Wednesday 16 October 2013

UAMSHO 'HATUJABADILISHA KAULI ZANZIAR KWANZA !!!

Na Waandishi Wetu. MIEZI 12 baada ya kukamatwa na kufunguliwa kesi inayohusu mashtaka ya uchochezi na kushawishi fujo, masheikh na viongozi wa Uamsho hawajabadilika.
Viongozi hao walio chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (JUMIKI) wanaendelea na msimamo wao wa kutaka kuona Zanzibar inarejesha mamlaka yake kamili ya kujiendesha kama dola huru.
“Msimamo wangu mimi na wenzangu ni uleule. Ingawa tuna mwaka mmoja sasa tuko gerezani, tungali na msimamo wetu uleule wa kupigania Zanzibar. Hii ni nchi yetu na tuna haki ya kuitetea kikamilifu,“ anasema Sheikh Azzan Khalid Hamdan, mmoja wa masheikh hao.
Sheikh Azzan ambaye ni Naibu Amir wa Uamsho, ametoa kauli hiyo katika mahojiano maalum na Zanzibar Daima Online, yaliyofanyika nyumbani kwake Mfenesini, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, siku moja kabla ya kiongozi huyo kuondoka nchini kuelekea India kwa matibabu.
Anasema hakuna sababu ya kuonekana wao eti wameondoka kwenye malengo ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo kwa kuwa hata taasisi ya dini kama hiyo yao, inao wajibu wa kushughulikia maslahi ya wananchi.
“Si sawa jumuiya yetu kuchukuliwa kuwa imekiuka sheria za kuanzishwa kwake. Jumuiya inapaswa kuwa karibu na kujihusisha hasa na mas’ala yanayohusu haki ya wananchi,“ alisema Sheikh Azzan akiwa anajibu hoja inayotolewa mara kwa mara ndani ya Serikali na katika mazungumzo ya watu wa kawaida kwamba jumuiya ya Uamsho imevunja sheria kwa kujihusisha na harakati za kupigania mustakbali wa Zanzibar.
Anasema yeye na wenzake wanaamini kuwa hawajavunja sheria yoyote kwa sababu kama ni hivyo, Serikali ingekwishaifuta jumuiya hiyo ambayo ilisajiliwa kwa mujibu wa sheria za Zanzibar mwaka 2003.
“Wanajua kwamba hatujavunja sheria yoyote mpaka sasa. Shughuli yetu tumezifanya kwa mujibu wa sheria. Hawa watu wa Serikali wanajua kuwa tungekuwa hatuna uhalali, wangekwishatufuta kwenye usajili. Hawajafika hapo kwa sababu tupo kwenye misingi za sheria.
“Hao wanatusingizia kuhusika katika matukio ya uhalifu na matukio ya kutia watu tindikali, wanajua wanatuonea. Wanajua hatuhusiki. Nasi kwa kinywa kipana kabisa, tunasema hatuhusiki kwa namna yoyote na matukio haya ya kuchafua watu, ya kujeruhi watu kwa risasi au kwa kuwamwagia tindikali. Mara zote na kila tunapoyasikia, tunasikitika na kuwalaani kwa nguvu wale wanaoyatenda,’’ anasema.
Katika hoja kwamba watu wengi ndani ya nchi Zanzibar, ndani ya Tanzania na ulimwenguni wanainasibisha jumuiya yao na makundi mabaya ya kigaidi kama Al Shabaab, Al Qa’eda na Boko Haram, anasema ni bahati nzuri hakuna mwenye ushahidi wa mnasaba huo.
“Kuna watu wana chuki tu na sisi. Kwa sababu ya chuki zao dhidi yetu, wanasema watakavyo juu yetu. Wanatuhusisha na uhalifu unaofanywa wakati sisi tuko gerezani. Inawezekana wanaofanya wanajulikana lakini wanalindwa kwa sababu wanazozijua hao wanaowatuma. Ni chuki yao tu hawana ushahidi hata chembe wa kuhusika kwetu.
“Hata hiyo kesi waliyotufungulia, ni chuki tu waliyonayo baadhi ya viongozi. Na ndo maana nasema mimi na wenzangu tuna ujasiri wa kusema watoe ushahidi wa sisi kuhusika na matukio hayo… Hii kesi ina mwaka mzima sasa haijasikilizwa. Ni kwa sababu hawana ushahidi,’’ anasema.
Sheikh Azzan na wenzake tisa wamekuwa kwenye gereza la Kiinua Miguu, lililopo Kilimani, mjini Zanzibar wakiendelea kusota huko wakati kesi walizofunguliwa hazijapata kusikilizwa.
Wengine ni Masheikh Mselem bin Ali Mselem, Farid Hadi Ahmed, Suleiman Juma Suleiman, Mussa Juma Mussa, Abdalla Said Madawa, Fikirini Khamis Fikirini, Gharib Said, Khamis Suleiman Ali na Hassan Bakari.
Walikamatwa Oktoba 16 katika maeneo tafauti ya mjini Zanzibar, na siku tatu baadaye ndipo walipelekwa mahakamani kwa mashtaka ya kula njama ya kutenda jinai. Baadaye mashtaka yalibadilishwa na kuwa ya kushawishi watu kufanya fujo – uchochezi.
Wanatuhumiwa kuvunja Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1968 ambayo inasimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Kwa sasa wanakabiliwa na kesi mbili ambazo mashtaka yake yanafanana, moja ikiwepo Mahakama ya Wilaya iliyopo Mwanakwerekwe na nyingine mbele ya Mahakama Kuu, Vuga.
Sheikh Farid ndiye kiongozi wa Maimamu wa Zanzibar, ambaye kutoweka kwake kwa siku tatu ambako masheikh wenzake walikulalamikia ndiko chimbuko la kukakamatwa kwao.
Sheikh Farid alitoweka katika mazingira ya kutatanisha akiwa eneo la Mombasa Kwa Bakathir usiku wa siku hiyo, na akaibuka siku tatu baadaye majira yaleyale ya usiku na palepale alipokuwa amechukuliwa na watu ambao hajawahi kuwataja kwa kudai hawafahamu.
Jeshi la Polisi lilimwita na kumhoji atoe ushahidi wa madai yake kuwa alitekwa na watu wa Serikali. Alipofika kituoni Mwembemadema, yalipo makao makuu ya Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, alishikiliwa na halafu wakakamatwa masheikh wengine tisa walio ndani mpaka sasa.
Dhamana yao imezuiliwa na Mahakama kutokana na Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee, kusema wasitolewe kwa dhamana.
Ila Sheikh Azzan, yeye yuko nje kwa dhamana iliyotolewa na Mahakama Kuu wiki iliyopita ili kumwezesha kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Ombi lake ambalo lilisikilizwa na kuamuliwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, lilikuwa ni jitihada za mwisho za mawakili wake na masheikh wenzake baada ya kupata maradhi ya vijiwe kwenye figo ambayo yamemzidi gerezani kiasi cha kuanguka na kuzimia mara tano, mara mbili ikiwa ndani ya gereza.
Kabla ya hapo, alikuwa amelazwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, mjini Zanzibar. Mbele ya Jaji Makungu, mawakili waliwasilisha maelezo ya madaktari yaliyomthibitisha kuwa ni mgonjwa na hakuna hospitali ndani ya nchi inayoweza kumtibu isipokuwa kupelekwa nchini India.
Sheikh Azzan anatarajia kusafiri wiki hii kwenda India kwa matibabu ambayo anajilipia kwani serikali imesema haina uwezo wa kumpeleka haraka hivyo kwa kuwa wapo wagonjwa waliomtangulia ambao wangali wanasubiri kupatikana fedha ili wapelekwe nje ya nchi kutibiwa.
Akizungumzia maisha ya gerezani, alisema ni ya unyonge mkubwa, yasiyopendeza na yanayosikitisha.
“Angalau siku hizi kuna afadhali kidogo. Zile siku 42 za kwanza tulipoingia tu gerezani zilikuwa siku mbaya na ngumu sana. Tukiishi katika upweke na udhalilishaji mkubwa. Tulipofika tu tulinyolewa ndevu. Tukawa tunakaa mbali na watu. Kwa wiki nzima tulikuwa hatukutanishwi. Tumetengwa.
“Tukiishi katika vyumba vidogo na vya kiza. Afya zetu zimeathirika sana kwa kila mmoja na hali yake. Siku hizi angalau tunapata taarifa za yanayotokea huku nje, tafauti na siku zile tulipoingia,’’ anasema.
Alipoulizwa kama anajua kwa nini wako gerezani, labda anajua wana kesi gani, Sheikh Azzan alisema yeye hajui anashtakiwa kwa sababu gani. Anaona hawana kesi yoyote ila wamefungwa kwa sababu viongozi wametaka wafungwe.
Sheikh Azzan anasema kwa kuendelea kukaa gerezani, huduma mbalimbali za kusaidia watu dhalili walizokuwa wakizitoa zimezorota. Shughuli zao za kimaisha pia zimekufa na familia zao zimepata pigo kubwa.
“Tulikuwa tunahudumia watoto yatima zaidi ya 1,000 kupitia jumuiya yetu ya Uamsho. Hatujui wanapata vipi huduma sasa. Wengine tukiwasomesha, hatujui maendeleo yao. Baadhi wako nje ya Zanzibar, hatujui hatma zao. Wakati ule ilikuwa dhima kwetu lakini kwa sababu tumetiwa gerezani, dhima yote imemuangukia Rais Dk. Shein. Yeye anajua kwa nini sisi tuko gerezani, yeye ndo Rais anajua sababu.
“Dk. Shein tunamwambia aliapa, tena kwa kushika Mas’hafu kuwa atakuwa mwadilifu. Sasa tungependa aoneshe uadilifu, atende uadilifu. Sisi tunaendelea kukaa gerezani kwa sababu viongozi wa Serikali wameamua tu tukae ndani, hakuna ushahidi wa kesi yetu. Hawana ushahidi, wangeuleta na kesi ikaendelea. Kwa hivyo dhima anayo Rais,’’ anasema.
Sheikh Azzan anasema walichokuwa wanakipigania ni lazima kiendelee kupiganiwa na Wazanzibari kwa sababu anasema walianzisha kampeni kwa madhumuni ya kuhangaikia maslahi ya Wazanzibari ambayo yamekuwa yakidhoofishwa na watu wabaya.

No comments:

Post a Comment