Rose Migiro,Mathias Chikawe, Askofu Mokiwa, Amir Kundecha,Butiku na wengineo wengi wa aina hiyo.

Joseph Warioba

katika kikao hicho aliyetegemewa kufanya hotuba yaUfunguzi ni Rais Kikwete, ila badala yake alimtuma Bilal kumwakilisha, ndipo katika hotuba yake ya ufunguzi alipoishambulia tume ya Warioba na kuweka msimamo kama ifuatavyo;

1. Kuwa tume haikutumwa kwenda kuandaa rasimu itakayopendekeza uwepo wa serikali tatu , hivyo hayo ni mambo ambayo tume ilijitungia yenyewe , na hivyo Bunge la katiba litaenda kufanya uamuzi kwa misingi ya KURA .....na kila mmoja ajiandae kupokea maamuzi ya kura , hata kama yataenda kinyume na mawazo ya tume ya Warioba .

2. Wao hawakutumwa kwenda kupunguza mambo ya Muungano bali ni kwenda kuyaongeza kama vile suala la Afya, Elimu yalipaswa kuongezwa kwenye rasimu hiyo , ila tume imeenda kuyapunguza , hivyo wanatishia uhai wa Muungano na hivyo ni mawazo ambayo hayapaswi kuungwa mkono na mtu yeyote mwenye akili timamu.
3. Kongamano , limeandaliwa kwa lengo la kupigia debe mawazo ya wakina Warioba ambao ni kikundi kidogo katika jamii na ambao hawawakilishi mawazo ya wengi.

Baada ya maneno hayo na mengine mengi alifungua mkutano , na akitaka kuondoka ila aliombwa anakiri ili aupate majibu kutoka tume na ili asiwe wa kwenda kuambiwa nini kimesemwa , ndipo Warioba alipomuoa kumjibu kwa hoja na vielelezo vya kutosha kuhusu walivyoweza kufikia kwenye HITIMISHO la kuwepo kwa Serikali tatu
MAJIBU YA WARIOBA YALIKUWA KAMA IFUATAVYO !
1. Wao walichofanya ni kukusanya maoni ya wananchi na kuyachambua , na hivyo kutengeneza rasimu kutokana na maoni yao na sio kuwa walijifungia na kuanza kuandika maoni yao binafsi 
2.Wananchi ambao walipendekeza muundo wa Muungano ni kuwa asilimia 4% walisema Muungano usiwepo, 13% walisema uwe wa serikali moja , 22% walisema Muungano wa serikali tatu na 61% walisema kuwa Muungano uwe wa serikali tatu, hivyo kiongozi kusema kuwa tume imejitungia ni kutokujipa muda wa kutazama video na nyaraka mbalimbali walizopewa kama vielelezo vya maoni ya wananchi.

3. Kuwa serikali ya Muungano , imejivika koti la Muungano wakati ikiwa inajishughulisha zaidi na mambo ya Tanganyika , ndio maana Waziri Mkuu hajawahi kwenda Zanzibar kufanya shughuli za kimaendeleo wala kukagua miradi ya maendeleo huo , kwani anajiona yeye ni wa Tanganyika, pia alisema kuwa ukitazama Bunge la Muungano , maswali asilimia 90 yanayoulizwa ni kuhusu mambo ya Tanganyika , kuliko ya Muungano, bajeti ya Muungano asilimia 80 inashughulika na mamb ya Tanganyika kuliko mambo ya Muungano, ndio maana hakuna pesa inatengwa kwa ajili ya maendeleo ya zanzibar , hakuna mtu anajiuliza Zanzibar utapata wapi fedha za kujiendesha nk.

4. Zanzibar ni nchi na katiba yao imepuuza kabisa uwepo wa serikali ya Muungano , ndio maana katiba yao inasema kuwa wao ni nchi na wana Wimbo wa taifa, bendera nk , hivyo kuendelea kujidanganya kuwa Muungano wa serikali mbili upo ni kujivika Tabia za mbuni.......

5. Tume ili pitia ripoti ambazo waliochukua kwenye ofisi ya makamu wa Rais kama vile ripoti ya kamati ya Amina, Shelukindo, Kisanga nk kuhusu Muungano na kote huko kuna malalamiko juu ya Tanganyika kujivika koti la Muungano , nashangaa hata waziri mkuu hapa aliposema Zanzibar sio nchi mnakumbuka yaliyokumkuta huko Bungeni.....

Pius Msekwa, amemuunga mkono Warioba na Kumtaka Wassira ajenge hoja ni kwanini serikali mbili ni muhimu , na sio kuishia kuwa na Mazoea kuwa tumezoea hivi , fear of the unknown....na pia hata hati za Muungano ziliweka wazi kuwa serikali mbili ilikuwa ni kwa interim period only.....sasa je ? Tuendelee kuwa kweye hai hyo baada ya miaka50

Hayo ni ni baadhi ya mambo yalivyo kuwa kwenye kikao na bado kikao kinaendelea 

HUYU NDIYE NYERERE ,ASIYE MJUWA WATANGANYIKA

“MUUNGANO huu unatubana mno…..na Muungano ni kama koti tu, likikubana unalivua”.  Haya ni maneno ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar na mwasisi wa Muungano, hayati Abeid Amani Karume aliyoyatamka mwaka 1968, miaka minne kabla ya kifo chake akionyesha kukerwa na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kauli hii haikumfurahisha Baba wa Taifa la Tanzania [la Tanganyika na Zanzibar?], Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyetaka Muungano ulindwe kwa nguvu zote, tofauti na Karume alipoonekana kuchoshwa na Muungano kutokana na kile alichokiita “kupelekwa puta kwa Muungano unaokiuka makubaliano”.
Tangu mwanzo, Karume alielewa kwamba, alilazimika kuingia Muungano kwa shinikizo na ghiliba. Aliwahi hata kutishia kutohudhuria sherehe za kubadilishana “Hati za Muungano” na kutangazwa rasmi kwa Muungano huo, mjini Dar es Salaam Aprili 26, 1964.  
Na kwa sababu hizo hizo, aliendesha Zanzibar atakavyo, kana kwamba haikuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati Nyerere alizidi kuimeza Zanzibar kwa kuongeza mambo ya Muungano kwa imla, kutoka 11 ya mwanzo hadi 16 wakati wa kifo cha Karume. 
Uhasama kati ya viongozi hawa wawili ulifikia hali ya kutisha kuelekea kipindi cha kifo cha Karume kiasi cha wawili hao kutoongea ana kwa ana kwa zaidi ya mwaka mmoja.  Mawasiliano yao yalikuwa kupitia wapambe wao, Bhoke Munanka kwa upande wa Nyerere, na Aboud Jumbe kwa upande wa Karume.  Kisa? Mfarakano juu ya Muungano!
Kuna wakati Mwalimu Nyerere [mwaka 1968], alikuwa karibu kusalimu amri. Akiandika katika gazeti la “The London Observer” la Aprili 20, 1968, alisema kwa kulalama: “Kama umma wa Wazanzibari, bila ya kurubuniwa kwa hoja za nje, na kwa sababu zao wenyewe, wataona Muungano si wa manufaa kwa uhai wao [na kuamua kujitoa], sitawapiga mabomu kuwalazimisha waendelee na Muungano”. 
Yote haya yalitokana na kutekeleza Muungano wenye muundo tata. Wakati Karume aliamini aliingia Muungano wenye Shirikisho lenye Serikali tatu – Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali Kuu ya Muungano, Nyerere kwa upande wake, alitaka Muungano wenye Serikali mbili – Serikali ya Muungano [ambayo pia ndiyo Tanganyika] na Serikali ya Zanzibar, lengo likiwa kuelekea Serikali moja kwa sababu maalumu kama tutakavyoona baadaye. 
Na hiyo ndiyo sababu ya kuongezwa kwa mambo ya Muungano kinyemela, kinyume na matakwa ya Mkataba wa Muungano wa Aprili 22, 1964.
Siku moja kabla ya Karume kuuawa Aprili 7, 1972, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Salim Rashid, alikwenda kumuaga kwamba alikuwa anajiuzulu kazi serikalini. Karume alimsihi asifanye hivyo na kumhakikishia kwamba [yeye Karume] alikuwa anakusudia kuvunja Muungano siku chache baadaye. Hata hivyo [Karume] hakubahatika kuifikia siku hiyo kuweza kutekeleza alilokusudia, kwa sababu ya kifo.
Wachambuzi wa mambo ya siasa za Muungano wanaamini kwamba, kama Karume angeishi mwaka mmoja zaidi ya 1972, Muungano huu ungevunjika haraka, kwa adha na kwa hali ya kutisha. Lakini pamoja na hayo, kifo chake hakikuzika mzimu wa kero za Muungano tangu hapo hadi leo, mambo yameendelea vile vile.
“Tunang’ang’ana kujadili Muungano kijuujuu bila kugusa Mkataba wa Muungano. Kwa nini hatujadili Mkataba wa Muungano?  Hii ndiyo hati pekee inayohalalisha Muungano na ni msingi na chimbuko kuu la Katiba.  Kwa nini tumefanya kujadili Mkataba wa Muungano kuwa dhambi?
Migogoro, mikanganyiko na mitafaruku yote juu ya Muungano inatokana na kukataa kujadili Mkataba huo ambao ndio “Cheti cha kuzaliwa cha Muungano”. Ni maneno ya Rais wa awamu ya pili Zanzibar, Aboud Jumbe akihoji Kikao Maalum cha Halmashauri Kuu [NEC] ya CCM iliyomwita kumhoji na hatimaye kumvua nyadhifa zote za uongozi kwa kuhoji muundo wa Muungano, Dodoma, Januari 24 – 30, 1964:  Soma Mhtasari wa Kikao hicho, ukurasa 116 – 117].
Jumbe, kama Karume, alikuwa ameanza kubaini jinsi utekelezaji wa Muungano ulivyopelekwa puta bila kuzingatia Mkataba wa Muungano kwa mtizamo wa Muundo wa Serikali mbili kuelekea Serikali moja, na kuzua hofu miongoni mwa Wazanzibari kwamba “nchi” yao ilikuwa inamezwa taratibu na Tanganyika. 
Na hiki ndicho kilichomsukuma Jumbe kutumia haki yake ya kikatiba kutaka kuhoji kwenye Mahakama Maalumu ya Katiba kupata ufafanuzi juu ya Muundo sahihi, ridhaa inayopatikana kwa kila Mtanzania chini ya ibara ya 125, 126 na 128 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977.
“Awali ya yote, niweke wazi kuwa, chini ya Mkataba wa Muungano, uhusiano wa kisiasa uliokusudiwa ni wa Shirikisho. Mkataba wa Muungano haukufuta Tanganyika wala Katiba na Sheria za Tanganyika”, alisema Jumbe kwa kutoa changamoto kwa NEC ya CCM iliyomwita kumhoji.
Akaendelea, “Ule ukweli kwamba Tanganyika ilikabidhi mambo yake kwenye Muungano, haimaanishi kwamba Tanganyika ilikufa. Huu ulikuwa mpango wa muda tu kusubiri Katiba ya Muungano”,
Kwa hili, bila shaka, Jumbe alikuwa ananukuu ibara ya 5 ya Mkataba wa Muungano na kifungu cha 8 (1) cha Sheria ya Muungano, Namba 22 ya 1964, vinavyotamka kuwa; “Kuanzia siku ya Muungano na kuendelea, Sheria za Tanganyika na Sheria za Zanzibar zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo kwa mambo yote yasiyo ya Muungano”,”.
Mwalimu akacharuka, akasema: “Sasa mkanganyiko wa mawazo umezuka.  Makamu [Makamu Mwenyekiti wa CCM - Jumbe] anasema kuna Serikali tatu; mimi nasema mbili. Ni suala la Mkataba wa Muungano. Na kesi imeandaliwa kwenda Mahakamani kwa Serikali ya Mapinduzi kuishitaki Serikali ya Muungano kwenye Mahakama [maalumu] ya Katiba. Ukuu wa Chama.  Kwa kosa gani Serikali ya Zanzibar iishitaki Serikali ya Muungano?..... Makamu, jiuzulu sasa hivi”, Mwalimu akamwagiza Jumbe kikaoni. 
Jumbe akajiuzulu [kwa shuruti?] nyadhifa zote za Chama na Serikali kwa dhambi ya kuhoji Muundo wa Muungano. Na kuanzia hapo akawekwa chini ya Ulinzi nyumbani kwake “Mji mwema” kwa miezi mingi.
Mwalimu alikuwa muumini wa Serikali tatu.
Kama tutakavyoona baadaye, tangu mwanzo, Mwalimu hakuwa muumini wa Serikali mbili, bali wa Shirikisho.  Kwake Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulivyo, ulikuja kama ajali tu. 
Ulitokana na shinikizo la nchi za Magharibi enzi za vita baridi, zikimtumia Nyerere “aimeze” Zanzibar ndani ya tumbo kubwa la Tanganyika baada ya Shirikisho la Afrika Mashariki kushindwa ili isiangukie mikononi mwa Wakomunisti kufuatia Mapinduzi ya Kikomunisti Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Mwanzoni, Nyerere alikuwa mpinzani mkubwa wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, pale wazo hilo lilipowasilishwa kwake na Balozi wa Marekani, Februari 1964; na tena Machi 7, 1964 na Naibu Waziri wa Nchi wa Marekani [Mambo ya Afrika], Jimmy Trimble.  Lakini taratibu, alianza kuona hatari mbele yake kwa Zanzibar ya Kikomunisti [hakupenda Ukomunisti mwanzoni] kuwa mlangoni mwa Tanganyika, huku nchi za Magharibi nazo zikimshinikiza achukue hatua juu ya jambo hilo.
Alianza kutambua udhaifu wa Serikali yake na wa nchi zingine za Kiafrika dhidi ya hatari kutoka nje. Si hivyo tu, tangu mwaka 1960 kabla ya uhuru, alihofia Zanzibar kuwa karibu na Tanganyika akatamka wazi wazi akisema: “Kama ningekuwa na uwezo wa kukisukuma kisiwa kile [Zanzibar] hadi katikati ya bahari ya Hindi, ningefanya hivyo. Sitanii. Nina  hofu [kwamba], huko mbele kitakuja kutuumiza kichwa”.
Juhudi zote za Nyerere kuona Shirikisho la Afrika Mashariki [EAF] likiundwa, zilikuwa ni kuhakikisha Zanzibar inamezwa ndani ya Shirikisho, na pale Shirikisho hilo liliposhindwa, akaona njia pekee ya kuondokana na hofu yake [na sasa kwa kupewa nguvu pia na Marekani na Uingereza ambazo nazo zilikuwa na hofu ya Ukomunisti kuenea Afrika Mashariki kupitia Zanzibar] ni kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika. 
Kuhusu Muundo wa Serikali mbili alioendeleza, tofauti na Serikali tatu za Mkataba wa Muungano, unalenga Serikali moja kwa kuongeza taratibu [kinyemela] mambo ya Muungano ili hatimaye Zanzibar ijikute imenyang’anywa mambo yote kuwa chini ya Serikali ya Muungano ambayo ndiyo Tanganyika pia. Ugomvi wa Karume na baadaye Jumbe juu ya Muungano umejikita hapo. Na hivi karibuni, Rais wa Zanzibar, Dakta Mohamed Shein, amewakemea wote wanaodhani Zanzibar siyo nchi yenye mamlaka kamili waache uzandiki huo.
Nyerere alisalimu amri kwa shinikizo
Vitisho na shinikizo la Marekani na Uingereza vilimfanya Mwalimu akubali Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kukidhi matakwa ya Mataifa hayo. Vitisho vipi?. Kwanza, alikuwa bado na kumbukumbu yenye hofu jinsi alivyonusurika kupinduliwa na Jeshi lake mwenyewe, Januari 20, 1964; na jinsi alivyookolewa na Jeshi la Waingereza ambao ndio pia walioshinikiza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Na hata kama angekataa kuungana, Uingereza na Marekani, chini ya mpango wa kivita ulioitwa “Zanzibar Action Plan” [ZAP], zilikuwa tayari kuivamia Zanzibar kijeshi, kama Karume angekataa Muungano.
Uhakika ni kwamba, majeshi ya Uingereza, chini ya Kamanda wa Jeshi la Anga – “Royal Air Force” [RAF], Brigedia Jenerali I. S. Stockwell, na Kamanda wa Jeshi la Ardhini nchini Kenya, Brigedia Jenerali I. H. Freeland, yalipewa Amri [Joint Operation Instruction] Namba 2/64 kuvamia, huku yakitarajia upinzani na kipigo kutoka Jeshi la Zanzibar [Zanzibar Liberation Army – ZLA] chini ya Uongozi makini wa Kanali Ali Mahfoudh, na pengine kwa msaada kadhaa wa silaha kali kutoka China na Urusi.
Pili, Mwalimu bado alikuwa akikumbuka kwa hofu, kuuawa kwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Kongo, Mwanamapinduzi Patrice Emery Lumumba, na Rais Sylivanus Olympio wa Togo, waliouawa kikatili chini ya kile kilichoitwa “mchezo mchafu wa nchi za Magharibi dhidi ya Viongozi wanamapinduzi barani Afrika”. 
Kwa hili, Nyerere aliona lazima achukue hatua haraka badala ya kusukumwa na kujiweka rehani kwa ugomvi wa mataifa makubwa ya Magharibi na Mashariki. Na hii ilikuwa Baraka pia kwake kumaliza “hofu” yake juu ya Zanzibar huru.
Muungano huo, ambao ulibuniwa baada ya kuvunjika kwa mpango wa EAF mjini Nairobi, Aprili 10, 1964, ulikuwa njia pekee ya kumzuia aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Mambo ya Nje wa Zanzibar wa wakati huo na Mkomunisti, Abdulrahman Mohamed Babu na mawakala wenzake wa Wachina [Chicoms] na Warusi, asidhibiti na kuhodhi madaraka ya Serikali ya Mapinduzi Visiwani.
Kuna dhana isiyo kweli kwamba Machi 1964, Mwalimu na Karume walikutana Ikulu Dar es Salaam ambapo Mwalimu alipendekeza kwa Karume juu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na eti kwamba Karume alikubali mara moja akisema: “Ita waandishi wa magazeti; waambie kwamba sisi tuko tayari sasa hivi”.
Dhana hii imepotoshwa.  Maneno ya Mwalimu yalikuwa hivi:  “Tazama, nimewaeleza wazi wazi Waziri Mkuu [Jomo] Kenyatta na Waziri Mkuu [Milton] Obote kwamba, wao wakiwa tayari kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki, sisi [Tanganyika] tuko tayari.  Na sasa nakwambia na wewe [Karume, kama nilivyowaambia Kenyatta na Obote], kwamba Zanzibar mtakapokuwa tayari kuunda Shirikisho [hilo], sisi [Tanganyika] tuko tayari”.
Ukweli ni kwamba, alichomwambia Karume ni juu ya uundaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki na si Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.  Ingekuwaje hivyo wakati muda huo Nyerere alikuwa akifukuzia Shirikisho la Afrika Mashariki kuliko kitu kingine chochote, hadi juhudi hizo ziliposhindwa Aprili 10, 1964 na kugeukia Zanzibar?
Nani anasema Mwalimu alitaka Serikali mbili?
Tumesema, Mwalimu tangu kale hakuwa muumini wa Muungano wenye Serikali mbili ila kwa Tanganyika na Zanzibar kwa lengo maalumu.  Kwenye Mkutano wa nchi huru za Afrika mjini Cairo, Julai 1964, alionyesha wazi wazi kutopendelea Muundo huo aliposema, “Muundo wa Serikali moja [Unitary System of government] haufai kwa Afrika kwa sasa; Muundo bora ni ule wa Shirikisho la Nchi”.
Akitetea hoja hiyo baadaye, aliandika makala ndefu kwenye Gazeti la “Africa Forum” [Vol.1 No. 1] mwaka 1965 akisema: “Mfumo bora ni ule wa Shirikisho lenye Serikali Kuu ya Muungano na Serikali za nchi zinazoungana, kila moja ikiwa na Mamlaka juu ya Mambo yasiyo ya Muungano”. Msimamo wake huo ameurudia pia katika Kitabu chake: “Uhuru na Umoja” [Freedom and Unity] ukurasa 300 – 304.
Na hivyo ndivyo alivyoamini Mzee Karume. Akitoa taarifa kwa Serikali yake kwa simu ya maandishi [telegraph], aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini Zanzibar kabla na baadaye kidogo kufuatia Muungano, jasusi la CIA, Frank Carlucci, Aprili 23, 1964 alisema, “Karume ametia sahihi [Aprili 22, 1964] Hati [Mkataba] ya Muungano akiamini kwamba ameingia Mkataba wa kuunda Shirikisho lenye Serikali tatu”.
Na siku za karibuni kabla ya kifo chake, baada ya kuchoshwa na kero za Muungano zisizoisha, Mwalimu alitambua utata wa Muundo wa Serikali mbili alisema muundo huo yafaa ujadiliwe kuondoa utata hata kama yeye alikwishatoa msimamo wake wa Serikali mbili. 
Ukweli Mwalimu alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa, kama isingekuwa kwa “mambo fulani fulani” juu yake, asingemvua Jumbe madaraka kwa kuhoji Muundo wa Muungano.
Je, hawa wanaojifaragua, hivi sasa, kwamba kujadili Muundo wa Muungano nje ya Serikali mbili ni kumsaliti Mwalimu, wanatoa wapi ujasiri huo kuuhadaa umma? Kama ni kumsaliti Mwalimu, tusemeje juu ya hao hao waliohujumu Azimio la Arusha na Ujamaa; waliobinafsisha mali za umma bila kujali ili kuwapa ulaji mawakala wa ubepari? Je, si wasaliti, hao hao wanaokigeuza Chama cha Mwalimu [CCM] kichaka na kimbilio la mafisadi wasiotaka kujivua gamba?.
Sio siri tena kwamba Wazanzibari wengi hawapendelei Muungano wa Serikali mbili au moja, mbali na wanaotaka uvunjwe.  Lakini Wahafidhina wa siasa za makundi, kwa unafiki mkubwa, wanajifanya kutoliona hili.
Ni hao hao waliopinga mchakato wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Visiwani, wakiwamo Wajumbe wa NEC ya CCM, mpaka Rais wa wakati huo, Amani Abeid Karume akatishia kuwaumbua.
Uhafidhina huo na unafiki wao wa kutaka kuona migogoro na kero za Muungano zikiendelea ndio unaofanya waishi kwa gharama ya amani na umoja wa Kitaifa wa nchi yetu.
Sasa, ifike mahali waambiwe wazi wazi, waache demokrasia na mawazo ya wananchi juu ya Muundo wa Muungano wautakao yatawale badala ya ubinafsi wao. Na tunaposhinikiza mambo dhidi ya matakwa ya wengi tunatafuta nini, na nini hatima ya yote haya?