Wednesday 8 May 2013

DR SHEIN ASEMA TUMEAMKA TOKA 1964, LAKINI BADO TUNA TONGO !!!


JUMUIYA ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) ingali inahangaisha akili za wakuu wa serikali pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliomo katika shinikizo kutakiwa kuifuta katika usajili, FAHAMU limebaini.
Ufuatiliaji wa kinachoendelea ndani ya serikali na matamshi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, umebaini kuwa kiongozi huyo anaumizwa na kivuli cha Uamsho na kusababisha kutoa kauli kali zinazoonesha sura yake halisi kiuongozi.
Mara kadhaa Dk. Shein ameshuhudiwa akitoa kauli dhidi ya jumuiya hiyo na viongozi wake waandamizi, wengi wakiwa wako gerezani kwa sasa kutokana na kukabiliwa na tuhuma za uchochezi wa fujo na kufanya mkutano usio na kibali cha Mufti ambaye ni kiongozi katika serikali.
Kwa namna rais na viongozi wengine wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) wanavyochukulia harakati za Uamsho, inadhihirisha kile kinachoelezwa na vyanzo vya habari kuwa “Uamsho inawahangaisha viongozi wakuu wa Serikali.”
Uchunguzi unaonesha kuwa kauli zinazotolewa na Rais Dk. Shein, baadhi ya wasaidizi wake serikalini na katika miongoni mwa makada wa CCM, zinaashiria chuki na nia mbaya waliyonayo dhidi ya viongozi wa jumuiya hiyo.
Uamsho ni jumuiya iliyosajiliwa kwa mujibu wa sheria za nchi, kama zilivyo jumuiya nyingine, ili kufanya shughuli zake. Shughuli kuu za Uamsho ni kuamsha wananchi kuhusu kutambua haki zao za kikatiba ikiwemo ya kuabudu.
Kauli mojawapo inayodhihirisha chuki za uongozi wa serikali dhidi ya viongozi wa Uamsho, ni ile aliyoitoa Dk. Shein hivi karibuni akiwa katika ziara ya kichama katika Mkoa wa Mjini Magharibi.
Akihutubia wanachama wa CCM katika kijiji cha Kinuni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Dk. Shein alisema: “Uamsho Uamsho, wanamuamsha nani hapa. Watu waliamka tangu mapinduzi ya Januari 12, 1964.”
Mapinduzi hayo yalifanywa na wana Afro Shirazi Party (ASP) waliokuwa hawakuridhika na serikali ya wananchi iliyoundwa baada ya Zanzibar kupata uhuru wake Desemba 10, 1963 na hivyo kuondoka kuwa chini ya uangalizi wa dola ya Mwingereza.
(Serikali ya Uhuru ilijumuisha viongozi wa vikundi mbalimbali vya kisiasa na kijamii na kuonesha uzoefu wa kwanza wa serikali kuendeshwa kwa mfumo wa umoja wa kitaifa).
Dk. Shein alitoa kauli hiyo katika kujibu matamshi aliyochomekewa na baadhi ya wanachama wa CCM waliposema “tunataka jumuiya ya Uamsho ifutwe.”
Baadhi ya waliotoa matamshi hayo imeelezwa kuwa ni viongozi wa mitaa mjini hapa wanaoitwa masheha ambao wanajulikana vema walivyo washabiki wakubwa wa CCM ingawa wanalipwa kwa fedha za kodi za wananchi wote.
Masheha walisikika wakisema harakati za Uamsho zimesababisha kuwabadilisha vijana wengi Zanzibar wakiwemo wale ambao kabla, walikuwa wakikipenda chama hicho cha CCM na kukichagua kinaposimamisha wagombea wakati wa uchaguzi.
Walisema vijana wengi wamekigeuka CCM kwa sababu wameshawishika kutokana na kuifuatilia mikutano ya hadhara na hotuba za viongozi wa Uamsho tangu pale walipoanza kufanya mikutano ya kushawishi watu kukataa mchakato wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Mheshimiwa Uamsho ifutwe… wasipofutwa watakiweka chama katika wakati mgumu kushinda uchaguzi ujao. Uamsho imewabadilisha vijana wetu na sasa kuwa wanaokichukia chama chetu na badala yake kuifuata CUF,” alisikika mmoja wa masheha akimwambia Dk. Shein.
CUF ni Chama cha Wananchi ambacho kwa lugha ya Kiingereza kinatambuliwa kama Civic United Front. Ni chama chenye nguvu kubwa Zanzibar kiasi cha kusema kimeporwa haki yake ya ushindi unapofanyika uchaguzi. Pia kinakubalika katika maeneo mengi ya Tanzania Bara.
Baada ya kusikia kauli hizo, imeelezwa kuwa ndipo Dk. Shein alipobadilisha gia. Alianza kuzungumza kwa hasira na kutoa matamshi makali ya vitisho dhidi ya jumuiya hiyo.
Rais wa Zanzibar amekuwa akitoa matamshi mara kwa mara ya kuonya kwamba serikali anayoongoza haitamvumilia mtu yeyote au kikundi chochote kinachochochea vurugu.
Wakati fulani Dk. Shein alisikika akisema serikali yake itawashughulikia watu wote wanaochochea vurugu na kusababisha kuvunjika kwa amani.
Hata hivyo, hakuna rekodi yoyote inayoonesha kuwa Uamsho imehusika na vitendo vya vurugu. Kwa sasa viongozi wake tisa wako gerezani wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali za uchochezi lakini kesi zao zote katika mahakama tofauti, hazijaanza kusikilizwa.
Moja ya kesi hizo iko Mahakama Kuu ya Zanzibar ambayo imeahirishwa kwa siku 60 ikisubiri Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aliyekata rufaa mbili kupinga maombi ya dhamana ya watuhumiwa.
Kesi hiyo inawahusu masheikh Farid Hadi Ahmed (42) anayeishi Mbuyuni, Mselem Ali Mselem (52) anayeishi mtaa wa Kwamtipura, Mussa Juma Issa (47) anayeishi Makadara, Azzan Khalid Hamdan (48) wa Mfenesini, Suleiman Juma Suleiman (66) wa Makadara, Khamis Ali Suleiman (59) wa Mwanakwerekwe, Hassan Bakari Suleiman (39) anayeishi Tomondo, Ghalib Ahmada Juma (39) wa Mwanakwerekwe na Abdalla Said Madawa wa Misufini.
Haijulikani ni lini hasa Mahakama ya Rufaa Tanzania itaketi hapa Zanzibar na wala haijafahamika kama rufaa hizo ni miongoni mwa zile zitakazopangiwa kusikilizwa na majaji watakaotumwa kuja kusikiliza rufaa za kesi zilizoamuliwa Zanzibar.
Mahakama ya Rufaa Tanzania ni moja ya mambo yaliyo katika orodha ya Mambo ya Muungano. Mahakama hiyo inapokutana Zanzibar, hushughulikia masuala yote isipokuwa yanayohusu mirathi miongoni mwa familia za Waislamu, na masuala ya haki za binadamu.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kijamii Zanzibar wameliambia gazeti hili kuwa ndani ya serikali kuna viongozi wenye chuki dhidi ya viongozi wa Uamsho kiasi kwamba hiyo imeleta mgawanyiko katika serikali.
Viongozi wengine hasa wanaotoka CUF wamekuwa wakionekana kama wanaounga mkono shughuli za Uamsho hata baadhi yao kudaiwa kuwa wanafadhili shughuli za jumuiya hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai aliwahi kukaririwa na moja ya magazeti nchini mwaka jana akimlaumu kiongozi wa juu wa CUF aliyemo serikalini (hakumtaja kwa jina) kwamba anaunga mkono viongozi wa Uamsho na harakati zao.
Vuai alipoulizwa kama kiongozi anayemlenga katika maelezo yake ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema, “Sina haja ya kumtaja, unamjua wewe.”
Vuai alinukuliwa akisema kwamba tatizo kubwa lililopo Zanzibar ni kwamba baadhi ya viongozi wa upinzani ndani ya serikali wanachochea harakati zinazosukuma wananchi kuvunja amani iliyopo.
Alitahadharisha kuwa mwenendo huo utahatarisha mshikamano katika serikali ya umoja wa kitaifa inayoundwa na CCM na CUF.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Shein alikumbana na kadhia ya kushinikizwa kuifuta Uamsho alipokuwa katika ziara ya kichama Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika eneo moja akiwa kwenye mkutano wa ndani na viongozi waandamizi wa chama, alilalamikiwa kuwa serikali haijachukua hatua kuondoa bendera za Uamsho zilizojaa kwenye miti na milingoti kama ilivyofanya katika Mkoa wa Mjini Magharibi.
Haikufahamika haraka jibu la Dk. Shein ambaye anajua kuwa Uamsho imesajiliwa kulingana na sheria na kuifuta kimbinu itaonyesha ukandamizaji wa haki za wananchi kujiundia taasisi za kuendesha shughuli zao. Pia itafungua milango ya wadhamini wa jumuiya hiyo kudai haki mahakamani.
Serikali ya Dk. Shein imekuwa katika shinikizo nyingi za kutakiwa kuifuta Uamsho, zikiwemo zile zinazotolewa na taasisi za dini shindani kwa kuituhumu kuwa viongozi wake wanahusika na vitendo vya kuchoma makanisa na kudhuru viongozi wa dini na serikali nchini.
Viongozi wa Uamsho wanaokabiliwa na tuhuma mahakamani tangu Oktoba mwaka jana, wamenyimwa dhamana baada ya DPP kutoa kibali cha kuzuia kutolewa kwa dhamana hiyo bila ya kueleza sababu hata moja.
Kutakiwa kutoa sababu kwa maandishi ni moja ya madai aliyoyakatia rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania, kutokana na agizo la Jaji Fatma Hamid Mahmoud katika hatua zake za kwanza alipopangiwa kusikiliza kesi hiyo.
Jaji Fatma ndiye aliyeiahirisha kesi hiyo kwa siku 60 kutoa nafasi kwa DPP kukata rufaa. Siku hiyo alisema baada ya muda huo, atasikiliza kesi hiyo bila ya kujali kama rufaa imeamuliwa ama laa.
Viongozi wa Uamsho pia wana kesi nyingine katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu Khamis Rashid. Kesi nyingine katika mahakama hiyo ilifutwa baada ya Hakimu Mshamba kusema upande wa mashitaka umechukua muda mrefu kusubiriwa kukamilisha upelelezi.
Kesi nyingine ya mashitaka yanayofanana, ya uchochezi wa kufanya fujo, iko katika Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini, Mfenesini.

No comments:

Post a Comment