Friday 29 March 2013

JAJI ATOWA TAMKO ZITO KESI YA UAMSHO

 Mzee Ibrahim, kuwasilisha kwa maandishi sababu za kufunga dhamana ya viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) ndani ya wiki mbili kuanzia jana.

Agizo la mahakama hiyo lilitolewa jana na Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Fatma Hamid Mahmoud.
Jaji Fatma alitoa uamuzi huo baada ya kukamilisha kusikiliza pande mbili kuhusu hatua ya dhamana ya washtakiwa hao 10 kufungwa na DPP kwa kutumia sheria ya Usalama wa Taifa ibara ya 19 (3) d sura ya 47 ya mwaka 2002.

Jaji Fatma alisema kwamba baada ya kupitia kumbukumbu za mwenendo wa kesi ya msingi, anaona upande mmoja dhamana imefungwa, lakini bado upande wa pili anaona dhamana iko wazi dhidi ya washtakiwa hao.

“Upande wa DPP muwasilishe kwa maandishi sababu zenu kwa nini washtakiwa wasipewe dhamana ndani ya wiki mbili,” alisema Jaji Fatma.

Aidha, alisema kwamba dhamana ni haki ya mshtakiwa na hatua ya kutolewa sababu ya dhamana hiyo kufungwa itaisaidia mahakama kupata mwongozo mzuri kabla ya kutoa uamuzi. Kuhusu kesi ya msingi, Jaji Fatma alisema kwamba itaendelea kusikilizwa kama kawaida licha ya upande wa mashtaka kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kupinga uamuzi wa Jaji Abraham Mwampashi juu ya uamuzi wake wa kufuta maamuzi yote yaliyotolewa na Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar na kuungana na uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka wa kufunga dhamana.

“Pamoja na upande wa mashtaka kukata rufaa bado hakuzuii Mahakama Kuu kusikiliza kesi ya msingi na tutaendelea kama kawaida baada ya kupokea sababu za DPP kufunga dhamana ya washtakiwa,” alisema Jaji Fatma.
Alisema kwamba suala la kukata rufaa ni haki ya msingi ya kila mtu kikatiba na kwamba hakuna sababu za msingi za kesi hiyo kusimama kusubiri maamuzi ya mahakama ya juu.

Kutokana na hali hiyo, Jaji aliutaka upande wa mashtaka uwasilishe kwa maandishi hoja za DPP kabla ya kesi hiyo kutajwa tena April 10, mwaka huu.
Awali Mwendesha Mashtaka kutoka ofisi ya DPP, Raya Mselem Issa, alidai kwamba taratibu za kukata rufaa tayari zimekamilika na kuomba mahakama kutojadili ombi la dhamana na kuitolea uamuzi hadi Mahakama ya Rufaa itakapotoa uamuzi wake.

“Ombi letu kesi isimamishwe hadi Mahakama ya Rufaa itakapotoa mwongozo, rufaa tuliyoikata kwa ajili ya kupinga maamuzi ya Jaji Mwampashi ya Machi 11, mwaka huu,” alidai Mselem. Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka tayari umekwisha kutaarifu mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Kesi hiyo inawahusu viongozi 10 wa Uamsho akiwamo Sheikh Farid Hadi Ahmed, Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, Azzan Khalid Hamdan, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakari Suleiman, Gharib Ahmada Omari, Abdallah Said Ali na Fikirini Majaliwa Fikirini.

Washtakiwa hao wamefunguliwa mashtaka ya uharibifu wa mali za serikali na kuhatarisha usalama wa taifa kinyume cha kifungu cha 3 (d) cha sheria ya Usalama wa Taifa sura ya 47 ya mwaka 2002 na kutoa lugha za uchochezi kinyume cha kifungu cha 11 cha sheria ya Usalama wa Taifa sura ya 47 ya mwaka 2002.
CHANZO::belteirass.blogsport.nl

No comments:

Post a Comment