Wednesday 8 May 2013

SHEIN ANY"EREKESHWA NA WANA MASKANI !!!

BAADA ya kupewa imani na wananchi kwa kuonekana atajenga misingi imara ya umoja wa kitaifa hivyo kuharakisha maendeleo ya nchi na watu wake, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amebadilika sana.
Dk. Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (BLM), kwa kweli ameanza kuwa kiongozi asiyetabirika, asiyeaminika na asiyetumainiwa kwamba aweza kukidhi matarajio ya watu kimaendeleo.
Kwanini hatabiriki? Kwanini haaminiki? Na kwanini hatumainiwi kubadilisha hali ya nchi kutoka kugubikwa na umasikini kwa sehemu kubwa ya watu wake?
Dk. Shein ni kama vile amepoteza mwelekeo katika kuongoza. Lakini ni kwanini apoteze mwelekeo mapema hivo? Hili kwa hakika ni swali gumu na zito kulijibu. Ndivyo nionavyo kwamba pengine hata kujaribu kulijibu tu, inaweza kuchukua muda kufikia hatua.
Nilibahatika kuwa mmoja wa watu waliomsikiliza kwa makini siku alipokuwa anahutubia umma wa wananchi wa Unguja na Pemba ndani ya Baraza la Wawakilishi alipolizindua rasmi. Rais alikuwa katika shughuli zake za mwanzomwanzo baada ya kuwa ametangazwa mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010.
Moja ya ahadi alizozitoa mbele ya umma wa Wazanzibari ni kuongoza serikali kwa misingi ya Katiba na Sheria na kwa kufuata utawala bora. Ahadi hiyo ni pamoja na kusema kwamba atasimamia ipasavyo jukumu la utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama chake – CCM.
Inafaa kukumbuka na kutambua mapema kuwa CCM ndicho chama alichokiwakilisha katika kugombea urais, baada ya kuwa amepewa ridhaa na mkutano mkuu wake uliofanyika mjini Dodoma miezi kadhaa kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika.
Dk. Shein pia aliahidi kuleta maendeleo ya Zanzibar na watu wake kwa kutumia raslimali zilizopo, huku akitarajia wananchi nao kushiriki kikamilifu katika kuzalisha mali.
Ilikuwa ni matarajio ya watu wengi kwamba alikuwa anayajua majukumu mazito yanayomkabili ya kiuongozi. Lazima alikuwa anajua kuwa anaanza kushika usukani wa kuongoza watu wachache katika nchi yao ndogo tu lakini waliochoka kuongozwa chini ya siasa za chuki na hasama.
Watu wa Zanzibar walikuwa wamechoka umasikini na wamechoka kuongozwa na mtu anayedharau mahitaji yao. Daktari itakuwa alijua ana mtihani mgumu wa kuridhisha watu na matumaini yao. Haya aliyajua.
Mimi sina shaka hata chembe Dk. Shein anajua na alikuwa akijua wakati ule anaingia Ikulu, kuwa watu wa Zanzibar ni wastaarabu, tena waungwana na wakarimu sana.
Daktari anaujua ukweli huu kwa sababu amezaliwa Zanzibar, amekulia Zanzibar na anawajua wananchi kwa hulka zao, mila zao, utamaduni wao. Anajua kitu gani wanakipenda na kipi hawakipendi. Anajua wakati gani wanavumilia maskhara, mizaha na kauli za dhihaka.
Kuliko yote hayo, Dk. Shein anajua na alikuwa akijua fika tangu wakati ule anaingia kutaka uongozi wa juu kuwa ukitaka kumjua Mzanzibari kwa kiasi gani hastahamili maudhi, basi mtolee maneno ya dharau na kebehi pasipostahili.
Mzanzibari havumilii maudhi hasa pale anapoamini kuwa huyo anayemuudhi anamfanyia hivyo kwa sababu anamdharau na kumbeza.
Nazijua simulizi nyingi za vijana wenziwe wa wakati huo wakimzungumza jinsi yeye alivyokuwa mtu wa mizaha na maskhara vilevile. Ilikuwa ni muhimu kwake kuijua mizaha kwa sababu akishinda na vijana wapenda mizaha. Niseme Dk. Shein amecheza ndani ya mizaha na maskhara.
Imekuwa bahati mbaya kwamba akiwa kiongozi wa Zanzibar sasa, ameamua kutumia kauli za kibabe, kebehi na dharau kwa wananchi. Ni wananchi walewale ambao aliahidi kuwapenda, kuwaengaenga, na kuwasaidia kupata maendeleo.
Dk. Shein amekuwa mtu wa ajabu kabisa kiasi cha kuonekana kama vile amepoteza mwelekeo katika kuongoza kwake serikali ambayo kutokana na yaliyotangulia kabla ya uchaguzi mkuu ule wa 2010, inatambulika kuwa ni Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Katika ziara yake ya kichama ya mikoa yote mitano ya Zanzibar aliyoikamilisha mwishoni mwa wiki, Dk. Shein amesikika hadharani akitoa kauli za kudharau mamlaka ya wananchi ambayo anajua ndiyo iliyompeleka Ikulu.
Kauli nyengine alizozitoa nazichukulia kuwa ni kauli za kutisha na kwa mbali ni za kuwavunja moyo wananchi.
Hebu tafakari haya yafuatayo: “Mnaitakia nini serikali yangu… mimi nina miaka kumi ya uongozi wa juu… sijashindwa kuongoza… siogopi mtu yeyote mie… asiyetaka muungano huu wa serikali mbili ahame.”
Hivi Dk. Shein anamwambia nani kwamba anaongoza serikali yake? Anamfahamisha nani kuwa yeye ni mbobezi katika uongozi? Anamjuilisha nani kwamba hajashindwa kuongoza? Anamwambia nani kuwa yeye ni jabari asiyeogopa mtu yeyote?
Dk. Shein anapotoa sauti nzito jukwaani – ni jukwaa la CCM ijulikane – ya kuwaambia wananchi kuwa asiyetaka muungano wa serikali mbili ahame nchi, yaani Zanzibar, analenga kuonesha kitu gani?
Kwa tafsiri nyepesi na ya haraka, unakuta Dk. Shein amepoteza mwelekeo kama kiongozi. Ameamua kuchukua mkondo wa dharau, chuki na kibri dhidi ya wananchi, wale alioahidi kuwapenda na kuwaongoza kwa misingi ya utawala bora.
Kila mtu anaweza kukubali kwamba Dk. Shein anao uzoefu wa uongozi – na hii ni kama tu kuongoza kwa muda huo wa miaka aloitaja na kujigamba, ni kipimo kweli cha uzoefu katika uongozi.
Hapa linakuja swali, je kuongoza kwa muda huo ndiko kumemvimbisha kichwa na sasa kuamua kuwapandia vichwani wananchi? Kwamba kwa kuwa amekuwa kiongozi kwa muda huo anaojinasibu, basi ndio watu waseme amekuwa kiongozi hodari?
Si kweli hata kidogo. Kiongozi hodari na muadilifu hapimwi kwa muda alioongoza; kwa sababu wapo viongozi wenye muda mfupi kuliko alioongoza yeye Dk. Shein lakini wamejijengea sifa nzuri ya uongozi mwema.
Dk. Shein anapaswa kufahamu leo kwamba uongozi mwema haupimwi kwa muda ambao mtu ameongoza. Uongozi mwema na ulio bora, hupimwa kwa matendo ya kiongozi mhusika na kwa namna anavyotambua dhamana aliyonayo.
Kiongozi mwema hupimwa kwa vile anavyotekeleza mipango ya serikali anayoiongoza. Inaleta tija hiyo mipango? Inatoa matokeo yanayoonekana au yanayopimika? Au matokeo ya kwenye makaratasi huku yakishindwa kuakisi hali halisi ya mambo ilivyo?
Kiongozi akishafikia hatua ya kuthubutu kukebehi wananchi, kuwafanyia mizaha na tambo, kuwatolea maneno ya jeuri na dharau, kuwatunishia misuli ya shingo huku ukiwatolea macho ya hasira, huyo huwa anajionesha kuwa si kiongozi bora. Huyo ni kiongozi mbabe.
Dk. Shein anapotea njia kusema kweli. Anaiacha njia ile aliyoahidi kuwaongoza watu na kuchukua njia iliyojaa tope, mashimo na miiba. Haikubaliki kutumia njia ambayo ina nyevule, au kenge, au nyoka na au simba mla watu. Ni njia ya hatari hiyo.
Sasa, Dk. Shein achukue hatua ya kurekebisha haya. Arudi kwenye mstari kwa kuwaongoza watu kwa kauli njema na zile zinazoonesha upendo na huruma kwao. Aongoze kwa kuwasikiliza watu, kuzingatia wasemayo, kuyafanyia kazi matatizo yao na hatimaye kuyapatia dawa.
Pale ambapo haitawezekana kuyapatia dawa matatizo ya wananchi, basi ni vema akawaeleza kwamba haiwezekani kwa sababu zipi. Kiongozi anapaswa kusema waziwazi kuwa hili naliweza kulitatua na litachukua muda kadha. Aseme wazi hili nitalitatua hatua kwa hatua, na hili litahitaji muda mrefu zaidi.
Hizo ni kauli za matumaini kwa watu. Ni kauli zinazowatia moyo wananchi wenye matatizo kama walivyo wengi wa wananchi wa Zanzibar.
Kauli kama hizo zinawajenga wananchi na kuwasukuma kuzidi kuwapa imani viongozi wao. Ni tofauti kabisa na kauli za kebehi, jeuri, chusha na vitisho. Hizi hazijengi, hazitii moyo watu na wala haziwapi matumaini kwamba waendako si kubaya hivyo.
Wananchi wa Zanzibar hawataki kiongozi kutamba wakati matatizo yao mengi yanaendelea kukua – maji haba, tiba duni, elimu mbovu, uchafuzi wa mazingira, uporaji wa ardhi za wananchi pamoja na rushwa, uzembe na wizi ndani ya serikali na taasisi zake. Haya yanazorotesha maendeleo ya nchi.
Wazanzibari hawataki kiongozi ambaye anawakejeli na kuwadhihaki huku akishindwa kudhibiti watendaji wahuni, wazinzi na walevi wa madaraka wanaoendekeza ufisadi.
Wazanzibari hawataki kiongozi anayetoa kauli za vitisho kwao kama vile wapo kwenye nchi iliyo vitani. Hawataki kiongozi wa staili hiyo. Hawataki kiongozi anayetekenyeka kirahisi anaposikia kauli za wapambe wake.
Kiongozi anasikiliza kauli za wapambe na kuzipima kabla ya kuzitolea neno lolote. Ni kwa sababu moja tu: Tamko lolote atoalo kiongozi siku zote huchukuliwa kwa uzito wake.
Wala haitakubalika kuja baadaye kiongozi huyo na kusema kwa watu kwamba eti alijisahau. Kujisahau? Kiongozi gani ambaye hujisahau na kutoa kauli zinazoudhi watu anaowaongoza? Hata hii yenyewe haikubaliki. Kiongozi lazima achunge ulimi wake.
Wazanzibari hawataki kuwa na kiongozi anayejisahau na kujiachiaachia mbele ya watu wengine. Kama alivyo binadamu kikawaida, kiongozi anatakiwa kufikiria mara mbili kabla ya kutoa kauli yoyote. Kwamba je, akiitoa kauli hiyo itachukuliwaje na wananchi?
Hebu ajiulize Dk. Shein anapowaambia wananchi kuwa “mnaitakia nini serikali yangu” ana maana kwamba serikali anayoiongoza ni yake binafsi? Ni serikali yake kama ilivyo familia yake?
Tafsiri rahisi ya kauli hiyo ni kwamba sasa Dk. Shein ameanza kuwa dikteta. Hataki kusikia wananchi wanasema yao na yale mambo yanayohusu serikali yao. Wasieleze shida zao, mahitaji yao, matatizo yao. Wasiulize vipi serikali yao inaendeshwa, wasihoji namna gani fedha zao zinatumika?

No comments:

Post a Comment