Tuesday 29 October 2013

MAALIM SEIF AMPONDA MWENYEKITI WA ZEC!!!

Chama Cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa  Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, hana sifa za kushika wadhifa huo.

Akizungumza na wanachama na wapenzi wa CUF katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Pwepweu Tumbe, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema Jecha ni mkereketwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba kwa mazingira hayo hataweza kutenda haki katika chaguzi.

Maalim Seif alidai kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Jecha aliingia katika mchakato wa kugombea ubunge katika Jimbo la Kwamtipura kupitia CCM, lakini alishindwa.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar aliibua hoja hiyo baada ya kuwapo taarifa kuwa takwimu za wapiga kura wapya katika majimbo matano ya Unguja zimepotea kwenye kompyuta, na kudai kuwa huo ni mkakati maalum ulioandaliwa na CCM kwa kushirikiana na ZEC.

Ameyataja majimbo yanayodaiwa kupoteza takwimu zake za wapiga kura wapya kuwa ni Bumbwini, Donge, Kitope, Bububu na Mfenesini.

Maalim Seif alimtaka mwenyekiti huyo ajiuzulu wadhifa huo na kama akishindwa basi Rais wa Zanzibar achukue jukumu la kumfuta kazi.

“Kwa kweli huyu (Jecha) hana sifa kabisa za kuwa Mwenyekiti wa ZEC kwa sababu ni mkereketwa wa CCM aliyegombea nafasi ya ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2010, hawezi kabisa kutenda haki katika uchaguzi,” alisema Maalim Seif na kuongeza:

“Kwa hivyo namuomba sana mwenyekiti huyu ajiuzulu, na kama akishindwa basi kwa heshima zote namuomba Rais Dokta Shein amwajibishe kwa kumfuta kazi.”
Jana mwenyekiti huyo alipotafutwa kuzungumzia madai hayo hakupatikana. Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim, alisema kuwa Jecha alikuwa katika kikao.

Hata hivyo, mmoja wa maofisa waandamizi wa ZEC alisema waandishi wa habari wanaweza kuandika watakavyo.

Rais Shein alimteua Jecha kushika nafasi hiyo mwishoni mwa Aprili mwaka huu.
 

No comments:

Post a Comment