Tuesday 23 April 2013

RAIS SHEIN TUTAPAMBANA NA VITENDO VYA UVUNJIFU WA AMANI


23rd April 2013
Chapa
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema serikali yake haitavumilia vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani na umoja wa kitaifa.

Dk. Shein alitoa kauli hiyo wakati akihutubia kwa nyakati tofauti katika uwanja wa Kisonge na Vikokotoni akiwa kwenye ziara yake ya kichama kwa mikoa minne ya Unguja.

Alisema wajibu wa serikali yoyote duniani ni kusimaia sheria na katiba na kuhakikisha wananchi wake wanaishi katika mazingira ya amani kwa vile hakuna maendeleo yanayowezekana kupatikana bila amani.

Dk. Shein alisema Zanzibar imepata sifa kubwa kimataifa tangu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya pande mbili zinazounda serikali hiyo.

“Tunapimwa na Jumuiya ya Kimataifa kila kukicha, tumepata sifa na hivyo tusikitie kitumbua chetu mchanga kwa kuvusha mivutano ya kutotii sheria zilizopo kwa mujibu wa Katiba yetu,” alisisitiza Dk. Shein.

Aidha, alisema kila mwananchi anayo haki na wajibu wa kufuata chama anachokipenda, lakini suala la kutii sheria litabaki pale pale na hakutakuwa na mzaha au kumuonea mtu.

“Atakayehatarisha au kuvunja amani, serikali haitamuachia atambe, tutakabiliana naye kwa mujibu wa sheria kwa vile kazi ya serikali ni kulinda Katiba na kusimamaia sheria,” alisema.

Akihutubia katika uwanja wa Kisonge, Dk. Shein alisema safari ya uchaguzi mkuu mwaka 2015, tayari imeanza na kuwataka viongozi wa chama chake kuwa karibu na wananchi na kuhakikisha sera na Ilani ya Uchaguzi ya CCM zinasimamaiwa ipasavyo.

Hata hivyo, alisema vyama vya upinzani ambavyo vimeshindwa kuheshimu misingi ya demokrasia, ni vyema vikarudi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ili  kujifuta lakini serikali yake haitakubali kuona vokifanya siasa za ubabe, chuki na uharibifu wa mali za umma na binafsi kwa kufanya maandamano yasiokwisha ili kurudisha nyuma maendeleo.

“Hakuna serikali hata moja duniani ikiwemo na SMZ inayotaka kukandamiza wananchi wake, lakini pia hakuna serikali inayoweza kuvumilia uvunjai wa sheria ,ni lazima tujenge utamaduni wa kuheshimu sheria,” alisema Dk. Shein.

Kuhusu Muungano, Dk. Shein alisema CCM itaendelea kutetea sera yake ya mfumo wa serikali mbili na haina mpango wa mkataba au kuwa serikali tatu kwa vile siyo sera ya chama hicho.

Alisema pamoja na kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, utekelezaji wa sera unaofuatwa ni ule wa chama kilichoshinda nafasi ya urais na si vinginevyo.

No comments:

Post a Comment