Monday 8 April 2013

ABIRIA KULIPA NAULI KULINGANA NA UZITO WAO SAMOA


Shirika la ndege la Samoa Air katika visiwa vya Samoa, limeanza kutoza nauli ya abiria wake kutokana na uzito walio nao. Hatua hiyo imeibua hisia tofauti miongoni mwa wasafiri wa ndege kisiwani humo.
Golden-Tulip-Aeroplane-Htl.jpg
Tatizo la kuongezeka kwa unene na uzito wa watu duniani, limekuwa likiangaliwa kama ni moja ya hali inayosababisha harasa kubwa kwa jamii. Lakini hivi karibuni, katika visiwa vya Samoa, kumegunduliwa njia mbadala ambayo inaleta tija kwa jamii husika, na kutoa ujumbe ya kuwa ukiwa mnene na mzito kupita kiasi, basi kuna faida utakayoleta katika kukuza biashara ya usafiri, hususan katika swala la kutumia usafiri wa anga au ndege kama chombo cha kusafiria.
Hivyo wakazi, wanachi na wageni ambao watasafiri kutumia usafiri wa shirika la ndege la Samoa watakuwa wakipimwa uzito wao, ili kuweza kujua ni kiasi gani watalipa kutegemea na umbali wa eneo watakalosafiri ndani ya visiwa hivyo.
Moja ya mandhari ya visiwa vya SamoaMoja ya mandhari ya visiwa vya Samoa
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2011 za shirika la afya ulimwenguni, WHO, asilimia 86% ya wananchi wa Samoa wanakabiliwa na tatizo la unene na hivyo kushika nafasi ya nne duniani kwa kuwa na watu wenye uzito na unene kulinganishwa na Marekani yenye asilimia 69% Australia 61% na Japan 22%.
Akitetea uamuzi huo wa shirika la ndege la Samoa Air kuwalipisha nauli abiria kutokana na uzito walionao, Chris Langton, ambaye ni mkurugenzi wa shirika hilo alisema, "hii ni haki kwani mashirika ya ndege, yamekuwa yakisita kufanya hiyo kwa kuhofia hali ya utu wa mtu, lakini gharama za usafiri zimekuwa zikitozwa kutokana na uzito, kwani gharama za uendeshaji wa usafari wa anga umekuwa ukilipiwa kutokana na uzito siyo nafasi za viti, na abiria wetu wamekuwa wakipimwa uzito kabla ya kusafiri, japokuwa wengi wao wamekuwa wakishangaa lakini hawalipingi jambo hilo."
Akiongezea katika swala zima la kutozwa nauli huko, Langton alisema "ikiwa abiria anataka nafasi zaidi atapewa kulingana na matakwa yake, na tunahakikisha kuwa hakutokei makosa katika upimaji huo, kwani si halali kwa mtoto wa miaka 12 na 13 ambaye ana uzito mdogo kulipa nauli ya mtu mzima badala ya kulipa kutokana na uzito wake.
Abiria walalamika
Ana Fapouli abiria na ambaye ni raia wa visiwa hivyo na anayesafiri mara kwa mara kutumia usafiri huo, amesema " kupandishwa kwa nauli kutokana na uzito wa abiria kutanufaisha shirika hilo la Samoa Air kwani wameona njia ya kuongeza faida, na watakuwa na mashindano ya kibiashara na mashirika mengine mawili yanaoyotoa huduma ya usafiri wa anga kwa abiria wa wanaoingia na kutoka Samoa."
Abiria walio wanene na wazitoAbiria wanene kulipa nauli zaidi
Naye mkurugenzi mkuu wa afya wa Samoa, Palanitina Toelupe, akilizungumzia swala hili la abiria kulipa naili kulingana na uzito wao alisema "mpango huu unaweza kuwa mzuri wa kuhamasisha watu kupunguza uzito na kuwafanya wawe wanakula vyakula vyenye afya na unaleta maana, lakini kwa upande mwingine, usafiri wa anga utakuwa ghali kwa watu walio na maumbile ya unene na wazito, jambo ambalo tutalijadili tutakapokutana na viongozi wa shirika na pia nafikiria kuwa ni sehemu ndogo ya ujumbe kwa watu wapunguze uzito na unene."
Hata hivyo swala zima la kutozwa nauli kubwa kutokana na uzito wa abiria, limekuwa likiendelea tangu mwezi Novemba mwaka jana, baada ya kupewa baraka na idara ya usafiri ya Marekani, wakati lilipopitisha muswada wa kulipishwa nauli kutokana na uzito wa abiria, kwa wasafiri wote waendao visiwa vya Samoa.
Uamuzi huo wa shirika la ndege la Samoa wa kulipisha nauli kutokana na uzito wa mtu huenda ukaigwa na mashirika mengine ya ndege siku zijazo, ili kukuza kampeni ya kupunguza uzito na unene.

No comments:

Post a Comment