Friday 28 June 2013

HATA BADO LAANATULLAHI BALOZI SEIF IDD !!!


MAKAMU wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd amehadharisha kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inaweza kumeguka, iwapo viongozi wataendelea kutumia vibaya majukwaa ya kisiasa kwa kutoa kauli za chuki na matusi na kukashifu Serikali kwa maslahi binafsi.

Ingawa Balozi Idd alisema uhusiano wa viongozi wakuu watatu wa nchi ni mzuri: Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na yeye Balozi Seif Ali Idd, wanafanya kazi vizuri.

Makamu wa Pili wa Rais, alikishutuma Chama cha CUF kwa kutumia majukwaa ya kisiasa vibaya. Alidai kinatumia lugha za matusi dhidi yake na kumpa majina mabaya.

Alisema kasoro kubwa zinajitokeza katika majukwaa ya kisiasa ambako viongozi wamekuwa wakitoa kauli za chuki zenye kutia wasiwasi mkubwa wananchi na kuhoji uhusiano wa viongozi hao kiasi cha kutukanana hadharani.

Akifanya majumuisho na kujibu hoja za Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliyochangia Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka ujao wa fedha juzi, Balozi Idd, alilaumu hususan viongozi wa CUF.

Maalim Seif ni Katibu Mkuu wa Chama hicho, alisema katika mikutano yao yote wanayofanya, wamekuwa wakitumia vibaya majukwaa kumtukana yeye binafsi na kumchonganisha na wananchi na Serikali iliyopo madarakani.

“Napenda kuwaambia wananchi uhusiano wa viongozi wakuu wa Serikali ni mzuri sana…lakini majukwaa ya kisiasa yanatumiwa vibaya kutukanana…Tukiendelea hivyo hatufiki pahala na tutarudi tulikotoka,” alisema Balozi Idd.

Kwa mujibu wa Makamu wa Pili wa Rais, alisema amekuwa akipewa majina mabaya na viongozi wa CUF katika mikutano ya kisiasa; likiwemo ‘LAANATULLAHI’ wakimaanisha kumlaani. Jambo ambalo alisema anawauliza “amewakosea nini”?.

Balozi Idd, aliwahadharisha viongozi hao kwamba lengo la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kuleta mshikamano kwa Wazanzibari wote.

Alionya, kwamba watu wanaweza kurudi ambako walikuwa hawazikani wala kushirikiana katika matukio kutokana na siasa za chuki na uhasama kutawala tangu ulipoingia mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

“Tuache kutukanana katika hadhara za majukwaa ya kisiasa…Hawa CUF sijui nimewakosea nini na kama majina yanachuna basi tayari ngozi yangu ingeathirika,” alisema Balozi Idd.

Alikumbusha viongozi na wananchi kwamba kilichounganishwa ni Serikali yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa, lakini vyama vya siasa na sera ni tofauti na hakuna sababu ya kulumbana katika hilo.

Awali, Waziri wa nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) iko kwenye mchakato wa kuboresha daftari la wapiga kura nchini kote.

Alitaka wanasiasa kujenga tabia ya kuwaamini watendaji wa taasisi hiyo na kuacha kuwahukumu kwa kuwashutumu, kitendo ambacho kinaweza kuzorotesha utendaji wa kazi hiyo.

“Tume hii imefanya kazi vizuri sana tangu mchakato wa kura ya maoni mwaka 2010 pamoja na kusimamia uchaguzi mkuu ambao ulikwenda vizuri na vyama vyote kuridhika,” alisema Aboud.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, iliundwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, 2010 kutokana na matakwa ya wananchi kupitia kura ya maoni na kushinda kwa zaidi ya asilimia 64.

Muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, unajumuisha Vyama vya CCM na CUF, ulifikiwa ili kuondoa siasa za chuki na uhasama katika visiwa vya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment