Wednesday 1 May 2013

ZANZIBAR HAWATOPATA CHENJI YA RADA !!!

SAKATA la chenji ya fedha za rada jana lilizua balaa bungeni, baada ya wabunge wa Zanzibar kutaka fedha hizo pia zigawiwe katika visiwa hivyo. Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, alisema kuwa Bunge linashiriki kuvunja katiba kutokana na majibu ya Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene, aliyesema kwamba fedha hizo hazitakwenda Zanzibar.

Akiomba mwongozo mara baada ya kipindi cha maswali na majibu, Hamad alisema kwa mujibu wa katiba, suala la kodi ya mapato na masuala ya usafiri wa anga ni ya muungano, iweje fedha za rada zisipelekwe Zanzibar.

“Mheshimiwa Spika, Bunge hili linasimamia katiba na sheria, huoni kwamba Wazanzibari nao wana haki ya kupatiwa fedha hizi ili kuboresha shule wanazosoma watoto wa Kitanzania?” alihoji Hamad.

Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliagiza suala hilo likajadiliwe katika Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Nungwi, Yusuph Haji Khamis, Mbene alisema fedha za rada zilizorejeshwa Sh bilioni 72.3 ziliingizwa katika bajeti ya serikali kwa mwaka 2012/13.

“Aidha, bajeti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulipia masuala ya muungano na elimu ya msingi Zanzibar si suala la muungano,” alisema.

Mbene alikiri kwamba fedha hizo za marejesho ni za Serikali ya Muungano ambazo zilitokana na udanganyifu uliofanywa na Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza wakati wa kuiuzia Serikali ya Tanzania rada ya kuongozea vyombo vya usafiri angani.

Alisema kutokana na makubaliano yaliyofikiwa na kampuni hiyo, fedha hizo zitapelekwa sekta ya elimu kugharamia mahitaji muhimu.

Akiongezea majibu hayo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI-Elimu), Kassim Majaliwa, alisema fedha za rada ni kwa ajili ya kuboresha elimu ya msingi ambayo si suala la muungano.

Alisema Sh bilioni 55.2 zitanunua vitabu na Sh bilioni 18.9 zitanunua madawati katika halmashauri zote.

“Zabuni za kusambaza vitabu zilishatangazwa, kampuni tisa zimepatikana na wakati wowote vitabu vitaanza kusambazwa,” alisema Majaliwa.

Katika swali lake, Khamis alitaka kujua kiasi ambacho sekta ya elimu ya msingi imetengwa kutoka katika fedha za rada.

No comments:

Post a Comment