Tuesday 30 April 2013

KISHINDO KATIBA MPYA ,LENGO NI ZANZIBARI KOTOKUWA NA MAMLAKA KAMILI !!!

*Jaji Warioba atangaza msimamo mzito
*Asema tume itaingilia mawazo ya wananchi 


Jaji Joseph Warioba
TUME ya Mabadiliko ya Katiba, imesema italazimika kuingilia mawazo ya wananchi, kwa kuyaacha baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa katika mchakato mzima.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Joseph Warioba alisema tume yake itaondoa mawazo yote hasi yanayokinzana na misingi ya kitaifa.

Jaji Warioba, alisema ni dhamira yake kutengeneza Katiba inayokidhi maslahi ya wananchi wenyewe, lakini pia Katiba yenye kuzingatia misingi na maslahi ya taifa.

Alitaja baadhi ya mawazo yanayokinzana na misingi ya kitaifa kuwa ni pamoja na yale yanayohusu muungano, Serikali ya majimbo, madaraka ya Rais na kinga za wabunge.

Alisema kimsingi tume yake, italazimika kuingilia mawazo ya aina hiyo na kufanya uamuzi mgumu, ili kulinda maadili na maslahi ya kitaifa.

“Katika hili naomba Watanzania watuelewe masuala haya tutayatolea uamuzi. Kama mnavyojua watu wengine walitaka Muungano wa Serikali mbili, wengine walitaka muungano wa Serikali tatu, wengine muungano wa mkataba na wengine walitaka visiwa vya Pemba na Unguja vijitenge. 

“Wengine walitaka Serikali za majimbo, wengine walizungumzia madaraka ya rais na kinga za wabunge ziondolewe, sasa masuala yanayokinzana kama haya lazima tutayatolea maamuzi magumu ili tupate muafaka.

“Lakini pia kuna baadhi ya maoni mengine tutayaacha ingawa yalijadiliwa na wananchi, tunachowaomba Watanzania wawe tayari kuyajadili kwenye rasimu itakayoletwa mbele yao.

“Kama kila kikundi kitataka mawazo yake yaingie kwenye rasimu hatutafikia muafaka, katika masuala ya msingi tutayachagua baadhi ya mawazo na mengine tutayaacha,” alisema Warioba.

Kuhusu kuvurugwa kwa uchaguzi wa mabaraza ya Katiba, Jaji Warioba alivitupia lawama vyama vya siasa na makundi ya kidini na kusema kwamba wanahusika moja kwa moja kuvuruga mchakato huo.

Hata hivyo Jaji Warioba alisema licha ya kujitokeza kwa kasoro hizo, lakini tume yake inasonga mbele kwa madai kuwa kurudia ni kuchelewesha upatikanaji wa Katiba mpya.

Alisema ni kweli uchaguzi huo ulikuwa na matatizo, lakini pale ambapo uchaguzi haukufanyika hali ilichangiwa na mivutano ya kisiasa na ile ya kidini.

“Katika baadhi ya maeneo mikutano ya uchaguzi ngazi za vijiji, mitaa na shehia ilishindwa kufanyika kutokana na mivutano ya kisiasa na kidini, wananchi walifungamanisha chaguzi hizo na masuala hayo.

“Tume tumesikitishwa na namna watu walivyojihusisha pia na vitendo vya rushwa, hivi mtu unahonga katika mabaraza ili iweje, hivi Tanzania tunakwenda wapi?,” Alihoji.

Warioba alisema, uchaguzi wa mabaraza umefanikiwa kwani viongozi na watendaji katika ngazi za vijiji, mitaa, shehia na kata walizingatia mwongozo uliotolewa na Tume na maeneo mengi wananchi walichaguana kwa amani.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, shehia 323 sawa na asilimia 96.4 kati ya shehia 335 kwa upande wa Zanzibar zimekamilisha vizuri mchakato huo, ambapo kata 3,331 kati ya kata 3339 sawa na asilimia 99.8 kwa Tanzania Bara zimekamilisha mchakato wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya Katiba ngazi ya wilaya.

Kuhusu kulalamikiwa kwa watendaji wa kata kuchakachua majina ya wagombea ambao walishinda katika ngazi za vijiji na mitaa, Warioba alishangaa kupingwa uongozi ambao tayari unatumika kuchagua viongozi.

“Wote tunajua uongozi wa WDC ndiyo mara zote unachagua kamati za maji, shule, afya, barabara na nyinginezo, lakini uongozi huo usiaminiwe wakati wa uchaguzi wa mabaraza ya Katiba.

“Sheria za Serikali za mitaa sura ya 287 na 288 Mamlaka za wilaya na miji, zinaelekeza kata kuwa na vikao vya kamati za maendeleo za kata kwa Tanzania bara. 

“Vikao hivyo hushirikisha madiwani wote wakiwemo wa viti maalum wa kata husika, wenyeviti wa vijiji/mitaa na kata husika, hawa ndio wanaoruhusiwa kupiga kura kwenye maamuzi yoyote katika kikao hicho,” alisema.

Kuhusu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutishia kujitoa katika mchakato huo iwapo Tume yake itashindwa kurekebisha kasoro zilizojitokeza, alisema:

“Sisi tutapeleka rasimu kwa kila mdau, hao wanaotaka kujitoa mimi sitaki malumbano na wanasiasa, nadhani tume haitengenezi Katiba ya vikundi bali ya wananchi,” alisema.

Jaji Warioba alisema Tume yake itaunda na kusimamia mabaraza ya watu wenye ulemavu, ili kuwapa fursa watu hao bara na visiwani kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba.

Alisema Baraza moja litaundwa Tanzania bara na jingine Zanzibar na kwamba yatashirikisha wananchi kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa.

No comments:

Post a Comment