Tuesday 25 June 2013

UAMSHO ZANZIBAR !!!

TAARIFA YA JUMIKI KUHUSU TUKIO LA MUHADHARA WA MAHONDA TAREHE 21/06/2013 ALASIRI, JIONI

Siku ya Ijumaa tarehe 21/06/2013, askari walifika asubuhi mapema katika eneo la mahonda na kuwataka wenyeji wa wa eneo hilo kufunga maduka yao kwa kile walichokitaja kuwa hakutakuwa na muhadhara. Ilipofika majira ya saa 9:30 askari hao walifika na kuingia sehemu ya msikiti na kuwataka waislamu waliokuwa katika uwa wa msikiti huo kuingia ndani na kuanza kupachua bendera, tambara (lililokua na aya ya Mungu “walaa tahinuu walaa tahzanuu wa antumul a’launa inkuntum muuminiin) zilizokuwa zimepachikwa eneo hilo, maafisa 2 na askari 10 difenda waliendelea na vitisho vyao huku rova 4 zilizojaa askari wa FFU zikiuzunguka msikiti baada ya kuuziba mlango mkuu wa kuingilia ndani.

Mmoja miongoni mwa viongozi wa jeshi la polisi waliokuwa katika eneo hilo aliamrisha watu wapigwe mabomu na wamwagiwe maji, amri ambayo haikutekelezwa kwa wakati huo na askari waliokuwapo eneo la tukio.

Sambamba na hilo, Jeshi la polisi Zanzibar, mkoa wa kaskazini walisema uongo kwa kumdanganya Imamu wa msikiti wa mahonda kwa kumwambia kuwa wamekubaliana na kamati ya msikiti muhadhara usiwepo kitu ambacho kamati imekikanusha.

JUMIKI inatamka yafuatayo kutokana na tukio hilo:

1. Tunaalaani vikali kitendo cha jeshi la polisi - Zanzibar kuingia eneo la msikiti na kuwatisha waumini waliokusanyika kwa amani kwa lengo la kusikiliza muhadhara huo ilhali wakiwa hawajafanya fujo wala kubeba silaha ya aina yoyote.

2. JUMIKI inalaani kitendo cha jeshi la polisi - Zanzibar kuvamia eneo la msikiti na kushusha bendera tukufu ya Uislamu yenye shahada ya LAA ILAAHA ILLA ALLAH MUHAMMAD RASUULULLAH, nine ambalo ni nguzo ya kwanza ya Uislamu. Kitendo hicho si tu kinadhalilisha Jumuiya ya kiislamu ya Uamsho, bali pia kinaudhalilisha Uislamu na Waislamu kwa ujumla.

3. JUMIKI inalaani kitendo cha jeshi la polisi – Zanzibar kwa kumdanganya kiongozi wadini na kwa kufanya kazi kwa kufuata utashi wa kisiasa badala ya sheria na kanuni za kazi zao.

4. JUMIKI itaendelea na mihadhara ya kuuelimisha Umma wa kiislamu na haitatishwa na vitimbi vya watu wasiomjua Mungu wala wasioheshimu kanuni wala sheria hata zile walizozitunga wenyewe na kuzilia viapo wasivyovitekeleza.

Wabillah Taufiq

Imetolewa na:
OFISI YA KATIBU MKUU
JUMIKI, ZANZIBAR
14 Shaaban, 1434.
24/Juni/2013

No comments:

Post a Comment