Sunday 21 April 2013

PROF LIPUMBRA ,HAKUNA MAISHA BORA TUTAENDELEA KUSOTA !!!

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema hakuna maisha bora bila Serikali kuimarisha huduma za umeme, maji, afya, usafiri na miundombinu ya usafiri. Hayo aliyasema Dar es Salaam juzi, katika mkutano wa pamoja ulioandaliwa kwa ushirikiano kati ya CUF na Chama cha siasa Redikale Venstre kutoka Denmark.

Katika mkutano huo, Profesa Lipumba alichokoza mada kadhaa zilizochangiwa na viongozi zaidi ya 130 kutoka serikalini, dini, mashirika, taasisi binafsi na wanachama kutoka vyama vyote vya siasa.

Alisema hivi sasa Serikali ilipofikia imeshindwa kutatua kero za wananchi kwa kupunguza umasikini, badala yake imebaki inaendesha propaganda zisizo na manufaa kwa wananchi wote.

Alisema ni hali ya kushangaza kwamba, Serikali kutumia kigezo kama mwananchi anatumia Sh 650 kwa siku hayumo katika kundi la umasikini.

Alisema Serikali ya CCM inapaswa kujitathmini inachokifanya kama kina manufaa kwa wananchi badala ya kuandaa mikakati mingi isiyotekelezeka.

"Palipo na watu 100, 33 ni masikini wa kupindukia wasio na uhakika wa kula wala kulala nyumba iliyo na hadhi, sasa bila kuweka mikakati ya uwekezaji mwepesi hatuweza kuondokana na hali hii.

“Napendekeza na kutoa wito kwa Serikali kuwekeza katika viwanda vyepesi, yaani vinavyozalisha nguo, ngozi na maziwa pia suala la umeme, maji, usafiri, mawasiliano, ukusanyaji wa kodi ni jambo muhimu na la kuzingatia,” alisema 

Waliochangia katika mkutano huo ni Diwani wa Kata ya Kibada, Shabani Nkumbi (CUF) ambaye alisema Serikali isiposimamia vizuri huduma kwa jamii maendeleo hayawezi kupatikana.

Naye, Seif Kombo ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino), alisema Serikali imekuwa ikiamini ushirikina lakini inajikosha kwamba haiamini wakati wanaendelea kuuawa.

Wachangiaji wengi walilalamikia Serikali kwa kushindwa kushughulikia suala la elimu, ajira, barabara, usafiri, upandaji bei wa bidhaa, afya na mambo mengine ya kijamii na kuitaka kuweka mipango madhubut.

Naye, Mratibu wa chama cha Redikale Venstre, Anemone Birkebaek alisema lengo la kushirikiana na CUF ni kutokana na sera zao kufanana na chama hicho.

Alisema amekuja nchini kushirikiana na chama hicho kuzunguka baadhi ya mikoa nchini ili kuzungumzia maendeleo na changamoto zinazowakabili wananchi

No comments:

Post a Comment