Monday 8 April 2013

UNYAMA WA KUTISHA

*Baba anyonga watoto watatu, amtumbukiza mke kisimani
JESHI la Polisi mkoani Katavi, linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Majimoto wilayani Mlele, Justine Albert (24), kwa kosa la kuwaua kikatili watoto wake watatu kwa kuwanyonga. Baada ya kuwanyonga watoto hao, Albert aliichukua miili ya marehemu wote na kwenda kuitumbukiza kwenye kisima cha maji kilichoko jirani na kijiji hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema mauaji hayo yalitokea saa 11:30 alfajiri usiku wa kuamkia jana.

Alisema kwa muda mrefu mtuhumiwa, alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi na jirani yao na kwamba baadhi ya watoto wanadaiwa kuzaliwa nje ya ndoa yao.

Aliwataja watoto walionyongwa na baba yao, kuwa ni Frank Justine (6), Elizabeth Justine (4) na Maria Justine mwenye umri wa miezi minne.

Inadaiwa baada ya kuwanyonga watoto wake kwa zamu, alichukua miili ya Frank na Eliza akaitumbukiza kwenye kisima.

Kamanda Kidavashari, alisema Albert pia alimchukua mke wale, Jacqueline Luvika (21) na kumtumbukiza ndani ya kisima hicho ambacho kinamilikiwa na Kawaida Jonas.

“Baada ya kuona amewaua wale watoto, aliamua kumpiga mke wake kisha kumtumbukiza ndani ya kisima kile akiwa hai, lakini majirani walifika na kumtoa na hali yake ni mbaya,” alisema Kamanda Kidavashari.

Akisimulia mkasa huo, Kamanda huyo alisema kulipopambazuka baadhi ya wakazi wa kijiji hicho waliokuwa wakielekea kwenye shughuli zao, waliuona mwili wa mtoto ukiwa umetelekezwa kando ya njia na kumtambua kuwa ni Maria mwenye umri wa miezi mine, ambaye ni kitindamimba wa mtuhumiwa.

Inadaiwa ndipo walipoamua kufika nyumbani kwa mtuhumiwa na kumpatia taarifa hiyo na kuhoji alipo mama yake bila kupata majibu ya msingi.

Lakini mtuhumiwa aliwaeleza kuwa alikuwa ametoroka kusikofahamika na watoto wote.

Kutokana na maelezo hayo, wananchi hao walimtilia mashaka mtuhumiwa na kuamua kutoa taarifa kituo cha Polisi.

Baada ya polisi kwenda eneo la tukio, walikuta mwili wa Maria na kubaini ulikuwa na miburuzo ardhini na michubuko kitendo kilichowafanya wafuatilie mpaka kisimani.

Walipofika kisimani, waliamua kufungua mfuniko wa kisima hicho ndipo walikuta miili mitatu ikielea kwenye maji.

Kutokana na hali hiyo, polisi kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kuopoa miili yote, huku mama ambaye alikuwa amekunywa maji mengi akiwa taabani na kupoteza fahamu.

Kamanda Kidavashari, alisema baada ya kumuopoa mama huyo alikimbizwa kituo cha afya cha kijijini Mamba, ambako amelazwa kwa matibabu na mpaka jana mchana alikuwa hajajitambua.

No comments:

Post a Comment