Sunday 31 March 2013

ANAYEDAIWA KUMUUA PADRI MUSHI KIZIMBANI KESHOKUTWA




ALIYEKUWA mgombea wa uwakilishi jimbo la Rahaleo, Unguja kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) Omar Mussa Makame (37) atafikishwa mahakamani Aprili 2, mwaka huu kwa tuhuma za kumuua Padri Everistius Mushi wa Kanisa la Romani Katoliki, Zanzibar.

Mwanasiasa huyo alikamatwa na maafisa wa upelelezi, kufuatia taarifa za siri na baadae kutambuliwa mara mbili katika gwaride maalum ambalo liliwahusisha watu walioshuhudia mauaji hayo Februari 17, mwaka huu Kisiwani humo.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Hamad Masoud Hamad alithibitisha kuwa Makame ni mwanachama wa chama hicho na alikuwa mgombea wao katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Rahaleo yanaonyesha kuwa Omar (CUF) alipata kura 2310 ambapo mgombea wa CCM Nassor Salum Ali alipata kura 3952:

“Taarifa za kukamatwa Omar ni mpya kwa upande wetu kama Chama cha siasa, tukio lenyewe kiuhalisia halina uhusiano na Chama chetu,”alisema Masoud ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar, kabla ya kujiuzulu mwaka jana.

Hata hivyo, Masoud alisema kwamba kama Chama cha siasa, kitakaa na kumjadili kwa kina hatimae kitatoa msimamo wake kuhusiana na tukio hilo.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema jalada la uchunguzi wa kesi hiyo tayari limekabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) na siku ya Jumanne ijayo, atafikishwa mahakamani.

Alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa Mwanakwerekwe shehia ya Mwanakwerekwe mbali na shughuili za siasa ni fundi seremala.

Alisema mchoro wa mtu huyo anayedaiwa kuhusika na tukio hilo uliwasilishwa Polisi kabla ya kukamatwa kwake, hatimae kutambuliwa katika gwaride maalumu.

Wakati huohuo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kwa upande wake kimesema kukamatwa kwa watu wanaoshukiwa kuwahujumu viongozi wa Dini kutaondoa hali ya wasiwasi kwa wananchi na waumini wa madhehebu ya Dini mbalimbali, Zanzibar.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC (CCM) Zanzibar, Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu alisema wananchi walianza kupoteza imani na vyombo vya usalama wa raia kutokana na mfululuzo wa matukio bila ya wahusika kukamatwa.

CHANZO beltelraas.blogspot.nl

No comments:

Post a Comment