Tuesday 9 April 2013

POLISI ZANZIBAR HATUKUVUNJA SHERIA MTUHUMIWA WA MUUAJI !!!


Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar, Yusuph Ilembo.
Jeshi  la Polisi Zanzibar, limesema halikuvunja sheria  kwa kumshikilia kwa zaidi ya saa 24 mtuhumiwa wa mauaji ya Padri Evarist Mushi bila ya kumfikisha mahakamani.

Jeshi hilo limesema liliendelea kumshikilia mtuhumiwa huyo kutokana na kupewa kibali na Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe mjini Zanzibar.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar, Yusuph Ilembo, aliieleza Mahakama Kuu jana kufuatia ombi lililofunguliwa na wakili wa mtuhumiwa, Abdallah Juma Mohamed.

Wakili huyo anadai Jeshi la Polisi lilivunja sheria kwa kutomfikisha mteja wake mahakamani ndani ya saa 24.

Ilembo alisema kutokana na uzito wa kesi inayomkabili mtuhumiwa, Jeshi la Polisi liliamua kuendelea kumshikilia tangu walipomkamata Machi 17, mwaka huu hadi walimpofikisha mahakamani Aprili 5, mwaka huu kwa ajili ya kukamilisha taratibu za uchunguzi kabla ya kufungua hati ya mashitaka mahakamani.

"Siyo rahisi kesi kama hii kumkamata mtuhumiwa leo na kesho umfikishe mahakamani, ndiyo maana tumekaa naye zaidi ya saa 24 baada ya kupata kibali cha mahakama ya wilaya,” alisema Ilembo.
Alisema Jeshi la Polisi lilikuwa linawasiliana mara kwa mara na Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP), kwa vile ndiye mwenye jukumu la kufungua hati ya mashitaka mahakamani na kosa kama hilo halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

"Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi na tutaendelea kufanya kazi zetu kwa misingi hiyo, hivyo siyo kweli kama tulivunja sheria,” alisema Ilembo.

Awali, Wakili Abdallah Juma, katika maombi yake aliyoyafungua Mahakama Kuu, aliitaka mahakama hiyo itoe katazo dhidi ya Mkurugenzi wa Upepelezi wa Makosa ya Jinai isiendelee kumshikilia bila kumfikisha mahakamani kwa zaidi ya saa 24 kama inavyoeleza Sheria ya Jinai ya Zanzibar.

Aidha, alitaka mahakama itoe amri na imlazimishe DCI Zanzibar, kuhakikisha anafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria na mahakama itoe amri yoyote ambayo itakuwa na manufaa kwa mteja wake.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Jaji wa Mahakama Kuu, Mkusa Isaack Sepetu, alisema atatoa maamuzi kuhusiana na ombi hilo Aprili 18, mwaka huu

CHANZO beltelraa.blogspot.nl

No comments:

Post a Comment