Monday 27 May 2013

WABUNGE TANGANYIKA WASUTANA KWA UROHO WA MADARAKA !!!

ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, amewashutumu wanasiasa wenzake kuwa siasa zao zimezorotesha ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Ngeleja ambaye ni mbunge wa Sengerema aliwasuta wanasiasa hao bungeni juzi wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Alitolea mfano wa ubishi uliojitokeza baina ya wanasiasa wakati akiwa Waziri wa Nishati na Madini ambapo taifa lilikuwa kwenye hali tete ya mgawo wa umeme.

Ngeleja alisema kuwa baadhi ya wanasiasa hao licha ya kutambua hali mbaya ya mgawo uliokuwa ukilikabili taifa, walikataa nchi isinunue mitambo ya kampuni ya Dowans kwa madai kuwa ni ya kifisadi.

Licha ya kutotaja majina ya wanasiasa aliowalenga, lakini katika kundi hilo walikuwemo mawaziri Samuel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe ambao mpaka sasa wanapinga serikali kulipa deni la kampuni hiyo baada ya kuvunja mkataba nayo kinyume cha utaratibu.

Dowans ambayo ilirithi mkataba wa kampuni ya Richmond LLC iliibuka wakati wa Bunge la Tisa chini ya Spika Sitta ambaye aliunda Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Mwakyembe kuchunguza uhalali wa kampuni hiyo.


Februari mwaka 2008, kamati ya Mwakyembe ilitoa ripoti yake ikionyesha kuwa Richmond ni kampuni hewa ya kufua umeme ambayo ilipewa mkataba kijanja, hatua iliyomlazimu aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa kujiuzulu.

Tangu wakati huo, Sitta na Mwakyembe pamoja na wanasiasa wengine wa vyama tofauti wamekuwa wakiishambulia kampuni ya Richmond hata baada ya kurithiwa na Dowans.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), ni miongoni mwa wanasiasa wachache walioshambuliwa na kundi kubwa pale alipoishauri serikali kuinunua mitambo ya Dowans wakati huo ikiuzwa kwa dola milioni 59.

Wazo hilo lilipata upinzani mkubwa na baadhi ya watu wakidai mbunge huyo ametumwa na serikali au kampuni hiyo ili kuhalalisha ufisadi wa Richmond.

Kundi hilo lililokuwa likipinga mitambo hiyo kununuliwa lilikuwa likijiegemeza kwenye sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004 inayokataza kununua mitambo chakavu lakini Zitto alishauri kuwa wanaweza kufanya marekebisho wakainunua ili kupunguza gharama za kuendelea kuikodi.

Vuta ni kuvute hiyo iliendelea hadi mitambo hiyo ikanunuliwa kampuni ya Symbion Power ya Marekani kwa dola milioni 159 na sasa inazalisha umeme na kuiuzia TANESCO.

Ni katika msingi huo, Ngeleja alidai kuwa wakati mwingine siasa kama hizo zimezorotesha uchumi na hivyo kuwaasa wanasiasa kuwa makini ili kuepuka kuikosesha nchi fursa.

“Sisi hapa tulikataa nchi isinunue mitambo ya Dowans kwa gharama nafuu tukiitwa ni mafisadi, tumehongwa lakini mitambo hiyo imenunuliwa na Symbion sasa inazalisha umeme na kutuuzia,” alisema.

Amtetea Kinana

Wakati huohuo, Ngeleja alimsafisha Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kutokana na tuhuma za kampuni yake ya uwakala wa meli kuhusishwa katika biashara haramu ya pembe za ndovu mwaka 2009.

Tuhuma hizo zimeibuliwa bungeni mara mbili tofauti na CHADEMA, kupitia mawaziri vivuli wao wa wizara za Maliasli na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa na Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ezekiel Wenje.

Katika juhudi za kumsafisha kiongozi huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi, Aprili 30 mwaka huu, baada ya Msigwa kuibua tuhuma hizo alichangia hoja hiyo akisema ni tuhuma za uongo.

Wiki iliyopita Msemaji Mkuu wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika, alimgusa Kinana akisema anatajwa na vyanzo mbalimbali kwamba amewahi kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya Artumas.

Mnyika alisema kuwa kampuni hiyo iliingia mkataba na serikali wa kuzalisha megawatt- 300 za umeme Mtwara eneo la Mnazi Bay.

Mkataba huo ulikuwa wa misingi ya mabadilishano ya gesi kwa nishati ya umeme; kwamba Artumas ingechimba na kuuza gesi asilia na kuilipa serikali kwa pamoja na mambo mengine kuizalishia umeme wa 300MW.

Mnyika alisema baadaye mwaka 2010 Artumas baada ya kufaidika vya kutosha kutokana na uvunaji na uuzaji iliacha kuendeleza mradi huo kwa kisingizio cha madai ya mdororo wa uchumi mwaka 2009 na kuuza hisa zake kwa kampuni ya Wentworth ya Ufaransa.

Katika utetezi wake, Ngeleja alisema uwepo wa Kinana kwenye kampuni hiyo ni jambo la kawaida lenye heshima kubwa ya kuaminika kwa kampuni kubwa.

Alitolea mfano viongozi wengine wakuu wastaafu wa kitaifa ambao wamewahi kuwa ama wanaendelea kuwepo kwenye bodi mbalimbali za kampuni tofauti kama wajumbe wa bodi au wenyeviti na kuhoji kwa nini taabu iwe kwa Kinana.

Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, naye wakati wa kuhitimisha hoja za wabunge waliochangia bajeti yake, alimtetea Kinana na kudai kuwa kiongozi anaonekana kuwakera CHADEMA ndio maana hawaishi midomoni mwao.

“Kwa hiyo, mimi nadhani mambo haya tuyaache tu, mwacheni Kinana afanye kazi yake tutapambana majukwaani na mwisho wa yote majibu mtayapata kwa wananchi mwaka 2015.

Naye Sitta Tumma toka Mwanza anesema Ngeleja akiwashambulia wanasiasa wenzake, Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema watuhumiwa wa kashfa ya ufisadi wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond na Dowans ni hatari na hawastahili kuungwa mkono katika uongozi.

Ingawa hakutaja majina, Sitta alisema watu hao wameanza kuhaha kutafuta uungwaji mkono katika safari yao ya kutaka madaraka.

Sitta alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph Bakita, katika Parokia ya Igoma jijini Mwanza.

Aliwataka Watanzania kujihadhari na watu hao kwa kuchagua watu waadilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwaka 2015.

Sitta alisema yeye na mawaziri wenzake watatu wameungana kifikra katika kupambana na uonevu na ufisadi dhidi ya rasilimali za nchi.

Kwa mujibu wa Sitta, mikataba ya kinyonyaji na kifisadi ya Richmond imeliingizia taifa hasara kubwa sana, kwani kwa sasa nchi inadaiwa mamilioni ya fedha kutokana na mikataba hiyo mibovu.

“Nchi ikiingia kwenye wimbi la ufisadi, fisadi atatafuta watu wa kumuunga mkono kupata uongozi. Atataka aungwe mkono na mkuu wa mkoa mwenye mtazamo wa kifisadi, na mkuu wa mkoa atamtaka mkuu wa wilaya kumuunga mkono fisadi.

“Na leo nawaambieni wananchi kwamba kura yako ni silaha ambayo ukiitumia vizuri italeta matumaini na utawala bora! Kwa hiyo, msidanganyike kuchagua walafi mwaka 2015, maana nchi itaingia kwenye matatizo makubwa ya ufisadi,” alisema Sitta.

Ingawa hakutaja jina la mtu, ni wazi kwamba Waziri huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pengine alikuwa anamlenga Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye mwaka 2008 alilazimika kujiuzulu kutokana na kashfa hiyo ya Richmond.

Alisema yeye na mawaziri hao watatu wako pamoja katika fikra za kupambana na vitendo vya kifisadi, uonevu na mikataba tata inayoliangamiza taifa na kwamba wako mstari wa mbele kutetea wanyonge.

Aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe pamoja na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.

No comments:

Post a Comment