Tuesday 25 June 2013

JUSSA ASEMA MAMLAKA KAMILI TU HAKUNA JENGINE !!!

Very interesting leo Mhe. Omar Yussuf Mzee alipokuwa akifanya majumuisho ya mjadala wa bajeti ya SMZ (wind-up of the budget speech) aliamua kuzinyamazia kimya na hakujibu kabisa hoja nilizozitoa jana kuhusu wizi wa mchana kweupe wanaotufanyia Tanganyika katika mafungu ya fedha za misaada ya kibajeti (GBS), fedha za mifuko ya miradi kisekta na fedha za miradi ya maendeleo zinazotoka kwa washirika wa maendeleo zinazoombwa na kutolewa kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambazo ukifanya hesabu ya Zanzibar kupewa ule mgao wa 4.5% tu basi zinafikia TShs. 163 bn. 

Ukiacha hizo kuna na zile za mikopo ya elimu ya juu ambazo kama Zanzibar ikipewa 4.5% tu kutoka SMT basi ni TShs. 14.6 bn. wakati mahitaji ya Zanzibar kuwapatia mikopo wanafunzi wote wanaoomba ni TShs. 5 bn. 

Mbali ya hizo nilihoji gawio la Zanzibar kutoka taasisi za Muungano kama TCRA, TCAA, TTCL, TPC na TPDC ambazo zinakusanya mapato na nyingine Zanzibar ina hisa kabisa lakini hakuna tunachokipata. Chukulia mfano mdogo tu karibuni Vodacom peke yake ililipa TCRA kodi ya TShs. 36 bn. Je, ukichanganya na Zantel, Tigo na Airtel mbali na tozo na ada nyinginezo.

Ukiacha hizo hata kodi ya mapato (PAYE) inayotokana na wafanyakazi wa Taasisi za Muungano waliopo Zanzibar na ambao wanatumia huduma zote za hapa zinazolipiwa na walipa kodi wa Zanzibar nazo hazilipwi sawa sawa.

Halafu anatokezea mtu anasema Zanzibar inanufaika na mfumo uliopo wa Muungano na kwamba eti tunabebwa. Nani anambeba nani hapa? Nini faida ya Muungano wa aina hii?

Ndiyo maana tunasema hatupokei chochote pungufu ya MAMLAKA KAMILI ya Zanzibar kitaifa na kimataifa. Na tutahakikisha katika rasimu ya Katiba tunayarejesha kwenye mamlaka ya Zanzibar mambo yafuatayo ili tuweze kusarifu na kupanga uchumi wetu kwa maslahi ya nchi yetu na watu wetu. Mambo hayo ni:

1. Mambo ya Nje;
2. Sarafu na Benki Kuu; na
3. Uraia na Uhamiaji.

No comments:

Post a Comment