Friday 19 April 2013

DR SHEIN AONYA ,,,AWACHE KUWADHULUMU MASHEIHA WA UAMSHO KWA KUWAWEKA NDANI BILA YA SABABU !!!

Siku ya jana alkhamis ya tarehe 18 April, 2013 ilikuwa ni siku ya dua kuwaombea ithbati na subra viongozi wetu waliowekwa rumande kwa dhulma, dhulma inayotokana na kufeli kwa mifumo mizima ya maisha iliobuniwa na mwanaadamu, mifumo hiyo ikiongozwa na "UJAMAA" na "DEMOKRASIA" za nchi za magharibi hasa Marekani, Uengereza na Ujerumani. 

Zanzibar, kama ilivyo maeneo mengi yalio na idadi kubwa ya Waislamu duniani kama vile Pakistan, Bangladesh, Saudia na hata yale yenye waislamu wachache kama vile Burma (Myanmar), hunyimwa nafasi ya kumuabudu Mola wao kama alivyowaamrisha na kusimamisha sheria ya Allah katika ardhi ya Allah, badala yake viongozi wenye majina ya kiislamu hutumika kuwakandamiza waumini kwa kuwazuia kufanya da'awa, kuwafunga, kuwadhalilisha, kuwafukuza nchini na hata kuwaua. Jambo hili hupelekea ghadhabu za Allah (S.W.T) kushuka katika ardhi bila ya kuchaguwa kati ya dhalimu na mtu wa kawaida, wote hutiwa adabu.

Amir Haji, Amiri mstaafu wa Uamsho kwa kipindi cha miaka kumi na mlezi wa jumuiya, alimuasa Rais wa Zanzibar kuwacha dhulma kwa kushirikiana na makafiri kuudidimiza Uislamu hapa nchi ili tusija tukakutwa na janga lililowakuta kabla yetu. Amir akitoa mfano wa kiongozi wa Zanzibar aliemzuia Mwalim Said Njugu kutotoa darsa na kufundisha Qur'an katka maeneo yoyote ya Zanzibar kipindi cha miaka ya 1978 ambapo Mwenyezi Mungu alishusha adhabu ya kipindu pindu na kuwakumba waliomo na wasiokuwemo. Aidha Rais Shein aliaswa kuwa kuendelea kuwaweka viongozi wa taasisi na jumuiya za kiislamu gerezani ni kufanya kazi ya makafiri kwa niaba yao.

Vile vile, waislamu wametakiwa kuendelea na harakati za kudai nchi yao bila ya woga wala khofu kwani kufanya hivyo ni kuinusuru dini yao ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiandamwa na maadui wa ndani na nje. Wale wote wanaowarejesha nyuma waislamu na kuwasaliti ni watu wanaostahiki kuangaliwa kwa jicho la tahadhari ya hali ya juu. Vile vile, waislamu wametakiwa kushikamana na Uislamu wao badala ya vyama vya siasa ambavyo havitawanufaisha mbele ya Mungu.

Baadhi ya Waislamu waliohudhuria katika dua hiyo wamisisitizwa kuwa na umoja na mshikamano wakati huu mgumu na kuwa na subira kwa yatayo wakuta pamoja na kuwapuuza wale wanaowabeza. Waumini hao wamewahakikishia viongozi wa Uamsho kuwa wapo pamoja na kamwe hawatarudi nyuma inshaa Allah.

Habari kwa hisani ya ofisi ya katibu Mkuu Uamsho.

UAMSHO MEDIA CENTER
Email: jumiki@hotmail.com
twitter: Uamsho1
facebook: Uamsho

04 Jamad Al Akhar 1434
19 April, 2013

No comments:

Post a Comment