Wednesday 8 May 2013

ZANZIBAR KWANZA ILIONGOZWA KAMA DOLA HURU YENYE MAMLAKA KAMILI !!!


Jana nilipitia baadhi na makala za Muandishi wangu kipenzi Ali Nabwa (Allah Amrehemu), makala ambayo Ali Nabwa alikuwa ameandika mahojiano baina yake na Ndugu Salim Said Rashid (Katibu wa kwanza wa Baraza La Mapinduzi), ningependa kuleta kwenu baadhi ya maswali matatu waliohojiana.

Swali: Inasemekana kulikuwa na Wizara za Muungano hapa Zanzibar, ilikuaje zikaondoshwa ?

Jawabu: Baada Muungano walikuja mawaziri kufunguwa ofisi za Muungano hapa, lakini Serikali ya Mpinduzi ikakataa. Na napenda kukufahamisha kwamba, namna muungano ulivyoendeshwa katika awamu mbali mbali za Zanzibar inahitilafiana. Awamu ya Kwanza Zanzibar ilikuwa inaendeshwa kama taifa huru.

Swali: Kwa vipi ?

Jawabu: Kwa kuwa ilikuwa na jeshi lake, ilikuwa na idara zake, hakukuwa hapa na wafanya kazi wa Muungano, ilikuwa na chama chake, ilikuwa na kila kitu chake, na mamlaka yake ya kimataifa. Mambo yaliyokuwa yanafanya kazi yalikuwa mambo ya Muungano tu. Hata hayo ilikuwa matatizo. Kwa mfano, sarafu ya fedha za kigeni ya Zanzibar, ambayo ilikuwa nyingi, haikuchanganyishwa na ile ya Tanganyika na ilikuwa chini ya mamlaka ya Zanzibar, haikuwa chini ya mamlaka ya Muungano.

Swali: Unadhani ungefika wakati, hasa kwa mambo yalivyojitokeza baadae, Mzee Karume angevunja Muungano ?

Jawabu: Hata hii leo ikiwepo kura ya maoni Zanzibar asilimia 90 nadhani watasema wanataka mpango mwengine, hawataki mpango wa hivi sasa. Hili suala la muungano kwa sababu umma haukushirikishwa 1964, ulifanywa siri, ilikuwa siri ya watu wachache na tangu hapo hadi leo kuna malalamiko. Na Mzee Karume akisema, “Muungano ni kama reli, mnyonyoro unaounganisha behewa na behewa shoka la kuukata liko Zanzibar”, na mimi aliwahi kuniambia mara kadhaa shoka karibu atalinyanyuwa ili mnyonyoro ukatike, behewa la Tanganyika liende upande wake na behewa la Zanzibar liende upande wake. Nataka kusisitiza kwamba, hii miaka 42 hawezi mtu kusimama akasema kuwa Watanganyika na Wazanzibari wamepata manufaa kutokana na Muungano. Hakuna.

Mimi hapa kikubwa nilichokipenda ni kwamba Mzee Abeid Amani Karume kipindi chote cha Awamu ya Kwanza Zanzibar aliiendesha kama Dola huru, na pia kwa mujibu wa maneno ya Mh. Salim Said Rashid Muungano kwa Karume ilikuwa ni suala la Muda na Dharura tu.

Nataka kuwaambia wale wanaoenzi na kuheshimu Mapinduzi ya kweli ya Zanzibar, ambao ukiwagusa tu wanakuja na kauli za Mapinduzi Daima. Watambue Haya ndio Mapinduzi na kwa kiasi kikubwa Mzee Karume ameonesha dhana nzima ya Mapinduzi ilikuwa ni kujitawala na kujiamulia kwa maslahi ya Taifa.

Muandishi Ali Nabwa alikuwa na Msemo akisema “Siku Moja Itakua Kweli”, Siku hii Inakuja na ipo karibu na sisi wazanzibari tutaiharakisha iwe kesho ama keshokutwa Taifa letu liwe na maamuzi yake na Raisi wetu awe Raisi kamili sio Waziri kivuli asietambulika kimataifa, na bendera yenye motto juu tutaishusha tupandishe bendera Inayoiwakilisha Zanzibar Nchi za Nje hadi Umoja wa mataifa.

No comments:

Post a Comment