Tuesday 7 May 2013

WAANGALIENI WATANGANYIKA WALIVYO KUWA HAWATAKI ZANZIBAR KUWA NA MAMLAKA KAMILI !!!


MIAKA 29 iliyopita, Januari 1984, Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), iliyoketi mjini Dodoma kwa dharura, ilimvua (ilimpindua?) nafasi zote za uongozi, Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Alhaj Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi kwa kutenda ‘dhambi kuu’ ya kuhoji muundo wa sasa wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Nyadhifa alizovuliwa kiongozi huyo na kubakia kuwa raia wa kawaida na kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwake kwa kipindi kadhaa, ni pamoja na urais wa Zanzibar, uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, umakamu wa Rais wa Tanzania na umakamu Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Mkutano huo ulitawaliwa na kampeni chafu dhidi ya Jumbe, huku kambi mbili za Zanzibar zikiumana, kwa kambi moja kuunda tuhuma dhidi yake na nyingine kujibu mapigo, na hivyo kuchonga ufa na uhasama mkubwa miongoni mwa viongozi wa Zanzibar kati ya kambi mbili hizo kinzani; kambi iliyojiita ya ‘Wakombozi’ (Liberators), iliyoundwa na waliojiona kama watetezi halisi wa Mapinduzi ya 1964 na ile ya kambi ya ‘Wanamstari wa mbele’ (Front liners), iliyotaka mabadiliko ya sera visiwani.
Katika msuguano huo, Kamati ya Wakombozi ilishindwa na Rais Jumbe akatunguliwa kwa mzinga mzito, akaisha. Jumbe alikuwa mrithi wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, aliyeuawa katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililoshindwa, Aprili 7, 1972. Kabla ya hapo, Jumbe alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, akishughulikia mambo ya Muungano.
Kuuawa kwa Karume kulifikisha tamati ya utawala wa awamu ya kwanza kufuatia Mapinduzi ya 1964, utawala uliotawaliwa na vitisho, hofu, umwagaji damu na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya yeyote aliyetoa sauti kuhoji utawala huo, na au kwa aliyedhaniwa tu kuwa mpinzani wa Mapinduzi. 
Uporaji huo wa demokrasia, ulitekelezwa na utawala wa Karume kupitia genge katili lilojulikana kwa jina la ‘The Gang of Fourteen (Genge la Watu 14), likiongozwa na Kanali Seif Bakari. Kugongewa mlango tu usiku na genge hilo enzi hizo, kulitosha mtu kupatwa hofu kabla ya kuhojiwa.
Genge hili na sehemu kubwa ya wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, walitaka kuendelezwa kwa sera za Karume, na mtu pekee waliyeona angeweza kufanikisha hilo kama mrithi halali wa Karume, ni huyo Kanali Seif Bakari.
Hata hivyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere aliposikia hilo, akaona giza mbele. “Sera za Karume tena? Ukatili na mauaji ya kutisha kwa watu wasio na hatia? Hapana!” alisikika Mwalimu aking’aka mbele ya watu wake wa karibu, na kuamua kutokubaliana na pendekezo la Wazanzibari lililomtaka Kanali Bakari kumrithi Karume. Akajenga hoja nzito kupangua kisayansi hoja hiyo kwa kuhusisha na tukio la kuuawa kwa Karume!
Jaribio la mapinduzi lililoshindwa liliandaliwa na wanasiasa makini wa Kizanzibari kwa kuhusisha baadhi ya wanajeshi wa Jeshi la Zanzibar, ambalo hadi akiuawa, Karume alikuwa bado Amiri Jeshi Mkuu wake; kwa kushirikisha pia wanajeshi kadhaa wa Kizanzibari waliokuwa kwenye Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT) kwa upande wa Bara.
Muuaji wa Karume, Luteni Hamoud Mohammed Hamoud, alikuwa wa Jeshi la Zanzibar.  Alichukua hatua hiyo yeye mwenyewe baada ya kuhisi kwamba mpango wa mapinduzi umegunduliwa siku hiyo, na kwamba yeye na wenzake walikuwa wanatafutwa; na kwa sababu kikosi cha pili cha mapinduzi kutoka Dar es Salaam kilishindwa kufika Zanzibar muda uliopangwa, baada ya kuonywa kikiwa baharini juu ya kugunduliwa kwa mpango huo na kurejea hima Dar es Salaam.
Luteni Hamoud aliona kwa mikasa hiyo miwili, kwa vyovyote vile, angekamatwa na kuuawa kikatili. Akaamua na lolote liwe, na bila kupoteza muda akaamua kutekeleza mauaji hayo yeye mwenyewe na wenzake wengine watatu tu.
Imeelezwa kwamba ushiriki wa Luteni Hamoud katika jaribio hilo, mbali na kubeba hisia (sentiments) za kisiasa, pia alidhamiria siku nyingi tangu nyuma, kulipiza kisasi kwa Karume kwa kifo cha baba yake, Mzee Mohammed Hamoud, aliyeuawa kikatili na kiongozi huyo akiwa kizuizini kwa sababu za kisiasa.
Mwalimu Nyerere hakutaka mauaji ya Rais Karume yatafsiriwe au yahusishwe na jaribio la mapinduzi, bali alitaka yatafsiriwe kama mauaji ya kisiasa tu. Akasema, hatua yoyote ya kumteua Kanali Seif Bakari ambaye ni mwanajeshi, kuchukua nafasi ya Karume aliyeuawa na mwanajeshi pia, kungetafsiriwa kama Mapinduzi ya Kijeshi. Hapo, Wazanzibari wakanywea, wakatazamana kwa ishara bila kupata jibu kwa hoja ya Mwalimu Nyerere. Hawakuwa na namna isipokuwa kufuta pendekezo la uteuzi wa Kanali Seif Bakari kumrithi Karume.
Ndipo ikawadia zamu ya Mwalimu Nyerere kushawishi na kushauri  nani ateuliwe. Akasema, pamoja na kuuawa kwa Karume, ambaye alikuwa mwasisi mwenza wa Muungano wa Tanzania, Muungano huo lazima uendelezwe bila kuyumba; na mtu pekee aliyefaa, kwa maoni ya Nyerere, alikuwa ni Aboud Jumbe Mwinyi, kwa sababu kuu tatu:-
Mosi, ni msomi na mwanasiasa mkongwe mwenye kuzielewa vyema siasa na migongano ya jamii ya Kizanzibari. Pili, ni mtu ambaye hakuwa na majungu wala makundi yenye kuhasimiana. Tatu, wadhifa wake wa Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (Mambo ya Muungano) kwa muda mrefu, ilikuwa ni sifa ya ziada iliyompa uzoefu, na uwezo wa kuendeleza na kudumisha Muungano.  Hoja ya Mwalimu ikapita; Jumbe akapaa, akawa Rais wa Zanzibar wa awamu ya pili.
Jumbe na Mwalimu Nyerere walifanana kwa mengi. Wote walikuwa wasomi waliosoma pamoja Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, na kisha wote wakawa walimu wa sekondari. Kwa uhusiano mzuri huo, Jumbe alianza kulegeza mengi yenye ukakasi visiwani ambayo yasingewezekana enzi za Karume ambaye aligeuka mwiba kwa Mwalimu, akidai mara nyingi wavunje Muungano kwa kuwa uligeuka koti lililowabana Wazanzibari. Chini ya Jumbe, misuguano kati ya Bara na Visiwani  ambayo kabla yake ilizua kero za Muungano, ilianza kutoweka.
Jumbe alianza kukubalika haraka kwa wengi Visiwani na Bara; akawa kipenzi cha Rais wa Muungano, naye akaanza kupaona Bara kama nyumbani kwake. Akajenga makazi yake eneo la Mjimwema, Dar es Salaam. Akilala Mjimwema na kila asubuhi aliruka kwa ndege kwenda Ikulu ya Unguja na kurejea tena jioni baada ya kazi. Ufanisi wake wa kuihudumia Zanzibar ulipungua kwa sababu ya kuweka nguvu kubwa zaidi kwenye Muungano. Na kadri alivyozidisha ziara za kirais Bara na nje ya nchi kumwakilisha Mwalimu, (majukumu ambayo Mwalimu hakuthubutu katu kumpa Karume), ndivyo alivyozidi kujiweka mbali na siasa za Zanzibar na Wazanzibari.
Kwa kutumia hali hiyo ya maridhiano, Mwalimu alizidi kuchanja mbuga kwenda mbele zaidi bila Jumbe kushuku kitu. Katika kikao cha pamoja cha NEC ya TANU cha Bara na NEC ya ASP cha Zanzibar, kilichofanyika Dar es Salaam, Septemba 5, 1975, Mwalimu Nyerere alipendekeza vyama hivyo viungane ili kuimarisha zaidi Muungano.
Jumbe alikubali kimsingi wazo hilo, lakini akataka ASP kipewe muda kufikiria zaidi. Mwaka mmoja baadaye, Oktoba 1976, maridhiano yakafikiwa ya kuunda Chama kipya ‘Chama cha Mapinduzi’ (CCM), kilichozinduliwa Februari 5, 1977, tarehe na mwezi sawa na ilipozaliwa ASP miaka 20 nyuma, mwaka 1957.
Licha ya Wazanzibari kushinikiza tarehe na mwezi wa kuzaliwa chama chao, yaani Februari 5, walishinikiza pia na kufanikiwa kubakiza neno ‘Mapinduzi’ yaliyoleta uhuru wao Januari 12, 1964, liwe sehemu ya jina la chama kipya. Kwa maana ya Chama cha Mapinduzi bila kuwa na tafsiri yake kwa lugha ya Kiingereza.
Na hizo ndizo zilikuwa karata mbili pekee kwa Wazanzibari kukubali kuunda Chama kipya, chama ambacho kilipewa ukuu wa kikatiba wa kushika hatamu zote za uongozi wa nchi na kuweza kumng’oa madarakani Jumbe miaka saba baadaye, mwaka 1984, kama kitanzi alichojitengenezea mwenyewe. Hata hivyo, kwa mujibu wa Hati (Mkataba) ya Muungano ya Aprili 22, 1964, vyama vya siasa si jambo la Muungano kuweza kusimamia mamlaka za Muungano. Hivyo utaratibu uliotumika kumng’oa Jumbe unahojika kisheria!
Kadri Jumbe alivyozidi kujiona kukubalika kwa Mwalimu Nyerere, ndivyo alivyojiona pia kama mrithi halali mtarajiwa wa Rais wa Muungano kuliko mtu mwingine yeyote, Bara na Visiwani. Lakini kutokuwepo kwake Zanzibar mara kwa mara kulizua ombwe la uongozi kwa kuwa kila kitu kilimsubiri yeye, hata kama ni idhini ya kukata mti. Na kwa jambo la dharura, Waziri mwenye dhamana ya dharura hiyo ilibidi amfuate Dar es salaam.
Kana kwamba ombwe hilo halikutosha, hofu ilitanda miongoni mwa Wazanzibari pale Mwalimu alipopendekeza mabadiliko zaidi ya Katiba kutaka kuunda Serikali moja badala ya Serikali mbili, wakihofia  nchi yao kumezwa na Tanganyika.  Hali hii ilimweka pabaya Jumbe Visiwani juu ya uswahiba wake na Nyerere, wakimwita ‘msaliti’ wa Mapinduzi ya Zanzibar na Wazanzibari.
uona hivyo, Jumbe alianza kugeuka nyuma kwa kuchanganyikiwa; akawa njia panda. Wakati hilo halijapoa, jingine kubwa zaidi lilikuwa njiani likija. Mwaka 1983, Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Muungano, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu. Sokoine alikuwa na mvuto wa watu, shupavu na mwadilifu kiasi kwamba katika kipindi kifupi tu alijidhihirisha kuwa chaguo la watu na mrithi halali wa Mwalimu, ambaye naye alimkubali kwa ishara na kwa vitendo.
Kwa kuridhika na Sokoine, taratibu Mwalimu alianza kumbeza Jumbe kwa sababu nyingi, lakini itoshe hapa kutaja mbili tu.  Kwanza, alimwona kama kiongozi mpweke asiye na sapoti na aliyepoteza mvuto Visiwani, pia kama dikteta mkimya asiyeshaurika na watu wa chini yake.
Pili; Mwalimu aliudhika kwa Jumbe kugeuka mhafidhina wa kidini na mpambanaji wa Kiislamu katika Taifa lisilo na dini. Kwa hili, Jumbe alizuru nchi nzima akitoa hotuba kwenye misikiti, na Serikali ikalazimika kutoa Waraka mkali wa Rais, kuwakumbusha na kuwataka viongozi wa kitaifa kutojipambanua au kuendekeza mambo ya kidini. Jumbe alipuuza Waraka huo; kwake ndio kukawa kumekucha.
Habari za Mwalimu kupoteza imani na upendeleo kwa Jumbe hatimaye zilimfikia kiongozi huyo, zikamuuma sana na kumvunja moyo. Hapo uhasama ukazuka kati yake na Mwalimu kwa njia ya kukomoana. Kwa hasira na kukata tamaa, Jumbe akaanza maandalizi ya kuumbua Muungano, kwa minyukano na Mwalimu.
Kuanzisha minyukano hiyo, ilikuwa ni lazima kwanza Jumbe arejeshe imani yake iliyopotea kwa Wazanzibari, kutokana na hatua yake ya kuhamia Mji mwema, Kigamboni na kwa kuwatelekeza Wazanzibari. Baada ya kuridhika kwamba mambo ameyaweka sawa, aliomba mawazo ya Makatibu Wakuu wa Wizara zote na Watendaji Wakuu wengine wa Serikali, ni aina gani ya Muungano unaotakiwa.
Wote, isipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Zanzibar, Damian Lubuva, walikataa muundo wa sasa wa Serikali mbili au wa Serikali moja uliokuwa umeanza kupigiwa upatu na Mwalimu na baadhi ya wanasiasa. Jumbe na watendaji wake hao ndani ya Serikali ya Zanzibar wakapendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu. Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano kwa mambo kumi na moja tu yaliyoainishwa katika Mkataba wa awali wa Muungano.
Mtizamo huo ndio aliouweka wazi Jumbe baadaye katika kitabu chake kiitwacho ‘The Partnership,’ yaani ‘Ubia kati ya Tanganyika na Zanzibar,’ kilichosambazwa mwaka 1984. Kuthibitisha hilo, ananukuu ibara ya tano ya Mkataba wa Muungano inayosema kwamba kufuatia kuundwa kwa Serikali ya Muungano, “Sheria za Tanganyika zilizopo na zile za Zanzibar, zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo.” (The Partnership, uk. 22).
Vivyo hivyo, anathibitisha kwa kunukuu Ibara ya Sita (a) ya Mkataba, inayotanabahisha kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano, atasaidiwa na Makamu wawili wa Rais (mmoja kwa ajili ya Tanganyika na mwingine kwa ajili ya Zanzibar), Mawaziri na Maofisa wengine anaoweza kuwateua kutoka Tanganyika na Zanzibar ambapo kufuatia uteuzi huo, utumishi wao utahamishiwa kwenye utumishi wa Serikali ya Muungano.
Anahoji: “Kwa kuwa Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano Namba 22 ya 1964, vinatambua uwapo na kubakia kwa Serikali za Tanganyika na Zanzibar baada ya Muungano, kwanini Muundo uliokusudiwa usitafsiriwe kuwa Shirikisho? Kama Tanganyika na Zanzibar zinatajwa kuwa nchi ndani ya Muungano, lakini kwa vitendo na hulka kuna nchi ya Zanzibar pekee, Tanganyika ilikwenda wapi?
Hatua iliyofuata na aliyochukua Jumbe, ilikuwa ni kumrejesha kwao Tanzania Bara, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Damian Lubuva, akimwelezea kama mtumishi asiyeweza kusimamia maslahi ya Wazanzibari; na badala yake akamteua rafiki yake wa zamani, raia wa Ghana, Alhaj Bashir K. Swanzy kuwa Mwanasheria Mkuu.
Kuanzia hapo, madai ya Wazanzibari kutaka mabadiliko ya Katiba, huku wengine wakitaka warejeshewe Visiwa vyao (Zanzibar), kupitia mihadhara, magazeti na redio, yalipamba moto ambapo wanajeshi wa Kizanzibari nao walikuwa na malalamiko yao.
Mashambulizi yenye kashfa nzito nzito na matusi ya kisiasa yaliongozwa na redio ya ufichoni iliyopachikwa jina la ‘Kiroboto Tapes,’ hadi ilipogunduliwa na kuharibiwa na wanajeshi kutoka Bara. Mitafaruku yote hii ilikuwa na ridhaa ya Alhaj, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi.
Wiki ijayo, tutaona jinsi Jumbe alivyoandaa mashitaka dhidi ya Jamhuri ya Muungano kwenye Mahakama Maalum ya Katiba, lakini akatunguliwa kabla ya kufika Mahakamani.

1 comment:

  1. Makala nzuri lakini sijui watu wangapi wanafuatilia halafu ushauri wangu ni kuwa unapoandika nakala usifanye kama wewe ndio muandishi hii sio kazi yako halisi ni nukuu ya watu sasa uzuri ukamweka mwandishi halali ili watu wajue kwanza ni nakala ya ukweli pili kuepusha matatizo

    ReplyDelete