Wednesday 28 August 2013

CCM ZANZIBAR WAZUSHI FITNA !!!

Na Ismail Jussa. MANSOOR Yussuf Himid. Jina hili sasa huwezi kulitenganisha na matakwa halali ya Wazanzibari walio wengi wanaotaka Zanzibar irejeshe hadhi yake kama nchi yenye MAMLAKA KAMILI kitaifa na kimataifa. Kitendo cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumfutia uanachama wake jana ni kitendo cha kujiangamiza chenyewe katika siasa za sasa za Zanzibar ambazo zimetawaliwa na hoja moja kuu ambayo ni Mamlaka Kamili.
Tangu hapo vijana wengi wa CCM/Zanzibar wa kizazi kipya walishaonesha mwelekeo wa kupoteza imani na chama chao kutokana na ukakasi wa viongozi wake muflisi kushindwa kusimamia matakwa na maslahi ya Wazanzibari na badala yake kuonekana kama ni mawakala wa ukoloni wa Tanganyika dhidi ya Zanzibar.
Rais Ali Mohamed Shein, Balozi Seif Ali Iddi, Vuai Ali Vuai na Sekretarieti ya akina Haji Mkema, Hamad Masauni na Waride Bakari Jabu hawaonekani kuwakilisha hisia za Wazanzibari.
Kielelezo thabiti cha hali hiyo kilionekana pale mamia ya vijana wa CCM walipoonekana kupanga misururu mirefu huko Matemwe na Kitope kurejesha kadi za kijani kwa kiongozi waliyempa matumaini yao Maalim Seif Sharif Hamad.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula. Yeye anataka Muungano wa Serikali Moja. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula. Yeye anataka Muungano wa Serikali Moja. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Hali kama hiyo ikajitokeza kwa wazee wa CCM wa maeneo yenye ngome zao Pemba kama Kangagani ambao nao walirudisha kadi huku wakiomba msamaha kwa kuchelewa kufahamu kuwa kumbe CCM hakipo kwa maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari.
Katika hali kama hiyo ungetegemea chama makini na kinachojikosoa kingejirudi na kujitazama upya. Lakini wapi? Wahenga walisema: La kuvunda halina ubani.
Ni juzi tu nilipokuwa nikihutubia mkutano wa hadhara hapo katika viwanja vya Komba Wapya niliwaambia wanachama wa CCM na hususan vijana kwamba mpaka lini wataendelea  kukubali Dodoma kuwa machinjio ya kisiasa ya viongozi wa Zanzibar?
Alianza Aboud Jumbe mwaka 1984, akafuata Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake sita mwaka 1988, akaja Dk. Salmin Amour alipojiunga na OIC mwaka 1993 na sasa tena mwaka 2013 anadhalilishwa Mansoor Yussuf Himid kwa sababu tu amethubutu kukhitilafiana na watawala wa Dodoma kwa kusimamia kidete hoja ya Mamlaka Kamili.
Nikasema umefika wakati wana-CCM wa Zanzibar na hasa vijana kujiuliza hichi kweli ni chama chao na kipo kwa maslahi yao? Hichi kweli ndicho mzawa na mrithi wa kisiasa wa Afro-Shirazi Party (ASP)?
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai (Mbunge wa CCM). Naye anataka Serikali Tatu. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai (Mbunge wa CCM). Naye anataka Serikali Tatu. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wa kumfuta uanachama Mansoor ni ujumbe tosha kwamba yeyote atakayesimamia maslahi ya Zanzibar hana nafasi kwenye chama hicho. Kwa lugha nyingine, Zanzibar na CCM ni Lila na Fila, hazitangamani.
Na tazama hata majibu ya Katibu Mwenezi wa CCM wa upande wa Tanganyika, Nape Nnauye, alipoulizwa autaje usaliti wa Mansoor anaodaiwa kuufanya dhidi ya Chama. Alisema ni pale Mansoor aliposimama ndani ya Baraza la Wawakilishi mwaka 2009 na kusema Serikali ya Muungano ni wizi wa mchana kweupe wa rasilimali za Zanzibar. Swali la kumuuliza Nape ni kwamba je, madai hayo ni uongo?
Lakini hebu tuje kwenye hilo la kutetea msimamo wa muundo wa Muungano wa Mkataba unaokwenda kinyume na sera ya CCM ya Serikali Mbili. Kama hilo ni kosa mbona aliyeadhibiwa ni Mansoor peke yake?
Wajumbe vigogo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ndiyo iliyokuja na pendekezo la muundo wa Shirikisho la Serikali Tatu, wakiwemo Jaji Joseph Warioba, Salim Ahmed Salim na Joseph Butiku, ni wanachama wa CCM mbona hawakufukuzwa?
Beatrice Shelukindo, Mbunge wa CCM. Serikali Tatu. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Beatrice Shelukindo, Mbunge wa CCM. Serikali Tatu. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Mwaka 1994 Kundi la Wabunge 55 maarufu kama G-55 walipeleka hoja Bungeni na hoja ikapitishwa na Bunge zima ya kuanzisha Serikali ya Tanganyika kinyume na sera ya CCM. Mbona hawakufukuzwa?
Katika huu mjadala unaoendelea wamejitokeza wabunge kama Esther Bulaya na Beatrice Shelukindo na hivi karibuni Naibu Spika Job Ndugai kutetea mfumo wa Shirikisho la Serikali Tatu. Mbona hawakufukuzwa?
Achilia mbali hao, hata Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula alisema yeye msimamo wake ni kutaka mfumo wa Serikali Moja tu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jambo ambalo ni kinyume na sera ya Chama chao mbona hakufukuzwa?
Kwa nini Mansoor Yussuf Himid peke yake? Kwa mtazamo wangu mimi Mansoor ameadhibiwa kwa sababu ya msimamo wake aliouchukua katika kuleta amani kupitia Maridhiano ya Wazanzibari ambayo wahafidhina wa CCM/Zanzibar na wale wenye kujali matumbo yao tu hawakuyataka na mpaka leo hawajayaridhia na wakipata nafasi wanayamezea mate wayavuruge.
Wanaona Maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyopatikana kupitia Maridhiano hayo yamewatiribulia nafasi za kuwa Mawaziri au Manaibu Waziri na pia kufanya watakavyo kujinufaisha wao na aila zao huku watoto wa wanyonge, wakwezi na wakulima wakiendelea kusaga meno.
Esther Lubaya, Mbunge wa CCM. Anataka Serikali Tatu. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Esther Lubaya, Mbunge wa CCM. Anataka Serikali Tatu. Hajaitwa. Hajafukuzwa.
Na la pili ndilo hili la kusimama bila ya kuyumba kwenye hoja ya MAMLAKA KAMILI kwa Zanzibar, msimamo ambao unakwenda kinyume na misingi ya CCM iliyoachwa na mwasisi wake Julius Nyerere.
Ala kulli hali, hukumu imeshapitishwa na Mansoor Yussuf Himid siyo tena mwanachama wa CCM.
Kwa jinsi nimjuavyo Mansoor hakuyumbishwa na uamuzi huu na kwa hakika akiutarajia. Natambua jinsi alivyo jasiri, shupavu, mkweli na mzalendo na hivyo najua hatotetereka katika kuendeleza msimamo wake na kuendeleza harakati za Mamlaka Kamili kwa Zanzibar.
Nilikuwa namheshimu sana na kwa kule kuonesha kwake mfano katika kusimamia anachokiamini. Sasa namheshimu zaidi.
Sina shaka kwamba huu si mwisho wa Mansoor kisiasa bali naamini kwa dhati kuwa hatua ya leo ndiyo mwanzo wa kupaa kisiasa Mansoor Yussuf Himid. Nilicho na uhakika nacho ni kwamba huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM katika medani za siasa za Zanzibar. Kwa sababu ya chuki, choyo na visasi wamechukua maamuzi ya hasira ya kujipiga wenyewe risasi mguuni.
Mwaka 1988, CCM iliwatengenezea Wazanzibari shujaa Maalim Seif Sharif Hamad. Tuna furaha kuwa sasa 2013 imetutengenezea shujaa mwingine wa Zanzibar, Mansoor Yussuf Himid. Wazanzibari tumempokea kwa mikono miwili. Wakiungana mashujaa wawili hawa hakuna wa kuzuia wimbi kubwa la mabadiliko linalokuja. A’luta Continua!
Ismail Jussa ni mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe. Naye, kama alivyo Mansoor Yussuf Himid, ni mjumbe wa Kamati ya Maridhiano inayoongozwa na mwanaCCM Hassan Nassor Moyo.

No comments:

Post a Comment