Sunday 21 April 2013

WABUNGE VITI MAALUM CHADEMA WANAWAKE NI WACHUMBA !!! MOHAMMED SEIF KHATIB


LICHA ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuporomosha matusi mazito bungeni na kuachwa bila kuchukuliwa hatua, bado hawajataka kujirekebisha baada ya mbunge mwingine kuwadhalilisha mkutanoni wabunge wa Viti Maalumu wa CHADEMA.

Hatua hiyo inakuja zikiwa ni siku chache tangu wabunge wa CCM, Juma Nkamia (Kondoa Kusini) na Livingistone Lusinde (Mtera) kuwatukana wenzao wa CHADEMA wakiwaita mbwa na kwamba wana mimba zisizotarajiwa.

Pia Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba naye aliwatukana wapinzani mwishoni mwa wiki, tusi ambalo kimaadili haliwezi kuandikwa gazetini.

Matusi hayo yalionekena kumkera Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM) na kuwataka wabunge wanawake kwa niaba ya wanawake wengine wakatae vitendo hivyo.

Abdallah ambaye ni mwenyekiti wa Jukwaa la Wabunge Wanawake (Ulingo) pia alielezwa kukerwa na mifano ya Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) ya kwenye Biblia akidai inawadhalilisha wanawake.

Hata hivyo, katika hali ambayo haikutarajiwa, mbunge mkongwe wa Uzini, Mohammed Seif Khatib (CCM), alirudia mtindo ule ule wa matusi kwa kuwadhalilisha wabunge wa CHADEMA katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Morogoro jana.


Katika mkutano huo ambao ulirushwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni ya Taifa, Khatib ambaye pia ni Katibu wa Oganaizesheni ya CCM, alisema CHADEMA ina wabunge wa kuchaguliwa na viti maalumu.

Alifafanua kuwa ukiacha wale wa kuchaguliwa, wabunge wa viti maalumu walipatikana kutokana na kuwa wachumba, wake na wapenzi wa viongozi wa CHADEMA Taifa.

Khatib huku akifahamu wazi kuwa wabunge hao wamepatikana kwa utaratibu wa kikatiba ambao umeidhinishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), aliongeza kuwa CHADEMA inaongozwa na wazinzi wenye dhambi wasiofaa kwenda Ikulu.

Katika mkutano ambao kila kiongozi wa CCM aliyezungumza alitumia muda wote kuijadili CHADEMA, Khatib vile vile aliwadanganya wananchi kuwa Chama cha Wananchi (CUF) kina malengo mengine tofauti na siasa, hivyo wasihangaike kujiunga nacho kwani kina wenyewe.

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alidai CHADEMA ni wachochezi wanaopanga mikakati ya ugaidi ili kuteka watu na kuwang’oa kucha.

Katika kujenga hoja yake, Nape alimsingizia Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga kuwa ndiye aliyechochea vurugu za baada ya uchaguzi wa nchi hiyo mwaka 2007/2008 na kuua watu zaidi ya 1,300 huku wengine wakibaki bila makazi.

“Hawa CHADEMA ni kama Raila Odinga, huyu alishindwa urais mwaka 2007 na Rais Mwai Kibaki. Baada ya hapo akawachochea wafuasi wake waingie mitaani kuua watu wakati mwenzake mzee Kibaki alikimbilia Tanzania kwenye amani,” alisema.

Hata hivyo, licha ya Nape kumtaja Odinga, kauli hiyo haina ukweli wowote kwani Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) ya The Hague, Uholanzi katika uchunguzi wake kuhusu vurugu hizo Odinga si mmoja wa washukiwa wanaoshtakiwa.

Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulraham Kinana naye alitumia takribani saa nzima kwa kuichambua CHADEMA na viongozi wake akidai ni waongo na wachochozi wasio na shukrani.

Kinana alizungumzia mchakato wa katiba mpya huku akitumia hotuba ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na kudai imejaa matusi na uongo kwa viongozi.

“Hawa watu tumewalea sana, wanatukana hovyo, wamemtukana Rais Jakaya Kikwete, wameitukana CCM, Usalama wa Taifa na majaji. Wanajiona wao ndio kila kitu…hawafai kabisa hawa, ni wabinafsi,” alisema.

No comments:

Post a Comment