Saturday 11 May 2013

MWENYEKITI MPYA WA TUME YA UCHANGUZI ZANZIBAR


Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Bw. Jecha Salim Jecha
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Bw. Jecha Salim Jecha


KUNA wanenao kwamba uchaguzi ndio uhai wa demokrasia na kwamba huohuo uchaguzi ndio wenye kuuua udikteta.  Hoja yao kubwa ni kwamba bila ya kufanywa uchaguzi ulio huru na wa haki mfumo wa demokrasia hauwezi kusimama.  Wanasema kwamba hivyo ndivyo demokrasia ifanyavyo kazi.
Wanausifu uchaguzi kwa mambo mawili matatu.  Kwanza wanasema uchaguzi ni chombo cha kuimarisha demokrasia na wakati huohuo ni lengo la demokrasia.  Uchaguzi pia ndiyo silaha ya kuzidhoofisha na hatimaye kuzimaliza tawala za kimabavu.
Hata hivyo, kama tulivyokwishawahi kuhoji katika sahafu hii kufanywa uchaguzi nchini kila baada ya kipindi fulani hakumaanishi kwamba nchi hiyo ni ya kidemokrasi. Inaweza ikawa hivyo lakini si lazima iwe hivyo.
Wala uchaguzi si silaha yenye kuweza pekee kuua utawala wa kimabavu.  Ingelikuwa ni hivyo basi chaguzi zingelikwishaziua na kuzizika tawala kadhaa za kimabavu katika sehemu mbalimbali za dunia.
Tunayasema hayo huku tukitambua kwamba demokrasia ya kileo haiwezi kuendelea bila ya kufanywa uchaguzi.   Lakini vilevile zipo tawala za kimabavu barani Afrika na nje ya Afrika zinazoutumia uchaguzi kuwadhibiti wapinzani. Kwa kufanya hivyo tawala hizo zinakuwa zinauendeleza udikteta wao.
Kuna serikali katika nchi za Kiafrika ambazo zamani zikiharamisha kuwako zaidi ya chama kimoja cha kisiasa na ambazo sasa zinaruhusu mfumo wa vyama vingi. Hata hivyo, serikali hizo hazijaukumbatia mfumo huo kwa moyo safi.
Serikali hizo hazina insafu na hufanya juu chini kuviandama na kuvibughudhi vyama vya upinzani. Lengo lao huwa ni kuendeleza utawala wa vyama vyao.
Vyama vya upinzani kwa upande wao huwa na kibarua kikubwa kuving’oa vyama vyenye kutawala. Mara nyingi vinashindwa kufanya hivyo kwa sababu ya mizungu inayofanywa na hivyo vyama vinavyotawala.
Nyakati nyingine vyama vinavyotawala huwa havina hata haya na husema wazi kwamba chaguzi nazifanywe lakini havitokuwa radhi kuitoa serikali kuwapa wapinzani na havina nia hiyo.  Kwetu Zanzibar hayo si mageni.  Tumekuwa tukiwasikia baadhi ya viongozi wa CCM, mara kadha wa kadha, wakisema kwamba katu hawatoitoa serikali.  Ni kana kwamba Mungu amewapa wao tu haki ya kutawala.
Hii ndiyo sababu kubwa kwa nini baadhi ya nchi hazishuhudii vyama vya upinzani vikiunda serikali.  Daima serikali huwa inaongozwa na chama kilekile kilichokuwa kikiendesha nchi katika enzi za mfumo wa chama kimoja cha kisiasa.
Vyama vya upinzani huwa havipewi fursa sawa za kuchuana na vyama vinavyotawala.  Aghalabu vyombo vya dola, vikiwa pamoja na idara za usalama, polisi, jeshi, vyombo vya habari vya serikali na tume za uchaguzi hutumiwa na serikali kuvikandamiza au kuviminya vyama vya upinzani.
Katika mazingira aina hiyo chama kinachotawala, kinachotumia nguvu na nyenzo za dola kuselelea madarakani nacho huwa ni chama cha dola. Huwa ni sawa na vyombo vingine vya dola, na kama si sawa, basi kinakuwa na mahusiano maalumu na hivyo vyombo vya dola, mahusiano ambayo vyama vya upinzani havinayo.
Wiki iliyopita Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar aliwateua wajumbe wepya wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).  Uteuzi wa wajumbe hao ni katika hatua za mwanzo zilizo muhimu za kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015. Wajumbe wenyewe wakiwa pamoja na mwenyekiti wao Jecha Salim Jecha walikula kiapo kuitumikia Tume Jumamosi iliyopita.
Mwenyekiti Jecha ambaye sasa amestaafu serikalini aliwahi kuwa naibu katibu mkuu na pia mjumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG). Kwa hivyo ana uzoefu mkubwa katika nyanja hizi za haki za binadamu na utawala bora ambazo zinaendana vizuri na jinsi shughuli za Tume ya Uchaguzi zinavyopasa ziwe.
Tume ya Uchaguzi ni chombo kilicho muhimu katika mfumo wa kidemokrasia hasa katika nchi kama za kwetu ambako uchaguzi huonekana kuwa ni jambo la kufa kupona. Tume hiyo inatakiwa daima iwe inafanya shughuli zake kwa haki na uadilifu wa hali ya juu wa kutopendelea upande wowote ule kati ya pande zinazochuana kisiasa.
Kwa ufupi, tume aina hiyo inatakiwa iwe huru. Bila ya kuwa huru haitoweza kuendesha shughuli zake kwa haki, kwa uwazi na bila ya upendeleo.  Kutokana na Katiba ya Zanzibar Dk. Shein ana haki ya kuwateua awatakao wawe wajumbe wa Tume ya Uchaguzi.
Amejaribu kuweka mezani sawa kwa kuwateua wakereketwa wa CCM, kuwarejesha wajumbe wawili wa chama cha CUF (baada ya kushauriana na viongozi wa chama hicho) na kumteua mmoja kutoka chama kidogo cha upinzani. Bila ya shaka ni jambo zuri kwamba vyama hivyo vinawakilishwa ndani ya Tume.
Hata hivyo, kuingizwa kwa wajumbe hao katika Tume ya Uchaguzi si hakikisho kwamba Tume hiyo itaendesha shughuli zake kwa haki na bila ya upendeleo. Mengi yatategemea jinsi Mwenyekiti wa Tume atavyokuwa anaziongoza shughuli za Tume bila ya kuingiliwa au yeye kuongozwa na vigogo wa chama kinachotawala.
Si siri kwamba tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe Tanzania mwanzoni mwa 1992 wapinzani Visiwani Zanzibar wamekuwa wakizishutumu Tume za Uchaguzi zilizopita kuwa zilikuwa zikikipendelea chama cha CCM.
Kutokana na yaliyojiri katika chaguzi za 1995, 2000, 2005 na hata 2010 maoni ya wachanganuzi wengi wa chaguzi za Zanzibar ni kwamba Tume za Uchaguzi za huko hazikuwa huru wala hazikuonyesha uwazi kabla ya uchaguzi na wakati wa uchaguzi. Wanadai kuwa Tume hizo zilidhibitiwa zaidi na wajumbe wa CCM na zikionekana kuwa kama Tume za Serikali badala ya kuwa Tume huru zisizopendelea chama chochote cha kisiasa.
Shtuma hizo ndizo zilizosababisha ile mipasuko ya kisiasa iliyokuwa ikizuka kila baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.  Ndipo pakafanywa mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar mnamo 2010 ili kumaliza migogoro hiyo kwa kupatikana Maridhiano ya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Mwanzoni mwa mwaka huu Dk. Shein alisema kwamba ana nia ya kuitanua demokrasia Zanzibar na kuhakikisha kwamba chaguzi zijazo zitakuwa huru, za haki na za kuaminika.
Tume ya uchaguzi ni halmashauri iliyotwikwa jukumu la kusimamia na kutekeleza shughuli na taratibu za uchaguzi na kura za maoni au za maamuzi. Shughuli hizo ni toka zile za kupanga mipaka ya majimbo ya uchaguzi; kusimamia kusajiliwa kwa raia wenye sifa zinazohitajika za kuwa wapiga kura; kuendesha na kusimamia uchaguzi wa Urais, wa bunge na wa serikali za mitaa.
Tume hiyo pia ndiyo yenye kusimamia shughuli za upigwaji kura za maoni. Inatakiwa iwe inatoa maelezo kuhusu uchaguzi na iwaelimishe wananchi na wapiga kura kuhusu vipindi mbalimbali vya mchakato wa uchaguzi na hasa kuhusu uchaguzi wenyewe.
Hii Tume mpya ina dhamana kubwa hasa tukizingatia jinsi jamii ya Wazanzibari ilivyogawika kisiasa na jinsi mahasimu wakubwa wa kisiasa walivyokuwa hawaaminiani au hawaziamini taasisi zinazosimamia uchaguzi.
Katika hali kama hizo kuna uwezekano mkubwa wa kuzuka vurumai na machafuko endapo kutakuwa na dhana kwamba chombo hicho cha uchaguzi kinatumiwa na chama chenye kuhodhi madaraka makubwa serikalini.
Kwa hivyo, ni muhimu Mwenyekiti wa Tume na wajumbe wake wahakikishe kwamba wao watachangia kuitanua demokrasia kwa kutozifuata tabia mbovu za Tume zilizotangulia. Lazima wajiamini ili wawe wabunifu wa fikra mpya za kusimamia uchaguzi.

No comments:

Post a Comment