Wednesday 30 October 2013

SHEIKHE MTANZANIA ATAFUTWA KENYA !!!

POLISI mjini Mombasa, wanamtafuta raia wa Tanzania, Sheikh Ramadhan Juma, kwa tuhuma za kuhubiri chuki na uchochezi wa kidini katika Msikiti wa Masjid Mussa, uliopo Mombasa, nchini Kenya. Pamoja na Sheikh Juma, pia polisi inawatafuta raia watatu wa Kenya, ambao ni washirika wa Sheikh Juma.

Sheikh Juma anatambuliwa kuwa ni kiongozi mwenye itikadi kali za kidini na anadaiwa kutoroka baada ya kuibuka kwa purukushani zilizotokea wakati polisi walipovamia Msikiti wa Masjid Mussa, Alhamisi wiki iliyopita.

Hatua hiyo ya polisi kuuvamia msikiti huo ilikuja baada ya kutokea machafuko ya kidini katika baadhi ya maeneo ya mji wa Mombasa.

Akizungumza kwa njia ya simu na RAI Jumatano jana kutoka Mombasa, Balozi Mdogo wa Tanzania mjini humo, Yahya Jecha, alisema kuwa Sheikh Juma anatafutwa na polisi kwa tuhuma za kuhamasisha waumini wa dini ya Kiislamu wa Mombasa kufanya uasi dhidi ya serikali na polisi wa Kenya.

Inaelezwa kuwa mahubiri ya Sheikh Juma yamekuja baada ya mwanzoni mwa mwezi huu kufanyika mauaji ya viongozi wawili wa Msikiti wa Masjid Mussa, ambao ni Sheikh Abou Rogo na Sheikh Ibrahim Omar.

Akizungumzia hilo, Balozi Jecha alisema kuwa polisi wa Mombasa wana wasiwasi Sheikh Juma ametoroka pamoja na waumini wengine wa Mombasa na kurudi Tanzania.

Kwa mujibu wa maelezo ya Balozi, mahubiri aliyoyatoa Sheikh Juma, yaliwahamasisha Waislamu kutorudi nyuma baada ya vifo vya viongozi wao kwa kuwataka kuingia mitaani.

“Alikuwa akiwahamasisha uasi dhidi ya polisi na kutokata tamaa na kuwaeleza hata kama Sheikh Rogo na Sheikh Ibrahim wameuawa, basi wao bado wako wengi, watalipiza kisasi,” alisema Balozi, akinukuu maneno yaliyokuwa yakitolewa na Sheikh Juma.

Balozi Jecha alisema, Ubalozi wa Tanzania unaendelea kutafuta taarifa za raia huyo wa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kujua iwapo aliingia nchini, na kwa njia zipi.

“Inawezekana kabisa bila shaka aliingia kwa kutumia hati halali ya kusafiria, lakini pia hatuna uhakika iwapo aliingia kwa njia za panya au vipi, tutatoa taarifa,” alisema Balozi huyo.

Wakati balozi huyo mdogo akitoa kauli hiyo, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, hakupatikana na taarifa zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa yuko nje ya nchi.

Wakati hayo yakiendelea, imebainika kuwa bado kuna vurugu kwenye msikiti huo na tayari Baraza la Maimamu la mjini Mombasa limeufunga Msikiti wa Masjid Mussa, hadi pale suala la usalama litakapotengemaa.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani nchini humo, Aggrey Adoli, mwishoni mwa wiki iliyopita alitoa wito kwa kiongozi huyo kujitokeza mwenyewe ili kutoa maelezo ya kilichotokea msikitini hapo.

“Tunataka kuweka ubinadamu mbele kwa kumuomba kiongozi huyo wa kidini ajipeleke polisi kwa hiari na kutoa maelezo bila kutulazimisha kutumia njia nyingine kumkamata,” alisema.

Hata hivyo, kauli ya juzi ya Adoli ya kumtaka sheikh huyo Mtanzania ajitokeze mwenyewe polisi inatofautiana na ile aliyoitoa Jumamosi kwa kusema kuwa kikosi cha kupambana na ugaidi kilimkamata mhubiri huyo na kuondoka naye mara baada ya kujitokeza nje ya msikiti huo.

Sheikh Juma anaelezwa kukubalika na idadi kubwa ya Waislamu mjini Mombasa, ambapo wafuasi wake waliamua kupambana na polisi muda mfupi mara baada ya swala ya Ijumaa.

Watu watano walikamatwa kufuatia purukushani hizo na walitarajiwa kufikishwa mahakamani jana.

No comments:

Post a Comment