Wednesday 28 August 2013

CHINJIO DODOMA KWA WAZANZIBAR LINAMAKALI.KWA WATANGANYIKA BUTU !!!

CCM inaenda kinyume na Mapinduzi ya Zanzibar

Waasisi wa Mapinduzi ambao leo watoto wao wanafukuzwa

Na Salim Salim

MACHINJIO ya Wazanzibari yameendelea kuwachinja Wazanzibari, mara hii wamemchinja Mtoto wa MwanaMapinduzi, Mansour Yussuf Himid,Mzanzibari Kindakindaki, Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki ambako mimi ni mkaazi. 

Sababu kuu ya kumchinja Mansour ni ile kauli yake ya kuunga mkono Muungano wa Mkataba ambao utarudisha Mamlaka Kamili Zanzibar katika mfumo wa Muungano.

Sisi wananchi wa Jimbo la Kiembesamaki tumefadhaika, tumeduwaa, tumeachwa mdomo wazi, huku tukisubiri kauli ya Mwakilishi wetu ili tuifanyie kazi.

Sio sisi wananchi wa Kiembesamaki peke yetu tulioduwaa na kufadhaishwa na wanaoisubiri kauli ya Mansoor ili waifanyie kazi, ni wananchi wote Wazanzibari, Unguja na Pemba, mashamba na Mjini.

Watu wamekata tamaa na CCM na wengi wana CCM wametamka hadharani watarudisha kadi CCM. 

Wazanzibari wamechoshwa na Machinjio ya Dodoma, leo ni Mansour, kesho Mwana CCM Zanzibari mwengine.

Swali lipo hapa, kwa nini ni Wazanzibari peke yetu tunaochinjwa Dodoma? Hatujapata kusikia chinjio hili likimchinja Mtanganyika.

Huenda labda kwa Watanganyika chinjio hiloni butu.

Tumeyashuhudia ya Aboud Jumbe, ya MaalimSeif na wenzake, ya Salmin Amour kutakiwa aitoe Zanzibar kutoka Jumuiya ya Organization of Islamic Conference na leo kufukuzwa Mansoor Yussuf Himid.

Tayari pia kuna wito wa kudai Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, afukuzwe Serikalini kwa kuunga mkono Rasimu ya Katiba yenye mfumo wa Muungano wa Serikali Tatu.

Maneno yanafika mbali zaidi kuwa hata Maalim Seif, Makamu wa Kwanza wa Rais, ambaye ameekwa Serikalini na Katiba ya Zanzibar pia afukuzwe kazi.

Kikubwa zaidi wenye kuchongea mambo yote hayo wanatamani Umoja wa Kitaifa Zanzibar uvunjike ili turudi nyuma tulipotokaambapo kila mwananchi wa Zanzibar hataki turudi huko.

Na kuibadili Katiba ya Zanzibar hawawezi. Kwanza hawana thuluthi mbili ndani ya Baraza la Wawakilishi lakini pia ni lazima waitishe Kura ya Maoni kuiondoa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hakuna mwananchi hata mmoja wa Zanzibar atakaye sema “Ndio Serikali ya Umoja wa Kitaifa iondoke”, isipokuwa labda wao, nao ni wachache.

Lakini yote haya yanatokea wakati Bunge Maalum la Katiba linakaribia kuundwa. Ni dhahiri kwamba lengo ni kuwatisha Wawakilishi na Wabunge watakaoteuliwa katika Bunge hilo wasende kusimamia hoja ya Mamlaka Kamili Zanzibar. 

Wahafidhina wa CCM/Zanzibar wanajidanganya; hakuna atakayetishika kuhusu hili.

Kufanya hivi wanadhani watawanyamazisha Wazanzibari; kufanya hivi wanadhani watairudisha haki nyuma; haki haijawahi kurudi nyuma. Siku zote haki huenda mbele hata ukiichelewesha kwa miaka mia.

Wazanzibari tulifanya Mapinduzi ili tuwe Huru. Wazanzibari hatukufanya Mapinduzi ili tuungane na Tanganyika. Tulifanya Mapinduzi ili tujitawale na lengo kuu ili tuweHuru, kukataa Zanzibar yenye Mamlaka Kamili ni kuyapinga Mapinduzi ya Zanzibar.

Mansoor na wenzake wanayalinda Mapinduzi ya Zanzibar kwani wanaujua msingi, malengo na sababu ya kufanyika kwake.
Suala la kutoa maoni ni haki ya kila mmoja wetu. Ni haki yetu ya kimaumbile na ni haki ya Kikatiba.

Wakati mchakato wa Katiba mpya ulipoanza viongozi wetu walituhimiza tusema chochote tunachokitaka. Rais Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo sehemu tafauti. Mara mbili alitwambia hayo uwanja wa Aman na wakati wa kuizindua Tume ya Katiba, Rais Jakaya Kikwete naye kayasema hayo mara kadhaa na hata alipokuwa analifungua Baraza la Katiba la CCM alisema wastahamiliwe wenye maoni tofauti na Chama. 

Nashangaa leo kumwona mwenye maoni tofauti na wao wamemfukuza CCM.

Rais Kikwete wakati anaizindua Tume ya Katiba alisema hata watakaotoa maoni ya kipuuzi wasikilizwe. Hiyo ndiyo CCM.

Uzuri wa mambo Mansoor amefukuzwa Chama, hajapokonywa Uzanzibari wake.

Kufukuzwa kwa Mansoor ni ushindi kwa wanaopigania Zanzibar irejeshewe Mamlaka Kamili na wananchi wote wa Zanzibar kwa ujumla. Huyu ni Shujaa wa Zanzibar, na mtetezi wa haki ya Zanzibar.

Hongera Mwana Mapinduzi, Hongera Shujaa wetu Mansoor Yussuf Himid. Mamlaka Kamili yatasimama japokuwa wapinzani wanachukia.

No comments:

Post a Comment