Tuesday 2 April 2013

Kichanga chawekwa ndani ya begi na kutupwa


MTOTO mchanga wa siku mbili amefariki dunia jijini Dar es Salaam baada ya mama yake kumweka ndani ya begi na kumtupa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minagi alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi maeneo ya Mongolandege Ulongoni baada ya mama wa mtoto huyo, Sauda Patric (14) mkazi wa eneo hilo kujifungua nyumbani kwa shangazi yake, Hadija Mwasite.
Alisema baada ya tukio hilo polisi walifanikiwa kumkamata mama huyo na baada ya kumuhoji alidai kuwa alijifungua siku mbili zilizopita akiwa jikoni nyumbani kwa shangazi yake huyo.
Kamanda Minagi alisema mwili wa kichanga hicho umehifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema kuwa juzi maeneo ya Mbezi, mwili wa Magreth Kusupa (35) ulikutwa ukielea katika mto Goba.
Alisema pia mkazi wa Maramba Mawili, Serafini Ameros (26) alifariki dunia baada ya kuzidiwa na maji katika karo alilokuwa akisafisha.
“Wakati Ameros akisafisha karo nyumbani kwa Damian Shayo ghafla alizidiwa na maji, Shayo aliingia kumsaidia, lakini naye alizidiwa ndipo Richard Shirima aliyekuwa maeneo hayo aliingia kutoa msaada ambaye naye pia hakufanikiwa kutokana na kuzidiwa na maji hayo hali iliyosabaisha kuita majirani kwa msaada zaidi,” alisema Kenyela.
Alisema majirani walifanikiwa kumwokoa Ameros, lakini muda mfupi baadaye alifariki dunia.
Katika tukio jingine, mkazi wa Temeke Mikoroshini, Hope Gondokewe (38) na mkazi wa Maguruwe, Zainab Codi, wamefariki dunia baada ya kugongwa na gari lisilofahamika juzi usiku maeneo ya Vetenary, Temeke.

Chanzo beltelraas.blogspot.nl

No comments:

Post a Comment