Tuesday 18 February 2014

POLISI WASHINDWA KUELEZA ALIPO HEMED BAADA YA FUJO MSIKITINI !!!

POLISI Jumatatu walishindwa kutekeleza agizo la Mahakama Kuu la kuwataka wamfikishe mahakamani mwanamume aliyeripotiwa kupotea baada ya kukamatwa wakati wa fujo zilizotokea katika msikiti wa Musa Masjid, mjini Mombasa, wiki mbili zilizopita.
Hemed Salim Ahmed
Hemed Salim Ahmed, 42, akikamatwa na polisi Masjid Musa mjini Mombasa Februari 2, 2014. Picha/KEVIN ODIT 

Badala yake, Mwendesha Mashtaka mkuu wa serikali, Alexander Muteti, alimuomba Jaji Edward Muriithi ampe hadi Alhamisi aweze kurudi mahakamani na maelezo kamili kuhusu aliko Bw Hemed Salim Hemed.

Bw Muteti aliwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma, Keriako Tobiko, Insketa Mkuu wa Polisi David Kimaiyo na Huduma ya Kitaifa ya Polisi, ambao wameshtakiwa kwenye kesi hiyo iliyowasilishwa na Bw Masoud Salim Hemed, nduguye mdogo Bw Hemed.

“Tumekubaliana na wakili wa mlalamishi kwamba kesi itasikilizwa Alhamisi, Februari 20, ili niweze kutoa maagizo fulani kwa polisi kwa ajili ya kutayarisha majibu kamili,” akasema Bw Muteti.

Akaongezea: “Mpelelezi anayechunguza kesi ya msikiti Musa aliniletea stakabadhi kwa niaba ya washtakiwa wa pili na wa tatu na haikuwa na majibu ya maswala yote yaliyo kwenye stakabadhi ya mlalamishi,” akasema.

Hata hivyo, wakili huyo wa serikali aliambia mahakama pasipo kunukuliwa kwamba polisi tayari wamekana kumkamata Bw Hemed kabla ya jaji kumfahamisha kuwepo kwa agizo lake la siku ya Ijumaa lililotolewa baada ya mahakama kukubali kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba Hemed alikamatwa na polisi kwa mujibu wa picha zilizoambatanishwa na stakabadhi za kesi.

“Kama alikamatwa na polisi kama inavyodhihirishwa kwenye stakabadhi ya kesi, basi kuna uwezekano alipotea,” akaeleza Jaji Muriithi.

Maelezo

Bw Muteti akajibu: “Kama huyu bwana yuko katika kituo chochote cha polisi hapa nchini, mheshimiwa Jaji nitafanya hima kuhakikisha ameletwa kortini au kutoa maelezo ya kina kuhusu aliko. Nitafurahi kuwafikisha maafisa wahusika mahakamani kujibu maswali yote.”

Wakili wa mlalamishi, Bw Yusuf Abubakar, aliambia Jaji Muriithi kwamba mteja wake na shirika la Haki Afrika

wamemtafuta Bw Hemed katika vituo vyote vya polisi katika jimbo la Mombasa bila kufanikiwa.

“Polisi hawawezi kusema hawajamkamata ilhali kuna ushahidi wa kuonyesha walimtia nguvuni,” akaeleza BwAbubakar.

Wiki jana, mahakama iliwaachilia huru zaidi ya watu 33 waliokuwa wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo ambapo afisa mmoja wa polisi aliripotiwa kuuawa. Awali, mahakama hiyo hiyo iliagiza watoto wenye umri wa chini ya miaka 12 waliokuwa wamekamatwa waachiliwe huru.

No comments:

Post a Comment