Tuesday 18 February 2014

WATU 13 WAZAMA BAHARINI , WENGINE INAVYO SEMEKAMA WAMEPOTEZA MAISHA !!!

WATU watatu hawajulikani walipo na wengine 10 wamenusurika kufa, kufuatia chombo walichokuwa wakisafiria kupigwa dhoruba na kuzama baharini katika maeneo ya Bumbwini wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja.

Majeruhi hao wakiwemo ndugu wawili wa familia moja na raia wawili wa Kenya, walifikishwa hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa matibabu baada ya kuokolewa na wawili kati yao wanasadikiwa wamekokotwa na maji hadi Bagamoyo.

Akithibitisha tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, SSP Issa Juma Suleiman, alisema, tukio hilo lilitokea majira ya saa 8:30 mchana wa Februari 14 mwaka huu.

Alisema, ajali hiyo ilitokea wakati watu wapatao 13 wakiwa ndani ya jahazi lijulikanalo kwa jina la Mv Hakim kuzama baharini baada ya kupigwa na wimbi lililoambatana na upepo.

Alisema taarifa za kuzama chombo hicho zilipatikana kutoka kwa mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Kheri Juma Nahoda mkaazi wa Amani.

Alisema, mtu huyo aliielezea polisi wanamaji kuhusu kuwepo tukio la kuzama kwa jahazi, ndani yake mkiwa na mabaharia 13 na mizigo ya aina mbali mbali.

Alisema kufuatia ajali hiyo mabaharia wanane waliogelea na baadae kuokolewa katika maeneo mbali mbali.

Alisema baada ya uokozi huo, majeruhi wanane walikimbizwa hospitali kwa matibabu na wawili waliokotwa Bagamoyo huku watatu wakiwa hawajulikani walipo.

Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Idd Hassan Hamadi mkaazi wa Nyerere ambae ndie nahodha wa jahazi hilo, Hamadi Bakari Hassan mkaazi wa Shumba Mjini kisiwani Pemba na Salum Bakari Hamadi wa Mtopepo.

Wengine ni Saburi Juma Hija wa Muange Kaskazini Unguja, Khamis Juma Hija wa Mkwajuni ambao ni ndugu wa familia moja, Juma Haroub Said anaeishi Mkokotoni na raia wawili wa Kenya Bos Horizoba Okash wa Paje na Khamis Mohammed Ali.

Waliokuwa hawajulikani walipo ni Hamadi Juma pamoja na watu wengine wawili waliojulikana kwa majina moja moja la Bakari na Thomas.


Kufuatia tukio hilo, Kaimu Kamanda huyo aliwasihi watumiaji wa bahari kufuatilia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.

No comments:

Post a Comment